Na Salma Said
MKUU wa Kituo cha Huduma za Sheria cha Zanzibar , Profesa Haroub Othman amesema kumekuwepo na ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu Zanzibar unaofanywa na wananchi wenyewe.
Alisema ofisini mwake Kibokoni mwishoni mwa wiki kuwa ukiukwaji huo umefikia asilimia 60 na unahusu kutofuata sheria za nchi na baadhi yao kufanya vitendo vya ukatili.
Alisema ipo haja ya kukemewa kwa nguvu zote vitendo hivyo ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakichukua sheria mikononi mwao bila ya kuzingatia sheria za nchi zilizopo.
“Vitendo vingi vya uvunjwaji wa sheria pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu unafanywa na wananchi kwa asilimia 60, tena kwa makusudi,” alisema Profesa Othman.
Aliongeza kwamba tabia ya kuwapiga watuhumiwa na wakati mwingine kuwachoma moto ni vitendo vya ukatili na havifai katika jamii na ipo haja ya kukemewa na kupigwa vita kwa nguvu zote.
Profesa Othman alisema mbali ya asilimia 60 ya wananchi wanaovunja haki za binaadamu na kutotekeleza sheria za nchi, asilimia 40 iliyobaki inatendwa na vyombo vya dola, ikiwamo polisi.
Aliongeza kuwa askari polisi, baadhi yao hujichukulia sheria mikononi mwao, kuwabambikizia kesi zisizokuwa na msingi, kuwatesa raia na kuwatia ndani bila ya kosa lolote.
Msomi huyo aliongeza wakati mwingine polisi hufanya makusudi kwa kumtia ndani raia siku ya Ijumaa huku wakijua kwamba siku inayofuata, Jumamosi na Jumapili hakuna kazi na hivyo kumwachia Jumatatu bila ya hata kumfikisha mahakamani, jambo ambalo linakiuka katiba.
Alisema kutokufahamu sheria za nchi kunasababisha wananchi wengi kukosa haki zao za msingi pamoja na kukoseshwa haki hizo ikiwemo hiyo ya kuwekwa ndani siku kwa tatu bila ya kufunguliwa mashtaka na kukutana mtu anafurahia kuachiwa baada ya siku tatu bila kufunguliwa mashtaka, lakini bila kujua kwamba haki yake imepotezwa.
Alisema wakati umefika sasa kwa wananchi kujua heria za nchi, ikiwemo somo la katiba kufundishwa darasani kwa kuingizwa katika mitaala ya masomo katika shule zote nchini kama ilivyo kwa nchi nyengine zilizoendelea, hasa za Ulaya ili wananchiwaweze kufahamu wajibu wao pamoja na kujua haki zao.
Alisema tangu kuanzishwa kwa kituo hicho miaka 15 iliyopita, amebaini kwamba wananchi wengi hawajui haki zao za msingi za kikatiba na hivyo hupoteza au kudhulumiwa haki zao na vyombo vya dola.
Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume anatazamiwa kufungua semina itakayowakutanisha wataalamu wa sheria kutoka katika nchi mbalimbali za Afrika ya Mashariki na Kati itakayofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Bwawani ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 15 ya kuanzishwa kwa kituo hicho.