Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kiti cha marehemu Akukweti kichungu
Kiti cha marehemu Akukweti kichungu
By Habari Tanzania | Published  02/27/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Happiness Katabazi

MWENYEKITI wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, amefungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu ya Tanzania, akitaka mahakama hiyo isitishe maandalizi ya uchaguzi mdogo katika Jimbo la Tunduru kwa kuwa unakwenda kinyume cha Katiba na maamuzi ya mahakama.

Kesi hiyo namba 19 ya mwaka 2007, ilifunguliwa jana saa nane mchana katika Mahakama Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, Mtikila, anadai kwamba tamko la mdaiwa wa kwanza (Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)), ambaye alitamka hivi karibuni kwamba wagombea binafsi hawaruhusiwi kushiriki katika uchaguzi katika jimbo hilo ni batili. Anadai kuwa tamko hilo linakwenda kinyume na Ibala 20(4), 21(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hati hiyo inaeleza kwamba tamko la maamuzi ya Mwenyekiti wa NEC la kukataa raia na wakazi wenye chini ya umri wa miaka 18 na kuendelea kutowaandikisha kwenye daftari la muda la wapiga kura kabla ya kufanyika kwa uchaguzi, ni uvunjaji wa Ibala ya 21(1) ya Katiba na kifungu cha 13 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 1985, ambayo tayari imefanyiwa marekebisho.

Mtikila ambaye anatetewa na Kampuni ya uwakili ya Mpale Mpoki, anadai kwamba endapo uchaguzi huo utafanyika, utakuwa umewanyima haki ya kupiga kura zaidi ya wakazi 11,552 wa Tunduru, ambao mwaka juzi walikuwa na umri wa miaka 16 na 17.

Kwamba wakazi hao hawakuandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura lakini mwaka huu, wametimiza miaka 18 na hawataruhusiwa kupiga kura.

Februari 17, mwaka huu, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Lewis Makame, alitoa tamko la kuzuia kuwapo kwa mgombea binafsi katika uchaguzi huo pamoja na kuwapo maamuzi ya Mahakama Kuu.

Alikaririwa akisema kuwa maamuzi ya mahakama yametangaza tu ibara za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinazotaka wagombea kupendekezwa/ kuteuliwa na vyama vya siasa tu, zinakiuka ibara nyingine ya Katiba hiyo ambayo inatoa haki kwa raia wote kushiriki katika kuchagua au kuchaguliwa, ili kushiriki katika shughuli za utawala.

Jaji Makame, alisema maamuzi hayo yanaielekeza serikali kuandaa utaratibu wa kisheria kuwezesha wagombea binafsi kushiriki katika chaguzi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Mwenyekiti huyo wa NEC alisema, kwa mujibu wa Ibara ya 30(5) ya Katiba, ina maana kuwa sheria isiyoruhsu ushiriki wa wagombea binafsi itaendelea kuwa halali/kutumika mpaka muda uliotolewa na Mahakama Kuu utakapokwisha au serikali itakapofanya marekebisho katika sheria na kuruhusu wagombea binafsi kushiriki katika chaguzi mbalimbali.

Hata hivyo, Mtikila ambaye ndiye alishinda kesi ya mgombea binafsi mwaka jana, alisema mahakama haifanyi kazi kwa kupiga ramli, hivyo hoja ya serikali kwamba ina nia ya kukata rufaa ni hoja isiyo ya msingi na kuwataka kuiacha mahakama ifanye kazi yake.

Wakati Mchungaji Mtikila akielekea mahakamani kuomba kusitishwa kwa uchaguzi huo, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Makamba, yuko tayari Tunduru ili kuhakikisha chama chake hakipotezi kiti hicho.

Makamba alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari wiki iliyopita akitamba kuwa, anakwenda Tunduru kuongoza mashambulizi dhidi ya vyama vya upinzani.

Alisema makada wa timu ya kampeni wa chama chake wamejipanga vizuri hivyo wana uhakika wa kuibuka na ushindi dhidi ya vyama vya upinzani na wagombea wao.

Aidha, Makamba alisema kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, John Malecela, naye yuko njiani kwenda Tunduru kwa ajili ya kuimarisha timu ya kampeni.

Wakati huo huo, mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Shaibu Akwilombe, jana alipata ajali akiwa katika heka heka za kampeni hizo.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Tunduru, Akwilombe alisema ajali hiyo ilitokea wakati akiwa njiani kutoka Kijiji cha Matemanga, akielekea Kijiji cha Lilunga.

Alisema ajali hiyo ilitokea baada ya gari aina ya Prado, mali ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, alilokuwa akitumia katika safari zake za kuomba kura kuserereka katika kokoto na baadaye kupinduka mara mbili.

Akwilombe ambaye alikuwa ndani ya gari hilo alisema hakuumia, bali dereva wa gari hilo, ambaye alipata majereha sehemu za mgongoni na huenda akafanyiwa operesheni.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.