Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Lowassa aagiza kazi saa 24 Bandari Dar
Lowassa aagiza kazi saa 24 Bandari Dar
By Habari Tanzania | Published  02/22/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Lucy Ngowi

SERIKALI imeagiza wadau wote katika Bandari ya Dar es Salaam kufanya kazi kwa saa 24 ili kumaliza tatizo la msongamano.

Agizo hilo lilitolewa na Waziri Mkuu Edward Lowassa, jana wakati akiwa katika ziara aliyoifanya katika Mamlaka ya Bandari ya Dar es Salaam.

Lowassa alisema serikali inachukizwa na msongamano ulioko bandarini, kwani inataka bandari iwe na heshima yake.

“Wadau wote mnatakiwa kufanya kazi kwa saa 24 ili kupunguza msongamano. Tatizo la ulinzi litaangaliwa…tunataka kontena zikifika ziondolewe bandarini. Ongezeni kasi katika shughuli zenu,” alisema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu alisema ili kupunguza msongamano huo, serikali imeamua kukodisha maeneo ya NASACO, UDA na Ubungo, kwa kampuni ya kusafirisha makontena ya TICTS ili iweze kuhifadhi mizigo yake.

“TICTS wataanza kutumia eneo la Ubungo, yale majengo watakabidhiwa lakini bado bandari ni ya Tanzania. Wao watakodishwa tu kwa kuwa yatawawezesha kuwa na nafasi kubwa katika kuhifadhia makontena,” alisema Lowassa.

Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya Miundombinu kuangalia kwa ukaribu suala hilo ili msongamano kwenye bandari uweze kupungua. Aliongeza kuwa serikali inaangalia heshima kwa taifa na si biashara.

Pia aliiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) isimamie kampuni ya kuhakiki mizigo ya TISCAN ili waharakishe kuondoa nyaraka bandarini, pamoja na kuitaka bandari iruhusu TICTS kutumia geti namba nane kwa ajili ya meli kushusha mizigo.

“TICTS iboreshe taratibu zake na kuongeza ufanisi zaidi ingawa wanajitetea, pia ni aibu kwa bandari kutokuwa na mfumo wa kompyuta katika utendaji kazi,” alisema Lowassa.

Katika ziara hiyo, Lowassa aliagiza kitengo cha magari kupunguza mlolongo mrefu katika ufuatiliaji wa magari yanayopakuliwa bandarini, badala ya kumsumbua mteja kuzunguka maeneo mbalimbali kwa nia ya kukomboa gari lake.

“Nimeambiwa kuna mlolongo mrefu wa kupata gari lako. Jaribuni kupunguza au kutafuta njia muafaka katika kuondoa kero hiyo. Ni vizuri mambo yote yakaishia sehemu moja, mwenye gari akimaliza anachukua gari lake na kuondoka nalo,” alisema Waziri Mkuu.

Mwakilishi wa kampuni moja ya kupakua mizigo bandarini hapo, Otieno Igogo, alielezea matatizo wanayokumbana nayo bandarini, ikiwa ni pamoja na msongamano mkubwa kwenye eneo la TISCAN, kwa sababu ya mfumo uliopo wa kuhakiki thamani ya mizigo inayoingizwa bandarini.

“Tunaiomba serikali utaratibu uliopo uweze kufutwa ambao baada ya mizigo kukaguliwa hapa nchini iweze kutozwa kwa viwango vya hapa hapa nchini badala ya kuwasiliana na wadau wa nje ya nchi kwa ajili ya kupanga bei, hali ambayo inachangia ongezeko la msongamano bandarini,” alisema Igogo.

Igogo aliishauri serikali kuwa badala ya kwenda kuweka makontena katika maeneo ya mbali yaliyopatikana, wafikirie eneo lililopo karibu na bandari hiyo ambalo limekuwa na mapipa ya mafuta. “Tunaliomba eneo hilo liwe la bandari badala ya kwenda Ubungo,”.

Awali akimkaribisha Lowassa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Peter Mtandu, alisema kuwa, bandari za Tanzania hazina uwezo wa kuwa na bandari mama, kwa kuwa milango ya bandari haiwezi kuhudumia meli kubwa, pia kina cha maji katika magati ni kifupi.

“Bandari hazina maeneo muhimu ya uchumi wala uwezo wa kuhudumia meli kama vile karakana za meli. Miundombinu inayoziunganisha bandari zetu na nchi jirani haiko katika hali nzuri. Mtandao wa reli na barabara ni duni pamoja na njia za mawasiliano siyo za kuridhisha,” alisema Mtandu.

Alikiri upungufu wa vifaa vya kuhudumia mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam. Pia bandari imekumbwa na matatizo ya upatikanaji hafifu wa umeme kutoka kwenye gridi ya taifa, hali iliyosababisha mamlaka kutumia umeme wa jenereta ambao ni gharama kubwa.

Alisema uzoroteshaji wa ufanisi katika utendaji kazi umechangiwa na ukiritimba katika utaratibu wa uingizaji na uondoshaji mizigo bandarini.

Kaimu Mkurugenzi huyo alipendekeza serikali iandae mikakati itakayojumuisha mipango ya uendelezaji wa bandari, usafiri wa nchi kavu na mifumo ya biashara ili kuvutia shehena ya nchi jirani.

Pamoja na kuhakikisha ubinafsishaji wa shughuli za mamlaka ya bandari zilizosalia unafanywa kwa uangalifu zaidi na pia kuwapo kwa ushirikishwaji wa Watanzania.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.