SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), inaangalia uwezekano wa kuagiza kuku kutoka nchini Mauritania ili kukabiliana na uhaba wa nyama ya kuku visiwani hapa.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Maliasili, Rahama Mshangama, aliliambia gazeti hili hivi karibuni kuwa, kamati ya kupambana na mafua ya ndege Zanzibar, imeagiza kuangaliwa uwezekano wa kuingizwa kuku wa nyama kutoka Mauritania.
Mshagama alisema mpango huo umefikiwa katika kikao cha kamati hiyo, chini ya Mwenyekiti wake Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha.
“Kamati imeagiza uangaliwe uwezekano wa kuingiza kuku kutoka Mauritania, kwa kampuni ambayo itathibitika uzalishaji wake unakidhi haja.
“Kampuni itakayochaguliwa, itahusika na kuingiza kuku mama. Na imeagizwa kuwa kampuni zitakazoruhusiwa ni zile zinazojihusisha na kuzalisha vifaranga vya kuuza,” alisema Mshagama.
Alisema chini ya utaratibu huo, kampuni maalumu itateuliwa na itaingiza kuku hao baada ya kupata kibali maalumu kutoka serikalini.
Mshangama alisema njia itakayotumika kusafirisha kuku hao kutoka Mauritania, itafuatiliwa kwa karibu ili kuhakikisha viwango vya ubora vinazingatiwa katika upatikanaji wa bidhaa hiyo.
Katibu Mkuu huyo alisema kamati imetoa wiki tatu kukamilishwa kazi ya kuangalia kampuni kutoka Tanzania Bara zitakazoruhusiwa kuingiza vifaranga kwa wafugaji wa Zanzibar.
Kuku na mayai kutoka Tanzania Bara walizuiwa kuingizwa Zanzibar zaidi ya mwaka mmoja sasa kufuatia habari za kuibuka kwa ugonjwa wa mafua ya ndege.
Marufuku hiyo iliathiri kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa kuku visiwani hapa, na idadi kubwa ya wafugaji waZanzibar walianguka kiuchumi.
Baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza katika kikao chao na maofisa wa SMZ katika Ukumbi wa Rahaleo, walisema kuwa uamuzi wa serikali kupiga marufuku uingizaji wa kuku na mayai kutoka Tanzania Bara umewasababishia hasara kubwa.
Walilalamika kuwa, wamechukua mikopo ya benki na taasisi nyingine za fedha kwa ajili ya kufanya biashara hiyo, lakini wameshindwa kuirejesha baada ya kupigwa marufuku kuku kutoka Tanzania Bara.
Baadhi ya wafanyabiashara na wafugaji, walilalamika kuwa, hawaoni sababu ya msingi za kupigwa marufuku kuku na mayai kutoka Tanzania Bara wakati hakuna kesi yoyote ya maradhi ya homa ya mafua ya ndege iliyoripotiwa.
Walidai kushangazwa na msimamo wa viongozi wanaosisitiza marufuku hiyo, huku wenyewe wakiwala kuku wa upande wa Tanzania Bara wanapokuwa Dar es Salaam au sehemu nyingine ya Tanzania Bara kwa shughuli zao mbalimbali.