SERIKALI imeokoa zaidi ya dola za Marekani milioni 650, sawa na sh bilioni 700 zilizopangwa kutumika kwa ajili ya kununulia gesi nje ya nchi.
Fedha hizo za serikali zimeokolewa baada ya serikali kuanzisha mradi wa Songas ulioko katika Kisiwa cha Songas kilichopo Kilwa. Gesi hiyo imesaidia matumizi ya viwandani na majumbani.
“Awali serikali ilikuwa ikiagiza gesi hiyo kutoka nje ya nchi, lakini sasa inapata gesi hiyo kutoka katika Kisiwa cha Songosongo.”
Hii ni kauli ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi. Mwakapugi alitoa kauli hiyo wakati anawasilisha taarifa yake kwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alipokuwa katika ziara ya kutembelea mradi wa gesi wa Songas, ulioko Kilwa, mkoani Lindi, wiki iliyopita.
Mwakapugi alisema fedha hizo zilichangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa umeme wakati wa matatizo ya ukame ambayo yalijitokeza kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita.
“Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Shirika la Umeme (TANESCO), Songas na Kampuni inayozalisha gesi ya Pan Africa, inaendelea na mpango zaidi wa kukuza uchumi kupitia gesi hiyo, ambapo wameamua kwa pamoja kusafisha gesi asilia kutoka mita za ujazo milioni 70 hadi 140 kwa siku,” anasema Mwakapugi.
Anasema katika kuhakikisha mita hizo za ujazo zitaweza kuzalisha mitambo hiyo, gesi hiyo itaweza kutosha na kukidhi mahitaji ya kuzalisha umeme katika mitambo iliyopo.
Gesi asilia, imesaidia kupatikana kwa umeme viwandani, hivyo kusaidia kukuza uchumi kutokana na uzalishaji wa uhakika wa viwandani.
Akielezea historia ya gesi hiyo kwa Waziri Mkuu, Mwakapugi alisema gesi ya Songas iligunduliwa mwaka 1974 katika Kisiwa cha Songosongo kilichopo katika Mkoa wa Lindi, Wilaya ya Kilwa, na walianza na uchimbaji wa kisima kimoja.
Anasema mwaka 1976, walichimba visima viwili na uchimbwaji wa visima hivyo ulikuwa ukiendeshwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC) na Pan Africa Energy.
Pan Africa Energy kwa kushirikiana na TPDC wameingia mkataba katika kuhahakisha kuwa mradi huo unakuwa na unafuu kwa Watanzania.
Kwa wakazi wa Dar es Salaam, tayari mradi huo umezaa matunda kwa kuzalisha umeme majumbani katika eneo la Ubungo, na pia Kilwa katika Kisiwa cha Songosongo.
Anasema hadi kufikia mwaka 1983, shirika hilo lilichimba visima tisa, na sasa wanatarajia kuongeza idadi nyingine ya visima ili kukidhi mahitaji ya Watanzania katika matumizi ya gesi viwandani.
Anasema gesi hiyo, itachangia kukuza uchumi kwa kuwa itazalisha umeme katika kipindi cha ukame endapo utatokea kwani hakuna haja ya kutegemea umeme unaotokana na maji ya mvua.
Naye Rais wa Kampuni ya Pan Africa Energy, Peter Clutterbuck, anasema kwa kushirikiana na wadau wa TPDC, kampuni yao itahakikisha uchumi wa Tanzania hauyumbi kwa kukosa umeme.
Hata hivyo Clutterbuck anasema kampuni yake imewekeza katika mradi huo kwa asilimia 100, hivyo utawanufaisha Watanzania kulingana na mahitaji yao katika kukuza uchumi.
Anasema wanakijiji waliozungukwa na mradi huo, watafaidika kwa kuwa watakuwa na umeme saa zote kwa kuchangia fedha kidogo, ukilinganisha na wenzao wa mbali.
“Hata hivyo kuna miradi ya kijiji ambayo tumeweza kuwachangia na kuwaendeleza, kwa mfano, zahanati imejengwa mpya, shule zimejengwa, na kuna mpango wa kuwaendeleza wanakijiji hao kwa kuwa mradi huo umewazunguka,” anasema Peter.
Anasema kwa sasa wanapeleka gesi hiyo Dar es Salaam, eneo la Ubungo, lakini wana mpango wa kupeleka gesi yenye futi 90 endapo mpango wa kusafisha kisima kimoja cha SS9, utakamilika.
Alisema kwa sasa kuna baadhi ya visima ambavyo vinatoa gesi ndogo kutokana na kutosafishwa lakini baada ya kusafishwa visima hivyo vitakuwa na uwezo wa kutoa gesi nyingi na kukidhi mahitaji ya Watanzania, ikiwa ni pamoja na kukuza uchumi wa nchi.
“Endapo tutazalisha gesi kwa wingi itakuwa ni neema kwa Watazania na jamii, kwa kuwa tatizo la umeme majumbani na hata viwandani litapungua na uchumi utakua,” alisema Peter.