Na Tausi Ally MENEJA wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mkoani Tabora, Damas Ngoiya (47), mkazi wa Dar es Salaam, Eliaisa Keenja (37) na mfanyabiashara, Josephati Nyambekwa, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashitaka matatu likiwamo la kuvunja nyumba na kuiba.
Akisoma hati ya mashitaka, mbele ya Hakimu Adolf Mahay, Kamishna wa Polisi, Charles Kenyela, alidai kuwa katika shitaka la kwanza, watuhumiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kutenda kosa la wizi wa Sh333.3 milioni mali ya Li Jinjlan.
Katika shitaka la pili, Kenyela alidai kuwa Mei 9, mwaka jana, majira ya saa 11.00 jioni, watuhumiwa hao walivunja nyumba namba 103 iliyopo katika barabara ya Haile Selasie jijini Dar es Salaam Kitalu namba 3579 ambayo ni mali ya Shirika la Nyumba (NHC) iliyokuwa imepangwa na Jinjlan na kufanya wizi huo.
Katika shitaka la tatu, watuhumiwa hao wanadaiwa kuiba bandari 74 za nguo, digital camera mbili, simu moja ya mkononi aina ya Nokia, kitanda kimoja cha mbao, kabati tano za mbao na moja la chuma, vipande vya madini aina ya almasi, vito vya Tanzanite na Rubi vyote vikiwa na thamani ya Sh333.3 milioni mali ya Jinjlan.
Watuhumiwa hao walikana mashitaka na upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Hakimu Mahay aliwataka watuhumiwa hao kila mmoja awe na wadhamini watatu ambao watasaini bondi ya Sh20 milioni na hati za nyumba ili waweze kupata dhamana. Aliiahirisha kesi hiyo hadi Machi 9, itakapotajwa.