Miswada miwili iliyopitishwa na Bunge katika kikao kilichopita, imeshatiwa saini na Rais Jakaya Kikwete na sasa imekuwa sheria kamili.
Kauli hiyo ilitolewa Bungeni na Spika wa Bunge, Bw. Samuel Sitta, wiki iliyopita.
Alisema katika kikao kilichopita, Bunge lilipitisha miswada miwili ambapo mmoja unaitwa Bank of Tanzania Act Number 4 of 2006 na mwingine ni Banking Financial Institutions Bill Number 5 of 2006.
’’Miswada hii ilipelekwa kwa Rais kwa utaratibu wa kikatiba ili ipate kibali chake. Baada ya kupitia taratibu zote za kuchapisha, ninayo furaha kuwaeleza kuwa Mheshimiwa Rais ametoa kibali chake kuwa miswada yote miwili iwe sheria,’’ alitangaza Bw. Sitta.
Pia, Spika alisema bunge hili ambalo lilianza kikao chake Jumanne wiki iliyopita litaahirishwa Agosti 15, mwaka huu.
Kazi zilizofanyika wiki iliyopita ni uzinduzi wa ukumbi mpya wa Bunge, uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete na kilichofuata ni hotuba za Waziri wa Mipango, Dk. Juma Ngasongwa na Waziri wa Fedha, Bi Zakia Meghji.
Bunge hili lina jumla ya wabunge 319, ambapo 273 ni wa CCM na wabunge 45 ni wa vyama vya upinzani vya CUF, CHADEMA, TLP na UDP. Mbunge mwingine mmoja ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali.