Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Rais Kikwete amtetea Mkapa kashfa ya rada
Rais Kikwete amtetea Mkapa kashfa ya rada
By Habari Tanzania | Published  02/23/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

Na Mwandishi Wetu, Burussels-Ubelgiji

RAIS Jakaya Kikwete amesema haoni sababu ya Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, kusimama hadharani na kuzungumzia suala la ununuzi wa Rada.

Kauli hiyo ya Rais Kikwete ilitokana na swali aliloulizwa na mmoja wa Watanzania wanaoishi hapa Brussels, Abubakar Hiza, ambaye pamoja na kutaka ufafanuzi kuhusu uchunguzi unaoendelea kuhusu ununuzi wa rada, pia alitaka Rais Benjamin Mkapa atoe tamko na aseme kwa ukweli na uwazi mambo yalikuwaje.

"Hivi mnataka mzee Mkapa atoe sauti, sauti kuhusu jambo gani? Mnataka aseme nini, mimi naona tumwache mzee wa watu," alisema Rais Kikwete.

Alikuwa akisalimiana na Watanzania wanaoishi hapa Brussels, Ubeligiji, mara baada ya kuwasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, ambayo madhumuni yake ni kuonana na kuzungumza na na Rais wa Jumuiya ya Ulaya, Kamishna wa Maendeleo na misaada ya kibinadamu, na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Fedha katika serikali ya Ubeligiji.

Rais alifafanua kuwa uchunguzi wa ununuzi wa rada unafanywa na serikali ya Uingereza kupitia kitengo chake maalum kwa kile kinachoamini kwamba kulikuwa na tuhuma za rushwa kati ya viongozi wa Kampuni ya BEA Systems na wakala aliyehusika na ununuzi wa rada hiyo.

Alieleza kwamba ilichofanya serikali ya Tanzania ni kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo pale ilipoomba kuja nchini kumfanyia mahojiano wakala huyo.

"Uingereza hawatuchunguzi sisi, wanachunguza kampuni yao na viongozi wa kampuni hiyo, tena Kampuni ya serikali, wanachunguzana wao kwa wao, kuona kama kuna tuhuma zozote za rushwa, na sisi tuliotoa ushirikiano wote," alisema Rais.

Aliongeza kuwa kwa kuwa suala hilo linaihusu Tanzania, serikali imeamua kulifikisha mikononi mwa PCB ili nao wachunguze na kujua ukweli na kisha kutoa taarifa yao serikalini.

"Ikionekana wametudhulumu tutaona namna ya kufurukuta, ndiyo maana tunashirikiana nao, matumaini yetu ni kuwa watatupatia taarifa ya nini kimetokea lakini kwa kuwa tuna maslahi nalo na sisi tunawataka PCB walitazame suala hilo," alifafanua.

Aliongeza kuwa si uuzwaji wa rada peke yake unaochunguzwa bali hata katika nchi za Afrka Kusini, Saudi Arabia nako kampuni hiyo inatuhumiwa kuhusika na vitendo vya rushwa.

Akijibu swali kuhusu kupanda kwa bei ya umeme na athari zake kwa wananchi wa kawaida na hifadhi ya mazingira, swali aliloulizwa pia na Hoza pamoja na suala la "Net Group" kushindwa kazi ya Menejimenti, Rais Kikwete alisema kuwa upandaji wa bei za umeme ulikuwa ni wa lazima kutokana na gharama za uzalishaji.

Alisema awli Tanesco ilitaka gharama za umeme zipande kwa asailimia 25 lakini serikali ilikataa na na kuruhusu asilimia hiyo sita aliyosema si kiwango kibaya sana.

Kuhusu "Net Group" kushindwa kazi ya uendeshaji wa Tanesco, Rais alisema serikali inalitambua hilo ndiyo maana iliamua kuachananayo na kutafuta menejimenti mpya.

Alisema serikali ilikuwa na nia njema katika kutauta menejiment mpya, baada ya ile iliyokuwapo kushindwa kazi na kulididimiza kabisa shirika hilo ambalo katika mika ya nyuma, lilikuwa moja ya mashirika bora ya umma katika nchi zinazoendelea.

Naye Koraniga Mkora aliitaka Serikali kuangalia upya ada ya Sh770,000 wanayolipa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwa ni kubwa hivyo ipunguzwe ili wanafunzi wengi wapate elimu hiyo na taifa liweze kujipatia wataalamu wa kutosha.

Akijibu hoja hiyo, pamoja na ile ya kutaka ile ya wakuu wa mikoa wapigiwe kura na wananchi badala ya kuteuliwa na cheo cha mkuu wa wilaya kifutwe, Rais alisema uendeshaji wa serikali kokote duniani upo katika mifumo miwili.

Alitaja mifumo hiyo kuwa ni viongozi wa kuteuliwa na wale wa kupigiwa kura, mifumo ambayo ndiyo inayotumiwa na serikali ya Tanzania. Alisema tofauti na madiwani au wabunge, wakuu wa mikoa na wilaya ni wawakilishi wa serikali katika maeneo yao, hivyo watateuliwa na serikali badala ya kupigiwa kura na wananchi wao.

Kuhusu kufutwa cheo cha ukuu wa wilaya, Rais alisema hakiwezi kufutwa, kwa kuwa wakuu hao bado wanahitajika na wanazo kazi za kufanya.

Akijibu hoja ya kupunguzwa kwa ada Chuo Kikuu, Rais alisema ada ya Sh770,000 wanayotozwa wanafunzi si ada kamili waliyotakiwa watoe kwa kuwa serikali imefidia sehemu ya ada iliyobaki.

Alisema serikali haiwezi kupunguza ada hiyo kwa sasa kwa kuwa imeshafanya mengi ya kutosha katika kusaidia wanafunzi wa elimu ya juu.

Katika hatua nyingine, Mtanzania mwingine, Shila Malegesi, aliitaka Serikali kutoharakisha uundwaji wa Shirikisho la Afrika Mshariki, kwa kile alichosema kuwapo kwa tofauti kubwa za kimsingi zilizopo kati ya Tanzania na wanajumiya wengine.

Alisema yeye mwenyewe asingependa kuwapo kwa Shirikisho hilo; "Uuundwaji wa Shirikisho hilo ni suala nyeti, sisi Watanzania ni wastaarabu sana kuliko hao tunaotaka kuungana. Serikali yetu lazima ilipatie umuhimu wa kipekee kabla ya ya kufikia uamuzi."

Akizungumza kwa hisia kali, Malegesi alisema kuundwa kwa shirikisho hilo kutawaletea Watanzania matatizo makubwa, huku akitoa mfano wa namna baadhi ya watu kutoka nchi jirani wanaofanya kazi ambazo zilipaswa kufanywa na Watanzania.

"Hivi sasa tu serikali haitoi upendeleo kwa wazawa, unashuhudia wageni wakipata ajira zetu, kwa nini tusifanye kama wenzetu wa Ulaya, ambapo mtu wa nje hapati kazi, kazi zote zimetengwa kwa ajili ya watu wao. Mimi ni daktari lakini nikiomba kazi, naambiwa niwe nesi au nikatunze wazee. Serikali lazima iwalinde Watanzania wazawa dhidi ya ajira zao," alisema Malegesi.

Alisema haamini kama Watanzania hawana sifa za kufanya kazi wanazochukua wageni, kwani wana elimu nzuri ambayo wakitoka nje ya Tanzania wanapata ajira kubwa na mishahara mikubwa kwa elimu hiyo hiyo waliyoipata Tanzania.

Malegesi alilalamika pia kwamba tovuti ambayo Watanzania wameshauriwa kupeleka maoni yao kuhusu shirikisho hilo, haipatikani kiurahisi na hivyo kufanya maoni yao kutowafikia walengwa na kuchapishwa kwenye vyombo vya habari.

Akijibu hoja hiyo Rais alisema, serikali itayashughulika kikamilifu maoni yote yanayotolewa na wananchi na kutafakari mwelekeo muafaka wa uundwaji wa Shirikisho na aliwataka wananchi kutoogopa kuwasilisha maoni au hisia zao.

Kuhusu serikali ubinafsishaji wa Menejimenti ya Shirika la Reli, mashirika mengine swali lililoulizwa na Thadeus Mugira, Rais alisema Kampuni ya RITES kutoka India ambayo ndiyo imeshinda tenda hiyo ni kampuni yenye uzoefu mkubwa na kwamba inafanya kazi kama hiyo, Msumbiji, Columbia na Cameroon na kwamba huko kote inafanya kazi vizuri.

"Watu wetu wametembelea nchi zote hizo na wameridhika kwamba Kampuni hiyo inao uwezo mkubwa, wapeni nafasi waendeshe TRC, nina imani tutafika mahala pazuri."

Watanzania hao walimpongeza Rais Kikwete kwa hatua mbalimbali anazozichukua katika kuwatumika wananchi kupambana na uhalifu, vitendo vya rushwa, ujambazi, elimu na uboreshaji wa mishahara ya watumishi wa umma.

Kwa upande wake, Rais aliwahimiza Watanzania hao kutosahau kwao walikotoka kuchangia maendeleo ya nchi na familia zao, kuheshimu sheria za nchi wanazoishi na kutojihusisha na vitendo vya uhalifu.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.