NI siku tano zimebaki kabla ya wawakilishi wa Tanzania Bara kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga, ikwaane na mabingwa wa Angola, Petro Atletico.
Hii ni mechi itakayofanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Machi 2 hadi 4 mwaka huu, ikiwa ni mechi ya awali ya raundi ya pili ya michuano hiyo.
Hadi kufika hatua hiyo, Yanga iliwafunga mabingwa wa Comoro, AGSM kwa mabao 5-1, katika mechi iliyochezwa pia kwenye Uwanja wa Taifa.
Ushindi huu, ulitosha kuivusha Yanga hadi raundi ya pili kutokana na kushindwa kufanyika kwa mechi ya marudiano ambayo kikanuni, ilipaswa ifanyike Comoro.
Hata hivyo, Yanga ikawa imejihakikishia tiketi ya raundi ya pili ya michuano hiyo, kutokana na kukosekana kwa uwanja wenye hadhi ya kimataifa nchini Comoro.
Mazingira haya, yalitosha kuipa Yanga fursa zaidi ya kujiandaa kwa mechi ya kwanza ya raundi ya pili dhidi ya Atletico iliyoifungasha virago Civic FC ya Namibia.
Hata hivyo, wachezaji wanane wa Yanga wakawa miongoni mwa msafara wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, nchini Brazil.
Awali, Yanga walilalamikia hali hii kwa hoja kuwa, hali hiyo inatibua mtiririko wa kocha wa timu hiyo, Mserbia, Sredojovic Milutin ‘Micho’.
Pamoja na hayo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), likawahakikishia viongozi wa Yanga kuwa, wachezaji hao watakwenda nchini Brazil, lakini watarejea mapema zaidi kabla ya mechi ya Ligi ya Mabingwa.
Akiwa na timu visiwani Zanzibar siku kadhaa zilizopita, Micho amekaririwa akizidi kulalamikia wachezaji wake walioko Stars.
Wakati hali ya mambo ikiwa hivyo, mwishoni mwa wiki, TFF ilisema wachezaji wa Yanga ambao awali, walikuwa warejee jana, watakawia kwa sababu zilizo nje ya uwezo.
Hii ilizidi kumchanganya Micho na viongozi wa Yanga kwa ujumla, kwani kwa mujibu wa TFF, uhakika wa wachezaji hao kurejea ni Machi mosi.
Tukiwa sehemu ya wadau wa soka na maendeleo kwa ujumla, ni wazi hali hii inaweza kuleta hofu, hasa ikizingatiwa wachezaji wanane walioko Brazil, ni kati ya wachezaji muhimu.
Pamoja na hayo, hatudhani kama ni sahihi kwa viongozi na kocha wa Yanga kuwa na hofu katika kipindi hiki kifupi kabla ya mechi hiyo.
Kweli, wachezaji wanane walioko Stars ni muhimu katika kikosi cha Yanga, lakini kukawia kwao au hata kukosekana, kusiwachanganye Yanga kwa kipindi hiki.
Tunayasema haya, kwa kuzingatia kuwa mbali ya uwezekano wa wachezaji hao kuiwahi mechi hiyo, pia wachezaji waliopo wanapaswa kujengwa kuwa wanaweza.
Kitendo cha kocha na viongozi wa Yanga kuwa na hofu, kunawafanya wachezaji waliosalia kujiona hawawezi kushinda bila nyota walioko Stars.
Hii ni sumu mbaya kwa wachezaji waliosalia, kwani kama nyota walioko Brazil hawatafika hadi siku ya mechi, Yanga itakuwa imefungwa kabla ya mechi kisaikolojia.