Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Hali si shwari Muhimbili
Hali si shwari Muhimbili
By Habari Tanzania | Published  02/27/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu

HALI ya mambo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) si shwari, baada ya menejimenti ya sasa ya hospitali hiyo, kuanza kufumua kashfa za ulaji fedha, uliokuwa ukifanywa na uongozi uliopita.

Uchunguzi wa Tanzania Daima unaonyesha kuwa, hatua hiyo ya menejimenti, imewaweka katika hali ya wasiwasi baadhi ya wafanyakazi wa hospitali hiyo, waliokuwa na maamuzi makubwa ya matumuzi ya fedha katika menejimenti iliyopita.

Tayari uongozi wa juu wa hospitalini hapo, umekwishapiga marufuku kuonekana katika maeneo ya hospitali, gari la wagonjwa (Ambulance) lililonunuliwa na uongozi uliopita.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya MNH, vililieleza gazeti hili kuwa, marufuku hiyo inatokana na kile kilichodaiwa, kuwepo kwa mianya ya rushwa katika tenda ya ununuzi wa gari hilo.

Kwamba menejimenti ililikataa gari hilo baada ya kuchunguzwa na kugundulika kuwa si jipya, halina ‘microphone’, kiyoyozi, mashine ya oksijeni na kitanda cha mashine cha kupanda na kushuka kwa ajili ya wagonjwa mahututi.

Habari zaidi kutoka Idara ya Utawala ya MNH, zinaeleza kuwa, menejimenti imeagiza kufanyika kwa uchunguzi wa kina wa utaratibu uliotumika kuagiza gari hilo, baada ya kubainika kuwa lina upungufu wa vifaa muhimu vinavyotakiwa kuwemo.

Zilisema, katika uongozi uliopita, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, January Karungula, aliidhinisha mpango wa kununuliwa kwa gari jipya la kubebea wagonjwa, lenye thamani ya shilingi mil. 100.

Kwamba katika mpango huo, MNH walitenga fedha za kununua magari matatu, moja likiwa ni Ambulance ya kisasa, na mengine mawili kwa ajili ya shughuli za kawaida za hospitalini hapo.

“Kikao cha Julai 10 mwaka jana, uongozi ulieleza kuwa, una mpango wa kununua magari matatu, mawili yakiwa Land Cruiser na moja Ambulance kwa ajili ya matumizi ya hospitali, lakini Ambulance limeleta utata mkubwa,” alisema mmoja wa viongozi wa MNH ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Alisema kwa muda mrefu hospitali hiyo imekuwa haina gari la kubebea wagonjwa na yanayotumika kwa kazi hiyo, hayana viwango vinavyotakiwa.

“Pamoja na kuwa Muhimbili ni hospitali ya taifa, haina gari la wagonjwa, yanayotumika ni magari ya kawaida tu, hayana ving’ora wala microphone.

“Muhimbili inazidiwa na manispaa za Temeke, Kinondoni na Ilala ambazo hospitali zake, zina magari mazuri ya kubebea wagonjwa, haya ya hapa Muhimbili hayawezi kutoa msaada wowote nje ya hospitali,” alisema.

Taarifa za hivi karibuni zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa, menejimenti imekuwa katika wakati mgumu baada ya wakala aliyeiuzia MNH gari hilo kugoma kulipokea mara mbili, na kulirudisha katika viwanja vya hospitali ambako limeegeshwa mpaka sasa.

Zinaeleza kuwa, wakala huyo amegoma kulipokea gari hilo kwa sababu kabla ya kuliagiza aliuandikia barua uongozi wa MNH, akiutaarifu kuwa pesa iliyotolewa kwa ajili ya kununua gari hilo ni kidogo.

Taarifa zinaeleza zaidi kwamba, kiongozi mmoja wa MNH alimwandikia barua wakala huyo, akimruhusu kununua gari lolote linaloweza kupatikana kwa kiasi cha pesa kilichotolewa.

“Tulisikia kuwa pesa iliyotengwa kwa ajili ya gari hilo ni shilingi milioni 100, lakini inasadikiwa kuwa manunuzi ya gari hilo ni kati ya shilingi milioni 60 na 70, ndio maana gari lililoletwa halina ubora unaotakiwa,” alisema mtumishi mmoja wa Idara ya Uhasibu, aliyeomba jina lake lisichapishwe gazetini.

Hata hivyo Mkurugenzi wa MNH, Prof. Leonard Lema, alipoulizwa jana kwa njia ya simu kuhusu hali hiyo, alikanusha na kueleza kuwa gari hilo ni zima wala halijazua utata wa aina yoyote.

Alisema bado halijaanza kutumika kwa sababu wanakamilisha taratibu za kuliandika ubavuni na kuliwekea kitasa maalumu kwa ajili ya usalama.

Lakini habari za uhakika zilizolifikia Tanzania Daima jana zinaeleza kuwa, Prof. Lema anasita kueleza ukweli kwa sababu anahofia kibarua chake.

Habari hizo zilieleza kuwa, Prof. Lema ndiye aliyeibua suala hilo, lakini analifanyia kazi kwa siri kwa sababu amekwishaonywa na baadhi ya wajumbe wa bodi kutojiingiza katika mambo yaliyofanywa na mwenzake aliyemtangulia.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.