Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Tujiulze, tunachohitaji ni sifa ya kuitwa wasomi?
Tujiulze, tunachohitaji ni sifa ya kuitwa wasomi?
By Habari Tanzania | Published  02/25/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
Na Yahya Charahani

HAIWEZEKANI kupuuza jitihada zote za serikali inazofanya kuwezesha kuanzishwa kwa chuo kikuu kipya kitakachowezesha kuchukua wanachuo 40,000 huko Dodoma.

Haiwezekani, pia kusema kuwa eti serikali haikufanya jambo la maana kuweza kufikia uamuzi huu mzito ilhali sekta ya elimu ya juu imekuwa ikididimia.

Pia, haiwezekani kupuuza jitihada zingine zozote za kujaribu kuonyesha nia njema japo kwa kauli tu kuanzisha vyuo vikuu vingi kadri inavyowezekana.

Lakini, inawezekana kuhoji na vile vile kuwa na shaka shaka sana hasa kama uamuzi huu unakuja wakati kile kitu tulicho nacho kinatushinda na tena kinakaribia kutushinda kabisa.

Hivi kwa akili ya kawaida kabisa Watanzania hivi sasa tunajisikiaje tunaposikia kilio cha wadogo zetu na watoto wetu huko katika taasisi za elimu ya juu wakilalama kutopata mikopo ipasavyo, kulala mzungu wa nne au wanane wanane ndani ya chumba kimoja, kufeli mitihani yao kwa kutokuwa na wahadhiri wa kutosha?

Iwapo wanachuo wasiozidi 10,000 wanatutoa jasho katika kuwapa hiyo mikopo ambayo imepewa jina maarufu siku hizi kuwa ni ni asilimia 40 inakuwaje hao 40,000 tunaofikiria kuwa nao huko Dodoma?

Tunasikia pia taarifa za wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma katika vyuo vikuu na taasisi nyingine nchini Ukraine, wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha na ambao sasa wanapanga kwenda katika ubalozi wa Uingereza nchini humo kuomba misaada ya kibinadamu, ikiwemo chakula na mahali pa kujihifadhi.

Wanafunzi hao wamekumbwa na hali hiyo ngumu ya maisha baada ya kufukuzwa katika vyuo walivyokuwa wakisoma baada ya kushindwa kulipa ada kwa muda mrefu, huku pia wakikosa fedha za kujikimu kwa ajili ya chakula na mahitaji mengine muhimu.

Tunazo pia taarifa za wanafunzi wa vyuo vikuu vingine nchini, kikiwamo kile kikongwe cha Dar es Salaam wanavyohangaishwa pia na tatizo la malazi yasiyokidhi haja zao na pia masomo nusu nusu.

Siyo hivyo tu, bali pia tunatambua changamoto kubwa zinazotukabili tena kwa kasi mbele yetu, kubwa ikiwa ni utandawazi, lakini nyingine ni hii ya shirikisho linaloharakishwa la Afrika Mashariki.

Jamani, hivi Watanzania tunaangukia wapi iwapo tunaharakisha shirikisho, tunaingia utandawazini na kisha elimu yetu ndiyo tunaiweka rehani namna hii?

Ingekuwa na maana sana tungeweza kulenga katika kupata elimu bora, tena ya kiwango kinachoridhisha na chenye ushindani ili kukabiliana na changamoto zote zinazotukabili.

Tungeweza kuanza kwa kuwaandalia vijana wetu wahadhiri wa kutosha, mikopo inayokidhi haja zao na angalau malazi ya maana hata kama ni kuwashirikisha wananchi waliopo pembezoni mwa taasisi zetu hizi.

Ingawa kwa baadhi ya mitazamo ya watu inaweza kuonekana si vyema kuwa na mrengo wa kuhakikisha unaimarisha kidogo ulicho nacho na kisha ndiyo uchukue kikubwa zaidi, lakini kama ningekuwa mimi ningechagua wazo la kuimarisha vyuo vyetu vikuu tulivyo navyo kwanza.

Tunachokiona sasa hivi tunaweza kuwa tunajisifu tuna matawi mengi tena ya vyuo vikuu vingi, lakini kumbe kimsingi uwezo tulio nao ni wa kuwa na vyuo vikuu vitatu au vinne tu na si kingine zaidi hapo.

Sababu kubwa ya kulizungumzia hili ni kwamba hivi vyuo vingi vikuu vinavyoanzishwa vinaanzishwa kwa mgongo wa vyuo vikuu vitano, kwa maana kwamba wahadhiri wa vyuo hivyo ndiyo wanaovisimamisha hivi vingine.

Maana ya hii ni nini? Ni kwamba tutakuwa tunapata wahitimu au ma-graduates walioiva nusu nusu na ambao hawataweza kamwe kujisaidia wao wenyewe na hata jamii inayowazunguka, watakuwa wame-graduate kwa sifa tu, lakini kiuwezo hakuna lolote.

Sasa, Watanzania tusiwe waoga, tutoke mbele, tujiulize hivi tunachokitaka ni kuwa na ma-graduate wa majina tu, au tuna lengo la kukisaidia kizazi cha sasa na hata cha baadaye, kwa maana kwamba hawa ndiyo wanapaswa wawe kichocheo cha utafiti, uvumbuzi, ugunduzi na utoaji wa huduma kwa jamii?

Kwa hali inavyokwenda ninafika mahali ninahofia kwamba tunaonekana kana kwamba tunalenga tuwe na watu wetu wengi ambao tunataka waitwe graduates, lakini kwa hali halisi ya mambo hawajiwezi.

Kwa msimamo na mtazamo huo, kwa hakika nadiriki kusema kwamba hatutakuwa tumefanya kitu. Ni sawa na kutwanga maji kwenye kina.

Tutambue kwamba tunahitaji maandalizi kuanzia sasa tunapoingiza asilimia 75 ya waliofaulu darasa la saba, tukumbuke kuwa na high school nyingi, bora zenye walimu, hatimaye wahadhiri wa vyuo vikuu.

*Yahya Charahani ni Kaimu Mhariri wa Mwananchi Jumapili. Anapatikana kwa email:charahani@yahoo.com Gazeti Tando: charaz.blogspot.com"


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.