TANZANIA imetajwa kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuanza kuzalisha na kutumia nishati mbadala ya ethanol itakayotokana na miwa.
Nishati ya ethanol ni mbadala inayoweza kutumika kuendesha mitambo, magari na viwandani na inazalishwa kutokana na mabaki ya zao la miwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya SEKAB ya nchini Sweden, Per Carstedt, ambao ni wazalishaji wa nishati hiyo, jana alimwambia Rais Kikwete kuwa, uzalishaji wa nishati hiyo utaanza kwa majaribio Septemba mwaka huu wiyani Bagamayo, mkoani Pwani.
“Tunatarajia kama mambo yote yatakwenda sawa tutaanza uzalishaji wa majaribio mwezi Septemba huko Bgamoyo, na baada ya majaribio hayo, tutahamia katika bonde la Mto Rufiji ambako tumepata eneo kwa ajili ya uzalishaji mkubwa,” alisema Carstedt.
Mkurugenzi huyo alisema, hatua ya kuanza kuzalisha nishati ya ethanol, si tu kwamba itaipatia sifa Tanzania duniani, bali itakuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa Watanzania.
Alisema kwa kuanzia mashamba ya miwa yataajiri wananchi 300,000 na baadaye idadi hiyo itapanda hadi kufikia watu 700,000.
Alisema pamoja na mradi huo kuwapatia ajira Watanzania, pia watapata ajira kwenye kiwanda cha kuunganisha magari cha Scania kilichopo wilayani Kibaha, ambacho kitafufuliwa na kuanza kutengeneza magari yatakayotumia nishati ya ethanol.
Carstedt alisema, tayari SEKAB na Scania ambazo zote ni kampuni za Sweden zimekwishaanza mazungumzo na mamlaka zinazohusika mkoani Dar es Salaam, ili kuangalia uwezekano wa Jiji hilo kutumia mabasi yanayotumia nishati mbadala ya Ethanol.
Alisema kukamilika kwa mradi huo kutaisaidia serikali kubana matumizi ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta kutoka nje.
Carstedt Alisema, uamuzi wa SEKAB kuwekeza nchini Tanzania, utafungua ukurasa mpya wa uingizaji teknolojia ya kisasa na mitaji nchini.
Akizungumza baada ya kupata taaarifa hiyo, Rais Kikwete aliitaka kampuni hiyo kuharakisha maandalizi, ili kazi ya uzalishaji wa nishati hiyo uweze kuanza.
Rais Kikwete alisema kuanzishwa kwa mradi huo, kutachangia ahadi ya serikali ya kuwapatia wananchi ajira na kukuza pato la taifa.
Baadhi ya nchi za Scandinavia zimeanza kutumia nishati hiyo, ikiwa ni juhudi za nchi hizo kupunguza utegemezi wa mafuta na vilevile kuhifadhi mazingira.
Akizungumza na wafanyabiashara wa nchini Sweden, Rais Kikwete aliwataka wampatie taarifa za watu wanaowaomba rushwa ili awashughulikie.
Katika mazungumzo yake na wamiliki wa makampuni na wafanyabiashara mbalimbali wa nchini hapa, Rais Kikwete alieleza kutoridhishwa kwake na uwiano wa kibiashara uliopo kati ya Sweden na Tanzania.
Alisema uuzaji wa bidhaa za Sweden nchini Tanzania ni mkubwa kuliko bidhaa za Tanzania zinazouzwa Sweden, alisema hali hii inafaa kuangaliwa upya.