Jengo la Kitega Uchumi lililopo Jijini Dar es Salaam, limenusurika tena kuungua baada ya majiko ya mgahawa wa Chinese uliopo pembeni yake, kulipuka moto.
Tukio hilo lilitokea juzi usiku na kusababisha hofu kubwa kwa wapangaji kikiwemo kituo cha Radio Clouds Fm.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Bw. Alfred Tibaigana, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 3:30 usiku.
Kamanda Tibaigana alifafanua kuwa, chanzo cha majiko ya mgahawa huo kulipuka na kusababisha moshi mwingi kutanda eneo hilo ni baada ya vyakula vilivyokuwa vikipikwa kuachwa kwa muda mrefu vikichemka kwenye mafuta.
Alisema kitendo hicho cha kuacha vyakula kwa muda mrefu kwenye mafuta, kilisababisha majiko kulipuka na moto wake ukatanda katika sehemu ya jengo hilo huku moshi ukitanda jengo la kitega uchumi.
Hata hivyo, Kamanda Tibaigana alisema moto huo uliozimwa na askari wa Kikosi cha Zimamoto cha Halmashauri ya Jiji, haukuleta madhara yoyote kwa binadamu wala mali zilizokuwemo ndani yake.
Baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo, waliiambia Nipashe Jumapili kuwa, tukio hilo lilisababisha kituo cha Radio Clouds Fm kukatisha ghafla matangazo yake kwa takriban dakika 30.
Jengo hilo limekuwa mara kwa mara likipatwa na ajali za moto kutokana na sababu mbalimbali.
Katika tukio la kwanza, jengo hilo lenye ofisi za makampuni, mashirika na makazi ya watu, lilishika moto Aprili, mwaka 2002 ambapo mali yenye thamani ya Sh. 891, 809, 225 zikiwemo za kituo cha Radio Clouds Fm.
Aidha, Desemba, 2004, jengo hilo lilishika moto tena ulioanzia katika ghorofa ya nne kwenye makazi ya mpangaji mmoja na kuenea hadi ghorofa ya sita na saba.