Wabunge leo wanaanza mjadala wa siku tano kujadili Bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha wa 2006/7 mjadala unaoelekea hautakuwa na mvutano mkubwa.
Hii inatokana na Bajeti iliyowasilishwa na Waziri wa fedha Bi. Zakia Meghji kuwavutia wengi na kuwa mwelekeo wa kugusa maeneo mengi muhimu.
Bajeti hii ya Waziri Meghji ambayo baadhi ya vyombo vya habari imeiita Bajeti ya Mama inaweza kupita bila mikwaruzo na hivyo Bi. Meghji kupeta kiulani tu.
Baadhi ya wabunge waliozungumza baada ya Waziri Meghji kuwasilisha Bajeti hiyo, walielezea waziwazi kufurahishwa kwao na Bajeti hiyo.
Wengi walisema imejibu ahadi za Rais Kikwete alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka jana ikiwemo falsafa yake ya ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya.
Katika kampeni hizo, Rais Kikwete, alikaririwa mara kwa mara akisisitiza kuwa, iwapo atachagu-liwa, atahakikisha maisha bora kwa kila Mtanzania.
Wabunge hao walieleza bayana kuwa, Bajeti ya mwaka wa fedha wa 2006/7, imegusa karibu maeneo yote aliyoahidi Rais Kikwete wakati wa kampeni zake za kuwania nafasi hiyo.
Lakini, wabunge hao walisema changamoto kubwa iliyo mbele, ni kuhakikisha kwamba, Bajeti hiyo inatekelezwa kama ilivyoanishwa ili kweli maisha bora kwa kila Mtanzania yaweze kufikiwa.
Mmoja wa wabunge wa kambi ya upinzani ambaye alielezea mtazamo wake juu ya Bajeti hiyo ni Bw. John Cheyo (UDP-Bariadi Mashariki).
Bw. Cheyo, maarufu kama Bwana Mapesa, alisema Bajeti hiyo imegusa maeneo mengi na hivyo kujibu ahadi za Rais Kikwete alizozitoa wakati wa kampeni.
Moja ya maeneo aliyosema kuvutiwa Bw. Cheyo ni namna bajeti ilivyotengwa kwa ajili ya sekta ya kilimo ambayo karibu asilimia 80 ya Watanzania, wanaitegemea.
Mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 chini ya vyama vingi vya siasa, ilikuwa kama desturi kwa wabunge wa kambi ya upinzani, kutoka nje ya Bunge wakati wa kupitisha bajeti kama ishara ya kutokubaliana nayo.
Safari hii inaelekea haitakuwepo hasa ikizingatiwa kuwa Rais Jakaya Kikwete mwenyewe alikutana na wabunge wam pande zote za CCM na upinzani kwa nyakati tofauti kabla ya kusomwa Bajeti ya mwaka huu.
Baadhi ya wachunguzi wa masuala ya siasa, wamelezea kuwa, kitendo hicho cha Rais Kikwete kukutana na wabunge wa kambi ya upinzani, kinaweza kusaidia kupunguza ’makali’ ya hoja za wabunge wa kambi hiyo.
Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Rais kupanga kukutana na wabunge wa kambi ya upinzani katika kipindi kama hiki cha Bajeti.
Mjadala huo unakuja baada ya Bunge kuahirishwa tangu ilipowasilishwa Bajeti Bungeni Alhamisi iliyopita.
Mbali ya Wabunge kujadili Bajeti, pia watachangia hotuba ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2005 na Mwelekeo wa Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2006/7, iliyowasilishwa na Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Dk. Juma Ngasongwa.
Kabla ya kujadili hotuba ya Waziri wa Fedha, kutakuwa na maoni ya Kamati ya Bunge ya Uchumi na Mipango juu ya bajeti hiyo, yatakayosomwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk. Abdallah Kigoda.
Baada ya Dk. Kigoda, Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Fedha, Bw. Hamad Rashid Mohamed ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, pia atataoa maoni ya kambi hiyo kuhusiana na bajeti.
Kitakachofuata baada ya hapo ni michango kutoka kwa wabunge mbalimbali, ambapo wamekuwa wakitafakari hoja hizo mbili kwa makini, kwa muda wa siku tatu sasa.
Akiahirisha Bunge siku ya Alhamisi, Spika wa Bunge Bw, Samuel Sitta, alitangaza kuwa hoja hizo mbili zitajadiliwa leo.
’’Ni utaratibu wetu kujadili kwa pamoja Hoja ya Wizara ya Uchumi na Mipango na ile ya Wizara ya Fedha. Hivyo hoja hizi mbili zitaanza kujadiliwa kwa pamoja siku ya Jumatatu.” alisema Spika.
Hivyo, Spika aliomba wabunge wanaotaka kuchangia hoja hiyo wapeleke majina yake kwake.
Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Luteni Yusuf Makamba, anatarajiwa kuapishwa Bungeni kesho (Jumanne), baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, kuwa Mbunge wa kuteuliwa.
Luteni Makamba ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa miaka mingi na amewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
Pia amewahi kuwa mkuu wa Wilaya kadhaa nchini.
Na katika hatua nyingine, Rais wa Filand, Bw Tarja Halonen, anatarajiwa kulihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katikati ya wiki hii.
Hata hivyo, habari zilizopatikana mjini hapa, hazikufafanua siku ambayo Rais Halonen atawasili hapa nchini.