SHIRIKA la Meli la Zanzibar (ZSC), limeanza kuwapa likizo za lazima wafanyakazi wake ambao hawana kazi za kufanya katika shirika hilo kwa sasa.
Shirika hilo ambalo linakabiliwa na uchakavu wa meli zake, linamiliki meli za mv Mapinduzi na mv Maendeleo zilizonunuliwa kati ya mwaka 1974 na 1980.
Akitangaza uamuzi wa kuanza kutoa likizo za lazima zisizo kuwa na malipo kwa wafanyakazi, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo, Issa Othman Ahmed, alisema wataanza na wafanyakazi 190 ambao watakuwa wakipumzishwa kwa makundi.
Alisema kila kundi litakuwa na wafanyakazi 26, na wafanyakazi hao
watalazimika kukaa nyumbani kwa muda wa miezi mitatu ili kupunguza gharama za uendeshaji.
Alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya menejimenti kutafakari na kufikia uamuzi wa kuchukua hatua hiyo baada ya kugundulika kuwa meli ya mv Maendeleo haitaweza kufanya kazi kwa zaidi ya mwaka mmoja, licha ya kutengenezwa hivi karibuni huko Mombasa Kenya.
Alieleza kwamba meli ya Mv Maendeleo yenye uwezo wa kubeba abiria 480 na tani 700 za mizigo ilipelekwa nchini Kenya kwa ajili ya matengenezo ambayo yaligharimu dola za Marekani 176,000, lakini babada ya matengezo hayo imeshindwa kurudi katika hali yake ya kawaida.
Alisema wataalamu walibaini matatizo makubwa yaliyogunduliwa katika sehemu ya njini zake na tayari uongozi umeagiza vipuri vyenye thamani ya dola za Marekani 15,000 kutoka Japan baada ya kukoseka nchini Kenya.
Kuhusu meli ya mv Mapinduzi, alisema ina zaidi ya miezi sita haifanyi kazi na inatarajiwa kwenda kutengezezwa nchini Kenya hivi karibuni.