Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Uwajibikaji wa pamoja serikalini umekwisha lini?
Uwajibikaji wa pamoja serikalini umekwisha lini?
By Habari Tanzania | Published  02/22/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:

SERIKALI yoyote yenye mafanikio ni ile ambayo inaheshimu misingi ya utawala bora, ambayo moja ya nguzo zake kubwa ni nidhamu ya utendaji wa kazi.

Moja ya miiko inayopaswa kuzingatiwa na watendaji na viongozi wa serikali imara ni mahusiano mazuri ya kazi kati ya watumishi, wakiwamo viongozi wa kada mbalimbali. Lakini kikubwa katika mahusiano hayo ni haja ya lazima ya kuwapo kwa uhusiano ulio imara na unaozingatia nidhamu za kazi kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.

Kwa lugha rahisi kabisa, serikali za mitaa zinazoundwa na halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji zinafanya kazi zikiwa na uhuru kamili wa kiutendaji na kimaamuzi huku zikitambua kuwa Serikali Kuu ndiyo mhimili mkuu wa sheria ambazo zinafanyia kazi.

Kwa sababu hiyo basi, ni wajibu wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kufanya kazi kwa karibu na ni kutokana na hali hiyo basi, ndiyo maana ndani ya serikali kuna waziri mwenye dhamana na masuala ya serikali za mitaa.

Hali hiyo iko hivyo katika masuala ya ardhi, makazi, kilimo, mifugo, elimu, afya, uchumi, biashara na mambo mengine mengi ambayo yatachukua muda mrefu kuyaorodhesha.

Ni kwa kulitambua hilo, ndiyo maana tukalazimika kuandika maoni haya ya leo, tukirejea katika mgongano wa kimasilahi unaoonekana kutokea sasa, kati ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa upande mmoja na Manispaa ya Kinondoni kwa upande mwingine.

Mgogoro huo ni ule unaohusu umiliki wa Baa ya Rose Garden iliyojengwa kando ya barabara itokayo eneo la Maji Machafu (Sayansi) na kutokeza Msasani-Butiama.

Mgogoro huu unatokana na hatua ya manispaa hiyo kwa muda mrefu sasa kutangaza kuivunja baa hiyo kwa maelezo kuwa imejengwa kwenye eneo la hifadhi ya barabara na kwamba mmiliki wake si mmiliki halali wa eneo hilo.

Hatua hiyo ya manispaa, hata hivyo imeshindwa kutekelezeka baada ya shauri hilo kufikishwa mahakamani na baadaye Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kuendelea kumtambua mmiliki wa Baa hiyo ya Rose Garden kuwa ndiye mmiliki halali.

Hatua hii ya wizara na hususan, waziri wake, John Magufuli ndiyo inayoonekana kuikera manispaa kiasi kwamba, siku chache tu zilizopita, madiwani wa manispaa hiyo, wakiungwa mkono na meya wao, Salum Londa, walivurumisha lawama kali.

Msimamo wa manispaa wa kumpinga Magufuli hata kufika hatua ya kutaka ajiuzulu, ulijibiwa vikali juzi na waziri huyo ambaye alionyesha kushangazwa na matamshi hayo ya manispaa na akatamka kuwa mmiliki wa sasa wa Rose Garden anayo hati halali ya umiliki aliyopewa na Kamishna wa Ardhi.

Malumbano hayo kwa mara nyingine yameifanya serikali iteleze na kujikuta ikikiuka misingi yake yenyewe inayohimiza katika uwajibikaji wa pamoja, kosa ambalo miaka zaidi ya 10 iliyopita lilisababisha aliyepata kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Augustine Mrema, aondolewe katika serikali.

Ni malumbano hayo ambayo yanatufanya leo hii tujiulize, je, imekwenda wapi misingi hiyo leo? Hivi viongozi wetu haoni kuwa malumbano ya namna hii yanabeba harufu mbaya ya ukiukwaji wa miiko ya uongozi na hata vitendo vinavyofanana na ufisadi?


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.