MSAFARA wa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, juzi ulipata ajali ukiwa njiani kutoka eneo la Ngurero, mkoani Kilimanjaro kuelekea Monduli, mkoani Arusha.
Ajali hiyo ilitokea saa 11:00 jioni baada ya gari la abiria aina ya Toyota Hiace, lenye namba za usajiri T476 AAT kuligonga gari la polisi aina ya Volks Wagen lenye namba za usajiri STH 1746, lililokuwa likiongoza msafara wa magari ya waziri mkuu.
Habari zilizopatikana kutoka eneo la tukio zilieleza kuwa, chanzo cha ajali hiyo ni kitendo cha dereva wa Hiace inayofanya safari kati ya Arusha mjini na Usa River kupiga kona ghafla kuukwepa msafara wa waziri mkuu, ambaye alikuwa akitokea Moshi katika mazishi ya aliyepata kuwa Mangi Mkuu wa Wachaga, Thomas Marealle (92), aliyefariki dunia zaidi ya wiki moja iliyopita.
Watu walioshuhudia tukio hilo walieleza kuwa dereva huyo ambaye jina lake halikupatikana mara moja alipiga kona kali ghafla baada ya kusikia ving’ora vya polisi vinavyoashirikia kuwapo kwa hali ya tahadhari barabarani.
Tukio hilo lilisababisha, ‘kigofu’ hicho cha polisi kilichokuwa kikiongoza msafara wa Lowassa kuligonga kwa nyuma basi hilo dogo la abiria.
Mara baada ya tukio hilo, majeruhi kadhaa waliohusika katika ajali hiyo walikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.
Daktari Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk. Naftali ole King’ori, alisema waliojeruhiwa ni Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Damas Cornel Mzambwe, Sajenti Otto Silvanus Basil na Sajenti Froliani, ambaye alitibiwa na kuruhusiwa kuondoka.
Taarifa zinaeleza kwamba, mara baada ya ajali hiyo, dereva wa Hiace alitoroka kutoka eneo la tukio na kukimbia, na hadi jana alikuwa akiendelea kutafutwa.
Kumekuwa na matukio kadhaa ya ajali yanayohusisha misafara inayokwenda kasi ya viongozi wakuu wa kitaifa katika vipindi tofauti.
Miaka ya mwanzo ya 1990, msafara wa Ali Hassan Mwinyi wakati huo akiwa Rais, ulipata ajali katika makutano ya barabara za Chang’ombe na Mandela Express jijini Dar es Salaam na kusababisha kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Polisi wa Kituo cha Chang’ombe.
Mwaka 2000 wakati wa kampeni, msafara wa Benjamin Mkapa aliyekuwa akipigania kuingia ikulu kwa kipindi cha pili, ulipata ajali mkoani Mwanza na kusababisha vifo vya watu kadhaa, baada ya basi moja lililokuwa limeegeshwa pembeni eneo la mlimani kukatika breki na kuanza kuporomoka kwa kasi.