Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Dar yazima mzuka wa Waanglikana
Dar yazima mzuka wa Waanglikana
By Habari Tanzania | Published  02/25/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

Na Simon Berege
KWA kipindi cha wiki nzima iliyopita masikio ya watu wengi yalielekezwa Dar es Salaam, Tanzania kutaka kujua nini kitatokea kwenye mkutano mkuu wa maaskofu wakuu wa Kanisa la Anglikana duniani uliokuwa ukifanyika Hoteli ya Whitesands.

Mkutano huo, ambao ni mara ya kwanza kwake kufanyika nchini ambao ulianza Februari 15 hadi 19, chini ya mkuu wa kanisa hilo, Askofu Mkuu wa Canterbury, Dk Rowan Williams, ulikuwa na mambo mengi yaliyozua mvuto wa kipekee.

Kwanza, ni namna ulivyofanyika, wajumbe wake, mvutano uliokuwepo, kati ya vikundi vya wanaharakati wanaotetea ushoga na usagaji na wale wanaopinga, usiri wa mkutano na hata idadi ya vyombo vingi vya habari vya kimataifa vilivyofika kuripoti mkutano huo.

Kitu kikubwa zaidi ni kutokana na ukweli kwamba mkutano huo ulikuwa muhimu na nyeti kutokana na kugusa mustakabali wa kanisa hilo lenye waumini zaidi ya milioni 77 duniani ambao wanakabiliwa na mgawanyiko unaosababishwa kwa kiasi kikubwa na msimamo wa uongozi wa Kanisa la Marekani unaounga wazi wazi mkono vitendo vya ushoga na usagaji na kushabikia ndoa za watu wa jinsia moja.

Maaskofu wakuu 37 kati ya 38 walihudhuria mkutano huo ambao chini ya busara za Askofu Mkuu wa Canterbury, Dk Williams aliyekuwa mwenyekiti wa mkutano huo na mwenyeji wao, Askofu Mkuu Dk Donald Mtetemela, mkutano huo ulishuhudia pia kuwapo kwa askofu pekee mwanamke, Katherine Jefferts Schori, kutoka New Hampshire, Marekani.

Maaskofu wengine waliohudhuria mkutano ni, Askofu Mkuu wa Australia, Dk. Phillip Aspinall, Michael Baroi (Bangladesh), Mauricio Andrade (Brazil), Bernard Ntahoturi (Burundi), Andrew Hutchison (Canada)na Bernard Malango wa Afrika ya Kati.

Walikuwapo pia, Askofu Mkuu, Martin de Jesus Barahona (Marekani ya Kati), Dk. Dirokpa Fidele (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), Paul Kwong (Hong Kong), James Ernest (Indian Ocean), Alan Harper (Ireland), Nathaniel Uematsu (Japan) na Mouneer Anis wa Yerusalem na Mashariki ya Kati.

Pia, orodha hiyo ilikuwa na Askofu Mkuu Benjamin Nzimbi (Kenya), Francis Park (Korea), Sir Ellison Pogo (Malaysia), Carlos Touche-Porter (Mexico), Samuel San Si Htay (Myanmar-Burma), William Turei (New Zealand), Peter Akinola (Nigeria) na Dk. Alexander Malik wa Pakistan, James Ayong (Papua New Guinea) na Ignacio Soliba (Philippines).

Wengine ni, Emmanuel Kolini (Rwanda), Dk. Idris Jones (Scotland), Dk. John Chew ( Asia Kusini Mashariki), Badda Sugandhar (India Kusini), Njongonkulu Ndungane wa Afrika Kusini, Gregory Venables (Southern Cone), Henry Luke Orombi (Uganda), Justice Akrofi (Afrika Magharibi), Drexel Gomez (West Indies) na John Sentamu (York, Uingereza, ambaye ana asili ya Uganda.

Askofu Schori, ambaye aliingia Tanzania na Afrika kwa mara ya kwanza alikuwa gumzo si ndani ya mkutano huo, bali katika kanisa hilo kutokana na sababu kuu mbili.

Kwanza, yeye ndiye mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo mkubwa wa uaskofu mkuu nchini Marekani na pili ni msimamo wake wa kutetea waziwazi mashoga, wasagaji na kubarikiwa kwa ndoa za jinsi moja.

Siku ya kwanza ya mkutano huo, Dk Williams alikutana na maaskofu wakuu wapya kisha kuwakumbusha majukumu yao ndani ya kanisa.

Mkutano huo ulitoa mwaliko rasmi kwa maaskofu watatu kutoka Marekeni, Robert Duncan, Christopher Eptino na Bruce Mc-Person ambao waliwasilisha mada ambazo zilikuwa na mitazamo inayokinzana.

Wakati Askofu Duncan (mwenye msimamo mkali) alilishauri kanisa kudumisha utamaduni na misingi ya kale kwa kutoruhusu ndoa za watu wa jinsia moja, kutokuruhusu wanawake kuwekwa wakfu kuwa maaskofu, Askofu Eptino (mliberali), yeye alitaka kanisa likubali mabadiliko kulingana na wakati, kuruhusu mashoga kwa kuwa Yesu hana ubaguzi na watu wote ni wana wa Mungu. Kwa upande wake, Askofu Mc-Person mwenye msimamo wa wastani (moderate) alikuwa na hoja zisizounga wala kupinga upande wowote.

Mgawanyiko ndani ya kanisa hilo ulianza rasmi mwaka 2003 baada ya Kanisa la Marekani (Episcopal Church) lilipoamua kumsimika Gene Robinson, mtu aliyekiri kuwa ni shoga kuwa askofu akiwakilisha jimbo la New Hampshire.

Askofu Robinson, awali alikuwa na ndoa halali, akiishi na mkewe kwa miaka 20 kabla hawajaachana na kisha yeye kuingia katika mahusiano ya kimwili na mwanaume.

Moto au tatizo hilo lilichochewa zaidi mwaka jana baada ya kusimikwa kwa Schori kuwa Askofu Mkuu wa Marekani ambaye mbali na kupingwa kutokana na kuwa mwanamke, amekuwa na msimamo wa kuunga mkono mashoga, wasagaji ndani ya kanisa hilo.

Kutokana na hali hiyo, maaskofu kutoka Afrika na Asia wamekuwa hawakubaliani na msimamo huo na mabadiliko ndani ya kanisa.

Mmoja wao, Askofu Mkuu wa Nigeria, Peter Akinola ambaye amekuwa msemaji wa majimbo 22 ya kanisa hilo katika Afrika ambayo yamefuta kabisa au kwa kiasi fulani kupunguza uhusiano wao na kanisa la Marekani baada ya uamuzi wa kumpa uaskofu Robinson.

Askofu Mkuu Akinola ni kiongozi mwenye msimamo na ushawishi mkubwa, kutokana na ukweli kwamba nchi yake ndiyo waumini wengi, kiasi cha 17.5 milioni, idadi ambayo ni kubwa ikizizidiwa tu na Uingereza. Takwimu zinaonyesha kwamba Marekani inao waumini 2.4 milioni.

Kutokana na msimamo huo, ikafika wakati wanaharakati ndani ya kanisa hilo, wale wanaopinga mabadiliko wakajiimarisha kwa kuunda chombo kilichojulikana kama Global South Network.

Mvutano mkubwa, hata kabla ya mkutano wa Dar es Salaam uliongezeka zaidi baada ya hatua ya Askofu Mkuu Akinola kumsimika, Martyn Minns, Mmarekani kuwa Askofu wa Nigeria anayeratibu majimbo ya Marekeni yanayotaka kujitenga na Kanisa la Marekani.


Moja ya mambo yaliyokuwa kivutio na kutawala safu za vyombo vya habari vya ndani na nje wakati wa mkutano huo ni kuwepo kwa vikundi vya wanaharkati watetezi wa ushoga ndani ya kanisa na wale wanaopinga vitendo hivyo.

Wanaharakati hao, ambao nao waliopiga kambi na kupata malazi katika hoteli ya Whitesands, wakiwemo waliotoka kwenye taasisi mahsusi za kupigania haki zao, wanaoandikia majarida na tovuti za mashoga na wasagaji waliuchangamsha na kuupa changamoto mkubwa huo.

Kwa upande wa wale waliokuwa wakitaka kukubalika kwa waumini hao ndani ya kanisa, alikuwemo Mkurugenzi wa taasisi inayojiita Changing Attitude kutoka nchini Uingereza, Mchungaji Colin Coward, taasisi ambayo inahamasisha mabadiliko chanya ya kimtazamo juu ya ushoga. Pia, alikuwapo mkurugenzi wa taasisi hiyo nchini Nigeria, Davis Mac-Iyalla.

“Nimetoka Nigeria kuja kukutana na Askofu Akinola kumuomba abadili msimamo wake wa kuwachukia mashoga, kule ni vigumu kuonana naye… sasa wanataka kuanzisha sheria inayokataza ushoga na usagaji isingekuwa rahisi kuonana naye,” alieleza Mac-Iyalla ambaye anaeleza wazi kuwa yeye ni shoga.

Naye Mchungaji Caroline Hall ambaye pia ni mwandishi wa jarida la Integrity la California, Marekani linaloandika habari za kuwatetea mashoga na wasagaji alisema kuwa alikuwa nchini ili kuwafanya maaskofu watambue kwamba msimamo wao si wa utani, bali unatoka moyoni.

“Tunataka watuone kwa sura kwamba tupo hapa kutetea wenzetu, hatuoni sababu ya kutengwa kwa baadhi ya watu fulani wakati Yesu mwenyewe tunayemwamini ni wa watu wote,” alieleza mchungaji huyo mwanamke ambaye amekiri kuwa ni msagaji aliye kwenye mahusiano wa kimapenzi na mwanamke mwenzie kwa miaka 15 sasa.

“Sitokwenda Zanzibar yanipasa kurudi California, maana Jumatano (21.02.2007) natakiwa kuendesha ibada muhimu huko,” akaeleza Mchungaji Hall na kubainisha kwamba amekuwa na hali ya kupenda watu wa jinsia yake tangu akiwa mdogo.

Mwanaharakati mwingine, Mchungaji Scott Gunn kutoka Marekani wa Kanisa la Inclusion, akaeleza kwamba ujio wake ni kujaribu kushawishi viongozi wa kanisa kutoa suluhisho litakalonufaisha makundi yote (win- win solution) ili kanisa lisimeguke.

“Cha msingi, Waanglikana waangalie jambo gani lina uzito kati ya Yesu Kristo anayewaunganisha na nguvu ya jambo linalotaka kuwatenganisha,” alieleza Scott ambaye muda mwingi alikuwa na mashoga hao. Anakiri kuwa yeye mwenyewe si shoga, ila hapingi ushoga.

Kwa mujibu wa imani, sakramenti takatifu au komunio katika kanisa ni moja ya alama muhimu inayowaunganisha waamini kuwa kitu kimoja. Sakramenti hiyo, huchukuliwa kuwa ni mwili halisi wa Yesu Kristo, ambao unaliwa kwa imani kupitia divai na mkate kama ishara ya malipizi ya dhambi zao kutokana na Yesu aliyekufa msalabani.

Sakramenti hii ambayo huitwa kwa majina mbalimbali, kama vile Komunio, Meza ya Bwana, Ekaristi na Ushirika Mtakatifu huonyesha umoja na mshikamano.

Hilo halikufanyika katika mkutano huo, ambako maaskofu saba katika kuonyesha msimamo wao dhidi ya Askofu Schori, maaskofu wakuu saba wenye msimamo mkali walikataa kushiriki Meza ya Bwana wakati wa mkutano huo. Wakiongozwa na Askofu Mkuu Akinola, viongozi hao walieleza wazi wazi msimamo huo..

Wakarejea msimamo huo kwamba katika mkutano wao uliofanyika mwaka 2003, maaskofu 14 waligomea Meza ya Bwana. Msimamo huo, ulikuwa kupinga kusimikwa kwa Gene Robison kuwa askofu.

Walipofanya ibada wakiwa ziarani Zanzibar, ambako Askofu Mkuu Akinola wa Nigeria hakwenda, maaskofu watatu walikataa kushiriki Meza ya Bwana. Ibada hiyo ilikuwa mahsusi kwa kumbukumbu ya miaka 200 ya kutokomezwa kwa biashara ya utumwa.

Maaskofu waliogomea chakula hicho ni, Askofu Mkuu, Dk John Chew wa Kusini Mashariki ya Asia, ambae pamoja na kulisha wengine, yeye aliendelea na msimamo wake wa kugomea chakula hicho.

Askofu Mkuu Schori alikuwa miongoni mwa maaskofu walioshiriki ibada hiyo na kuonekana kivutio kwa waumini wengi waliohudhuria misa hiyo.

Wakiwa na mwenyeji wao, Askofu Mkuu Dk Mtetemela, maaskofu hao walifika Zanzibar Jumapili ya Februari 18 kwa ajili ya kuadhimisha ibada ya misa iliyofanyika Kanisa la Kristu Mfalme lililoko eneo la Mkunazini.

Tangu mapokezi bandarini, njiani na kwenye ibada yenyewe kulikuwa na ulinzi mkali wa Askari wa Kutuliza Ghasia (FFU) waliokuwa na silaha mbalimbali yakiwemo mabomu ya machozi.

Sababu ya ulinzi huo, vyombo vya dola vya huko vilieleza kuwa ni kutokana na uzito wa ujumbe wenyewe, lakini pia kuwepo kwa uvumi wa matayarisho ya wanaharakati wanaopinga vitendo vya ushoga visiwani humo kutaka kuandamana kwa mabango kupinga ujio wa maaskofu hao. Hata hivyo, hakukuwa na kitu kama hicho.

Sababu kubwa ya maaskofu hao kwenda na kufanya ibada Zanzibar inaelezwa kuwa ni kutokana na kanisa hilo kuunganishwa na historia ya biashara ya utumwa kwani hata altare (madhabahu) ya kanisa hilo imejengwa katika eneo ilipokuwa nguzo ambayo watumwa walifungwa, kuteswa ili kupima ustahimilivu wao kabla ya kusafirishwa nje.

Ndani ya kanisa hilo ndipo pia mlimokuwa mashimo walimowekwa watumwa baada ya kutolewa sehemu mbalimbali tayari kusafirisha kwenda nje ya nchi kufanya kazi katika viwanda na mashamba ya mabepari.


Jaji Ramadhan avutia

Moja ya watu walioleta mvuto katika ibada hiyo alikuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, Agustino Ramadhan ambaye alikuwa akipiga kinanda (piano) kwa umahiri mkubwa ili kusaidia kupamba beti za nyimbo za wanakwaya waliokuwa wakiimba katika ibada hiyo. Kaka yake, Askofu Mstaafu Mkuu Mstaafu wa kanisa hilo, John Ramadhani alisoma Injili.

Wakati wa ibada hiyo, mwanamama kutoka Uganda, Hellen Wangusa alisimikwa na Dk Williams kuwa mwangalizi wa kanisa hilo ndani ya Umoja wa Mataifa (UN).

Maaskofu hao, walikutana na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Amani Abeid Karume ambaye baadaye aliwaandalia chakula cha mchana na kuwapa zawadi mbalimbali za kihistoria.

Uchaguzi mkutano wa Dar

Ili kutatua matatizo mbalimbali ndani ya kanisa hilo, mkutano huo uliunda kamati kuu (Standing committee) ambayo wajumbe wake ni maaskofu wawakilishi wa kanda mbalimbali za kanisa hilo duniani.

Kamati hiyo iliyo chini ya Askofu Mkuu wa Canterbury ndicho chombo kikuu kinachofanya maamuzi ya siku hadi siku ya kanisa hilo, na kupeleka mapendekezo ama taarifa za maamuzi hayo kwenye vikao vya Maaskofu wakuu wote.

Pamoja na kupingwa na maaskofu kadhaa hasa wa Kanda ya Afrika na Asia, Askofu Mkuu wa Marekani, Katherine Schori alichaguliwa kuwa mjumbe wa kamati hiyo kuwakilisha Kanda ya Marekani ya Kaskazini, Kati, Kusini na Caribbean.

Askofu mkuu wa Uganda, Henry Orombi kuchaguliwa kuwakilisha Kanda ya Afrika. Yeye ana msimamo mkali unaopinga kuruhusiwa kwa mashoga, ndoa za jinsi moja na kusimikwa kwa wanawake kuwa makasisi ndani ya kanisa hilo.

Maaskofu wa Mashariki ya Kati, Kusini na Magharibi ya Asia alichaguliwa askofu wa Misri, Mouneer Anis kuwa mwakilishi wao, Ulaya inawakilishwa na Askofu Barry Morgan kutoka Wales, ambaye hata hivyo hakuwepo kwenye mkutano huo wakati Askofu Mkuu, Phillip Aspinall wa Australia alichaguliwa kuwakilisha Kanda ya Asia Mashariki na Oceania.


Tamko la pamoja la maaskofu

Ili kuhtimisha mkutano huo, maaskofu hao walitoa tamko la pamoja ambalo lilihusu maazimio kuhusu mambo waliyokubaliana katika mkutano huo.

Mambo hayo yalililenga zaidi kulitaka Kanisa la Marekani ambalo linaonekana kuwa chanzo cha mtafaruku ndani ya kanisa hilo kujirekebisha.

Maazimio mengine ni nafasi ya kanisa katika kusaidia wananchi kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia (Millenium Development Goals), Elimu ya Theolojia katika kanisa hilo, mradi wa njia muafaka za kutafsiri maandiko (The Hermeneutics Project), ripoti ya Windsor, Mchakato wa kusikiliza hoja mbalimbali, kuundwa kwa baraza la Kichungaji, Mpango wa kichungaji ndani ya kanisa hilo na matarajio yajayo ya kanisa.

Kisa cha Askofu Mhogolo
Alipohojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) wakati mkutano huo , Askofu wa Dayodidi ya Central Tanganyika, Mdimi Mgogolo alitoa maelezo yaliyowatetea mashoga na wasagaji.

Msimamo huo wa askofu huyo kwamba watu hao hawastahili kufukuzwa kanisani, bali kuombewa vile katika kanisa kuna wadhambi wengine wakubwa lakini wamekuwa wakiendelea na ibada ulionekana kuwakera baadhi ya wajumbe wa umoja wa makanisa mkoani Dodoma ambao walitoa tamko la kumtenga askofu huyo.

Hata hivyo, baada ya tamko hilo, Askofu Mhogolo alijibu mapigo akiwataka wajumbe hao kumuomba radhi kwa kutoa kauli ya kumtenga bila kwanza kumuita ili awafafanulie hali ya mambo ni kosa.

Hata hivyo, Askofu Mhogolo alisisitiza kwamba makanisa hayo kwanza yakatae sadaka za wauaji, wezi, wazinzi na wadhambi wengine kwani asilimai 80 ya sadaka hizo hutoka kwa wadhambi .

Akasema kwamba vitendo vya ushoga na usagaji vinafanyika katika magereza, shule za bweni za wasichana na wavulana, hivyo haoni sababu ya kujifanya hakuna tatizo.

Hata hivyo, alionekana kukinzana na msimamo wake wa wenzake kutoka Afrika kukataa misaada ya Marekani kwa kusema kuwa wafadhili kutoka huko wamekuwa wakisomesha yatima wa dayosisi yake kwa kutoa dola 50 kwa kila mwanafunzi.

Msimamo wa Kanisa la Tanzania
Baada ya kumalizika kwa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Kanisa Anglikana nchini, Dk Mwita Akiri alieleza msimamo wa kanisa hilo akisema kwamba wataendelea kutokuwa na mahusiano na Kanisa la Marekani hadi hapo litakapotangaza rasmi kuacha kuunga mkono ndoa za jinsia moja, kutosimika mashoga kuwa wachungaji au maaskofu.

Akaeleza kwamba kanisa halitopokea fedha za misaada kutoka makanisa ya Marekani hadi hapo kanisa hilo litakapokuwa limejisafisha.

Hata hivyo, Dk Akiri alisema kwamba watu hao hawastahili kutengwa na kanisa kwani hali hiyo ni ya udhambi kama dhambi nyingine hivyo wanastahili kuombewa.

Upande wa wanaharakati
Baada ya kumalizika kwa mkutano huo, wawakilishi wa wanaharakati hao, Davis Mac-Iyalla kutoka Nigeria na Mchungaji Colin Coward wa Uingereza walisema kwamba wamefurahishwa na uamuzi huo wa maaskofu kwa vile unawapa fursa ya kutoa sauti zao.

“Kwanza ninashukuru kwamba kanisa halijaamua kututenga wala kutufukuza sisi (mashoga)… lakini tunafurahi kwamba kanisa halijasambaratika kama watu wengi walivyofikiri kwamba mkutano wa Maaskofu Dar es Salaam ndiyo utakaoligawa kanisa” akaeleza Mac-Iyalla.

Kwa upande mwa mwanaharakati anayepinga ushoga ndani ya kanisa hilo, Askofu Minns alieleza kwamba jambo lililopo sasa ni kuangalia mbele kwa manufaa ya kanisa kwa mkazo wa kusisitiza umuhimu wa kuenziwa kwa mafundisho ya asili ya kanisa hilo.

Hali ya baadaye ya kanisa
Maamuzi hayo ya Dar es Salaam ya maaskofu yanaonyesha kutuliza kwa muda hali na mtafaruku uliokuwa ukitishia kuligawanya kanisa hilo.

Kanisa limefikia hatua mpya baada ya Askofu Mkuu Akinola wa Nigeria kukubali kusaini tamko hilo la pamoja la maaskofu wakuu wenzake waliokutana Dar es Salaam. Kinachosubiriwa na uamuzi wa Kanisa la Marekani ndani ya miezi saba kuhusu maelekezo hayo mapya ya maaskofu wakuu. Kanisa la Marekani limepewa hadi Septemba 30 kutekeleza maazimio hayo.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.