Na Ramadhan Semtawa, Bagamoyo
KAMATI ya vyama vya CCM na CUF inayoshughulikia mazungumzo ya muafaka, inaendelea na vikao vyake, safiri hii wajumbe wa vyama hivyo wakiwa wamejichimbia Bagamoyo, lakini habari za ajenda zinazojadiliwa ndani, zikigubikwa na usiri mkubwa.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Kingunge Ngomable-Mwiru, zinaeleza kuwa kikao cha kamati hiyo kinaendelea katika Hoteli ya Oceanic.
Kingunge aliliambia gazeti hili kwamba mazungumzo hayo yalikuwa yakiendelea vizuri na kuongeza kwamba kama kungekuwa na kutoelewana kati ya pande hizo mbili, mazungumzo hayo yasingefanyika.
"Kama kungekuwa na ugomvi kila mtu angekaa kwake, lakini tuko hapa ina maana tunaendelea vizuri na mazungumzo, ila taarifa kamili za mazungumzo zitakuwa zikitolewa na vyama katika kila hatua itakayokuwa imekamilika," alisemae.
Alipoulizwa zaidi kama ni hatua gani hasa au jambo la msingi ambalo linajadiliwa kwa sasa, alijibu; " naomba unielewe, hatuwezi kuzungumza kitu sasa hivi taarifa zitakuwa zikitolewa, tukianza kuzungumza kila kitu mambo yataanza kuharibika," alisisitiza.
Hata hivyo, Mwananchi imeshuhudia ulinzi mkali katika chumba cha mkutano na hoteli hiyo, jambo ambalo pia limesababisha hata waandishi kutoruhusiwa kuingia ovyo katika hoteli hiyo.
Tathimini inayotokana na taarifa za ndani za mkutano huo inaonyesha kwamba mwenendo wa mazungumzo hayo unaleta matumaini ya kumaliza mpasuko wa kisiasa visiwani humo.
Wajumbe wa CCM wanaongozwa na Kingunge ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia siasa na uhusiano wa jamii, na CUF wanaogozwa na kiongozi wa upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohamed.
Taarifa zaidi ambazo gazeti hili ilizipata jana zinasema kuwa raundi hii ya mazungumzo hayo inatarajiwa kukamilizika Jumatatu.
Mwananchi ilishuhudia baadhi ya wajumbe katika kamati hiyo kutoka pande zote za vyama hivyo wakiwamo akina Masumbuko Lamwai kutoka CCM, msaidizi wa Katibu Mkuu wa CUF , Ismail Jusa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF visiwani, Juma Duni Haji.
Hata hivyo, kutokana na unyeti wa mazungumzo hayo, hakuna kiongozi yoyote wa CUF aliyekuwa tayari kuzungumzia maendeleo ya mazungumzo hayo jana mjini hapa.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Hamad, alifika mjini hapa kufuatilia mkutano huo juzi na jana asubuhi aliondoka, lakini Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba hakuonekana kutokana na taarifa kwamba mkutano huo si wa viongozi hao.
Hata hivyo, taarifa zaidi zilizopatikana kutoka kwa mmoja wa wajumbe wa mkutano huo zinasema mazungumzo hayo kwa sasa yamefikia katika hatua ya juu na mambo yanayojadiliwa ni mazito kiasi kwamba si rahisi kuyatoa hadharani.
"Kwa sasa mazungumzo yapo katika hatua ya juu, mambo yanayojadiliwa ni mazito, sasa kuzungumza zaidi kunaweza kuharibu mlolongo mzima wa mazungumzo," kilisema chanzo cha habari kutoka ndani ya mkutano huo.
Mkutano huo wa Bagamoyo ni miongoni mwa vikao kadhaa ambavyo vimekuwa vinafanywa na kamati hiyo iliyoundwa mapema Rais Jakaya Kikwete alipoingia maradakani ikiwa ni jitihada zake za kujaribu kumaliza mpasuko wa kisiasa Zanzibar.
Hivi karibuni kamati kuu ya CCM iliyoketi jijini Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine, ileleza kufurahishwa kwake na ripoti ya maendeleo ya mazungumzo hayo na ikaagiza kuwa kasi ya mazungumzo hayo iendelee.
Haijulikani ni mbinu zipi hasa zinazotumika kuondoa kutokuelewana kwa CCM na CUF visiwani Zanzibar, ingawa CUF wamekuwa wakipendekeza siku zote kuwa njia ya pekee ya kumaliza mpasuko uliopo ni kuunda serikali itakayoshirikisha watu kutoka vyama vote viwili.
Hata hivyo, upande wa CCM visiwani wamekuwa wakipinga kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, siku zote wakisema ushindi wao katika chaguzi unawapa mamlaka ya kisheria ya kuunda serikali.