Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kikwete akataa kufuta cheo cha ukuu wa wilaya
Kikwete akataa kufuta cheo cha ukuu wa wilaya
By Habari Tanzania | Published  02/23/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu

RAIS Jakaya Kikwete amesema, serikali yake haina mpango wa kukifuta cheo cha ukuu wa wilaya kwa kuwa bado ni wadhifa unaohitajika katika mfumo wa utawala na kwamba viongozi hao wanazo kazi muhimu wanazozifanya.

Kikwete aliyasema hayo jana katika Jiji la Brussels nchini Ubelgiji wakati akijibu swali la Mtanzania mmoja aliyehoji sababu ya serikali kuendelea kukikumbatia cheo hicho wakati kikionekana kutokuwa na sababu yoyote.

Alisema katika mifumo yote ya utawala wa duniani, kuna viongozi wa kuchaguliwa na kuteuliwa kama ilivyo kwa wakuu wa mikoa na wilaya ambao huteuliwa na rais.

Sambamba na hilo, Kikwete alikataa pendekezo la kutaka wakuu wa mikoa kupigiwa kura na wananchi badala ya kutumiwa kwa utaratibu wa sasa wa kuteuliwa.

Rais Kikwete alisema, tofauti na madiwani au wabunge, wakuu wa mikoa na wilaya ni wawakilishi wa serikali katika maeneo yao, hivyo wataendelea kuteuliwa na serikali badala ya kupigiwa kura na wananchi.

Katika hatua nyingine, Mtanzania mwingine, Shila Malegesi, alimuomba Rais Kikwete na serikali yake kuacha kukimbilia uundwaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki.

Alisema tofauti zilizopo kati ya nchi za Afrika Mashariki ni kubwa na za msingi, hivyo kuharakisha kuundwa kwa shirikisho hilo kunaweza kuwaletea matatizo Watanzania.

“Uundwaji wa shirikisho ni suala nyeti, sisi Watanzania ni wastaarabu sana kuliko hao tunaotaka kuungana nao. Serikali yetu lazima ilipatie umuhimu wa pekee hili kabla ya kufikia uamuzi.

“Mpaka hivi sasa, serikali imeshindwa kutoa upendeleo kwa wazawa, tunashuhudia wageni wakipata ajira zetu, kwa nini tusifanye kama wenzetu wa Ulaya, ambako mtu wa nje hapati kazi, kazi zote muhimu zimetengwa kwa ajili ya watu wao. Mimi ni daktari, lakini nikiomba kazi, naambiwa niwe nesi ama nikatunze wazee. Serikali lazima ilinde ajira za Watanzania wazawa,” alisema Malegesi.

Aidha alisema kuwa, tovuti ambayo wananchi wameshauriwa kupeleka maoni yao kuhusu shirikisho lao, haipatikani kwa urahisi, hivyo maoni ya wengi hayafiki sehemu husika na kuchapishwa kwenye vyombo vya habari.

Akijibu hoja hiyo, Rais Kikwete alisema serikali itayashughulikia kwa ukamilifu maoni yote yatakayotolewa na wananchi na kutafakari mwelekeo muafaka wa uundwaji wa shirikisho hilo.

Rais Kikwete, pia alizungumzia ubinafsishaji wa menejimeti ya Shirika la Reli. Alisema, Kampuni ya RITES kutoka India iliyoshinda tenda ya kuendesha shirika hilo, ina uzoefu mkubwa na inafanya kazi katika nchi za Msumbiji, Columbia na Cameroon na kwamba huko kote inafanya vizuri.

“Watu wetu wametembelea nchi zote hizo na wameridhika kwamba, kampuni hiyo ina uwezo mkubwa. Wapeni nafasi waendeshe TRC, nina imani tutafika mahali pazuri,” alisema.

Watanzania hao walimpongeza Rais Kikwete kwa hatua mbalimbali anazochukua katika kuwatumikia wananchi, kupambana na vitendo vya rushwa, ujambazi, elimu na uboreshaji wa mishahara ya watumishi wa umma.

Akizungumzia kupanda kwa umeme na athari zake kwa Watanzania, Rais Kikwete alisema, lilikuwa jambo la lazima kutokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji.

Alisema awali TANESCO ilitaka kupandisha bei ya nishati ya umeme kwa asilimia 25, lakini serikali ilikataa na kuruhusu asilimia sita kiasi alichokielezea kuwa si kibaya sana ikilinganishwa na iliyopendekezwa na TANESCO.

Aidha Rais Kikwete alisema kuwa, serikali inatambua kuwa Net Group ilishindwa kazi ya uendeshaji wa TANESCO na ikaamua kutafuta menejimenti mpya.

Alisema serikali iliamua kuachana na Net Group kwa nia njema baada ya kubaini kuwa, imeshindwa kazi na inalididimiza kabisa shirika hilo ambalo katika miaka ya nyuma, lilikuwa moja ya mashirika bora ya umma katika nchi zinazoendelea.

Kuhusu ada ya wanafunzi wa chuo kikuu, alisema kiwango wanacholipa sasa cha sh 770,000 si ada kamili bali ni sehemu tu, wakati kiasi kilichobaki hufidiwa na serikali.

Alisema serikali haiwezi kupunguza ada hiyo kwa sasa, kwa kuwa imeshafanya mengi ya kutosha katika kusaidia wanafunzi wa elimu ya juu.

Rais Kikwete yuko nchini Ubelgiji kwa ziara ya siku mbili na anatarajiwa kufanya mazungumzoa na Rais wa Jumuiya ya Ulaya, Kamishina wa Maendeleo na misaada ya kibinadamu na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Fedha katika Serikali ya Ubelgiji.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.