Na Daniel Mjema, Moshi
MTUHUMIWA wa kupatikana na gramu 783 za dawa za kulevya aina ya cocaine daraja la kwanza, zenye thamani ya Sh6 milioni, Abdallah Nassoro Makotta, amehukumiwa kulipa faini ya Sh4 milioni.
Hata hivyo, Serikali imekata rufaa ikisema adhabu hiyo inapingana adhabu iliyowekwa kisheria kwa watuhumiwa wa makosa hayo na kwamba pia itachochea kukithiri kwa biashara hiyo badala ya kuikomesha.
Makotta ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam, alikamatwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro(Kia) Julai 21 mwaka jana akitokea nchini Brazil na baada ya kukamatwa alitoa madawa hayo kupitia njia ya haja kubwa.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mwendesha mashitaka wa Polisi, Sajini Edson alidai kuwa siku hiyo ya tukio mtuhumiwa alikuwa akitokea Brazil kupitia Amsterdam akiwa na pasi ya kusafiria namba AB 089710.
Akitoa hukumu hiyo Jumanne wiki hii,Hakimu Mkazi wa mahakama ya mkoa Kilimanjaro,Mariam Lusewa,alisema mahakama imemtia hatiani mtuhumiwa huyo baada ya kukiri mwenyewe kosa hilo.
“makosa haya yanaathiri sana uchumi wa nchi yetu kwa hiyo nakuhukumu kulipa faini ya Sh4 Milioni au kutumikia kifungo cha miaka nane jela”alisema Hakimu Lusewa. Mtuhumiwa alilipa faini hiyo na kuachiwa huru.
Mara baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mwendesha mashitaka mkuu, Mrakibu wa Polisi (SP), Fredrick Masilamba aliwasilisha rufaa mahakamani kwa niaba ya Jamhuri akisema adhabu hiyo inapingana na sheria za nchi.
Katika rufaa hiyo,SP Masilamba analalamika kuwa Hakimu aliyetoa hukumu hiyo alikiuka kifungu namba 31 cha sheria ya madawa ya kulevya kinachotoa adhabu ya faini ya Sh5 milioni au kufungo cha miaka 30 jela.
SP Masilamba analalamika kuwa katika sheria hiyo hiyo kama ilivyofanyiwa marekebisho na sheria namba 9 ya 1995, adhabu ya kosa hilo ni faini ya Sh1 Milioni au mara tatu ya thamani ya madawa yaliyokamatwa au kifungo cha miaka 20.
“faini hiyo inatakiwa iwe mara tatu ya bei ya soko ya madawa yaliyopigwa marufuku na lazima kiwango cha faini kiwe ni kile kinachoonekana ni kikubwa au kifungo cha miaka 20 jela”anadai SP Masilamba katika moja ya sehemu ya rufaa hiyo.
Kwa mtizamo huo wa kisheria, kama Hakimu angetumia vifungu vya kwanza basi mtuhumiwa huyo angelipishwa faini ya Sh5 Milioni au kifungo cha miaka 30 jela lakini Hakimu huyo alimhukumu kulipa faini ya Sh4 Milioni au kifungo cha miaka nae jela.
Vile vile kama Hakimu angeamua kutumia vifungu vilivyofanyiwa marekebisho, faini ilitakiwa iwe ni mara tatu ya thamani ya madawa hayo ambayo ingekuwa Sh18 milioni au aende kutumikia kifungo cha miaka 20 jela.
Masilamba alilalamika kuwa usafirishaji dawa za kulevya sio tu kwamba ni suala la kitaifa hadi Serikali ikaamua kutangaza vita dhidi ya biashara hiyo lakini pia tatizo hilo ni la kidunia linalopiganwa sambamba na vita dhidi ya janga la ugonjwa hatari wa Ukimwi.
“kwa hiyo kutoa adhabu ndogo kiasi hicho inapeleka ujumbe mbaya na unakatisha tamaa juhudi za taifa za kutokomeza tatizo la madawa ya kulevya”alihitimisha SP Masilamba katika rufaa hiyo ambayo itasikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania.
Hakimu Lusewa alipanga Machi 26 mwaka huu kwamba kesi hiyo itatajwa ili kielelezo hicho cha madawa ya kulevya kiwasilishwe mahakamani kwa ajili ya kuharibiwa kama mahakama hiyo ilivyoagiza.