Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Sitta: Tutaijadili Richmond
Sitta: Tutaijadili Richmond
By Habari Tanzania | Published  02/22/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Irene Mark

HATIMAYE sakata la Kampuni ya Richmond Development, iliyoshindwa kutekeleza mkataba wa dola za Marekani milioni 172 wa kuzalisha umeme wa megawati 100, litajadiliwa katika kikao kijacho cha Bunge.

Spika wa Bunge, Samuel Sitta, jana aliithibitishia Tanzania Daima kwamba suala hilo la Richmond lililozua maneno mengi na wasiwasi miongoni mwa wananchi litajadiliwa katika Kikao cha Saba cha Bunge kitakachoanza Aprili.

Mbali ya hilo, na bila ya kuingia katika undani, Sitta alisema kikao hicho cha Bunge kitajadili pia miradi mingine kadhaa ya serikali ambayo imezua utata.

Sitta alisema, anachosubiri ni barua kutoka kwenye Kamati ya Uwekezaji na Biashara ya kumuomba suala hilo lijadiliwe ndani ya Bunge, ili aanzishe mchakato wa kuwezesha mjadala huo kati ya wabunge na serikali.

“Wanachotakiwa ni kukamilisha taarifa yao baada ya kuelewana. Hadi tunaondoka bungeni hawakuwa tayari…walitakiwa kukubaliana juu ya mapendekezo waliyoamua kwenye taarifa yao ndipo waiwasilishe bungeni.

“Suala hapa si Richmond peke yake, yapo mambo mengi ambayo kama Kamati ya Uwekezaji na Biashara inatakiwa kuyajadili…wamedai iwepo sera ya Nishati ya Taifa kwa miaka 10.

Sitta alisema kamati hiyo ina mambo mengi ya msingi inayotakiwa kuyatolea mapendekezo bungeni ili yapate muda wa kujadiliwa kwa kina.

Alisema baada ya mjadala huo, iwapo serikali itashindwa kutoa majibu ya kuridhisha kuhusu suala hilo la Richmond, basi Bunge litalazimika kuunda kamati maalumu kulifuatilia.

Alisema kilichotokea wakati wa kikao cha Bunge kilichomalizika hivi karibuni, ni mgongano kati ya wajumbe wa Kamati ya Uwekezaji na Biashara kuhusu suala la Richmond, jambo lililowafanya washindwe kufikia uamuzi wa pamoja.

Alisema wabunge hao hawakuelewana na walikuwa na taarifa ndefu kuhusu suala hilo.

“Wao walikuwa na rasimu, Bunge linapokea taarifa iliyokamilika na yenye mapendekezo ndani. Na lazima serikali ipewe muda na nafasi ya kufanya mambo yake. Ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri inaeleza kuwa, kazi ya Bunge ni kusimamia kamati, lakini uundwaji wa kamati hizo unatokana na majibu yasiyotosheleza ya serikali kuhusu jambo lolote linalojadiliwa bungeni,” alisema Spika Sitta.

Hata hivyo, ingawa kauli hii ya Sitta imefungua ukurasa mpya kwa wabunge kuweza kuhoji na kupata ukweli kuhusiana na kampuni hiyo, kwa upande mwingine imezaa utata, kwa vile inapingana na kauli ya mwanzo ya wajumbe wa Kamati ya Uwekezaji na Biashara.

Awali wajumbe wa kamati hiyo walidai kumpelekea barua Spika Sitta, iliyokuwa ikimtaka kuunda kamati maalumu ya kuchunguza mkataba wa Richmond uliogharimu mamilioni ya fedha za serikali.

Wajumbe wa kamati hiyo walilidokeza gazeti hili kuwa, barua waliyomwandikia Spika ilikuwa inataka kuona tume hiyo ikiundwa kabla ya kikao cha Bunge kumalizika, hatua ambayo haikutekelezwa.

Walidai kuwa, walimkabidhi Spika barua hiyo Februari 6, wakiwa wameeleza nia yao ya kutaka kuundwa kwa kamati hiyo haraka, ili ichunguze na kupata ukweli kuhusu zabuni iliyopewa kampuni hiyo.

Baadhi ya wabunge waliozungumza na gazeti hili walimlaumu Spika kwa kuchelewa kuundwa kamati hiyo, kwa kile kilichoonekana kuwa ni kubaini kwake kuwa inaweza kubaini mambo ambayo yatawatia baadhi ya wakubwa katika matatizo.

Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, aliyezungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, alithibitisha kwa mara nyingine kwamba, walikwisha kumkabidhi barua Spika.

Mbunge huyo alisema hawezi kuzungumza mengi lakini akaahidi kutoa maelezo kuhusiana na suala hilo mara tu atakaporejea jijini.

Uchunguzi zaidi za Tanzania Daima umebaini kuwa, kumeibuka mvutano miongoni mwa wabunge kuhusu Richmond, huku kukiwa na madai ya kukingiana kifua kutokana na kile kinachoonekana kuwa mchezo mchafu uliofanywa na baadhi ya viongozi serikalini wakati wa kuipa mkataba kampuni hiyo, ambayo baadaye iliuuza mkataba kwa Kampuni ya Dowans.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.