Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Umeme huu tunaamini hautakuwa mzigo tena
Umeme huu tunaamini hautakuwa mzigo tena
By Habari Tanzania | Published  02/27/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

MOJA ya habari kubwa katika vyombo vya habari leo hii, ni ile inayohusu kuruhusiwa kuanza kazi kwa kampuni binafsi ya kuzalisha umeme ya Artumas.

Mkataba kati ya Artumas moja ya kampuni zilizoingia mkataba na TANESCO, ulitiwa saini jana na Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (EWURA), jijini Dar es Salaam.

Mkataba huo unasainiwa wakati huu taifa likipita katika kipindi kisicho cha kudumu cha neema kubwa ya mvua iliyotoa matumaini ya mabwawa ya kuzalisha umeme kufanya kazi vizuri kiasi cha lile la Mtera kulazimika kutapishwa.

Ingawa katika jicho la haraka haraka, mkataba huo unaonekana kutokuwa na umuhimu mkubwa katika kipindi hiki, lakini ni ukweli ulio wazi kwamba, kama taifa tuna kila sababu ya kuwa na vyanzo mbadala vya kuzalisha umeme.

Tunasema hivyo tukiwa na kumbukumbu ya machungu makubwa ambayo yalilikumba taifa hili kwa kipindi kirefu mwaka jana, wakati sehemu kubwa ya nchi ilipokumbwa na giza.

Kwa kuwa tunatambua kuwa mvua za kudra zinazozaa maji yasiyodumu si jambo la kutegemea sana, tunauona mradi huu wa Artumas uliotengwa huko Mtwara na utakaotumia gesi kuzalisha megawati 18 za umeme, kuwa unaolitakia mema taifa hili.

Kwa sababu hiyo basi, ni imani yetu kwamba, Artumas wanaingia katika orodha ya wazalishaji umeme binafsi, wakija kulisaidia taifa hili, badala ya kuwalazimisha Watanzania wasiozidi asilimia 10 wanaotumia umeme kuingiza mifukoni zaidi ya ilivyokuwa awali.

Ni imani yetu kwamba, serikali yetu imeingia mkataba na Artumas ikitambua kuwa mradi huo kwa vyovyote hautakuwa mzigo mwingine kwa taifa hili ambalo sekta ya nishati ni moja ya maeneo yaliyojaa uchafu wa kila namna.

Ni imani yetu kwamba, maneno yenye ujumbe mzito ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya AG&P Power Ltd, Peter Gathercole ambaye kampuni yake inaiendesha Artumas ni ya dhati na yanayolitakia taifa hili mafanikio baada ya kupita katika vipindi vingi vyenye machungu.

Kauli yake kwamba, Watanzania wana kila sababu ya kuitumia gesi asilia waliyonayo kwa manufaa yao, ni ya kutia moyo.

Sisi tunasema ni maelezo ya kuridhisha, hasa kwa kutambua hali ya sasa ya nusu giza ambayo imekuwa ikilikabili taifa na kusababisha kuzorota kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Lakini pia tunaiona ahadi hiyo kuwa ni ya matumaini kutokana na ukweli kwamba, kadri siku zinavyosonga mbele, tatizo la umeme limeendelea kuchukua sura ya usugu na ya kukatisha tama, hususan nyakati za ukame ambazo huja bila ya taarifa.

Pamoja na matarajio hayo makubwa ya Watanzania, ni imani yetu kwamba, serikali itafanya kila linalowezekana ili kuhakikisha kuwa, ahadi za kutafuta nishati mbadala zinafikiwa kwa kuweka mbele maslahi ya taifa.

Tukiwa ni sehemu ya Watanzania wanaokabiliwa na mtihani mgumu wa kugharamia umeme ghali kutokana na mikataba mibovu ya siku zilizopita, tunaamini Serikali ya Awamu ya Nne haitakubali tena kuifanya sekta ya nishati kuendelea kuwa ni kichwa cha mwendawazimu.

Ingawa tunajua kwamba Artumas wamekubali kuja kusaidia sekta ya nishati wakiwa na uhakika wa kupata faida, bado tunaamini makubaliano mwafaka yaliyofikiwa yatatuwezesha kukipata kile ambacho Waingereza wanakiita Win-Win Situation, yaani ushindi kwa kila mhusika.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.