BWAWA la Mtera jana lilifunguliwa ili kuruhusu maji yaliyojaa hadi kutishia kingo zake kutiririka katika mto Ruaha ili kuliepusha bwawa hilo kupasuka na kusababisha maafa makubwa.
Hata hivyo kumekuwa na taarifa kuwa uhamasishaji wa watu kuondoka katika maeneo ya kandokando ya Mto Ruaha haukuwa mkubwa na hivyo kuwepo wasiwasi wa baadhi ya watu kukumbwa na mafuriko.
Kumwagwa huko kwa maji kumefanyika ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Edward Lowassa, ili kunusuru kingo za bwawa hilo kubomoka na kunusuru maisha wa watu wanaoishi jirani na bwawa hilo
Habari kutoka Mtera zimesema kuwa maji hayo yalianza kutapishwa jana saa 2.50 asubuhi kwa mkondo wa kwanza na saa 3.00 asubuhi katika mkondo wa pili.
Mmoja wa maafisa wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa kuwa si msemaji wa shirika hilo, alisema kazi ilikuwa ikiendelea vizuri na kwa ufanisi.
Alisema lengo lilikuwa ni kupunguza mita za ujazo 180 za maji kwa sekunde katika njia ya kwanza na kwamba njia zote mbili zitaruhusu mita za ujazo 360 kwa sekunde.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, maji hayo yanaelekezwa katika bwawa la Kidatu kupitia Mto Ruaha, hii ikiwa na maana kuwa kuna uwezekano wa bwawa la Kidatu kujaa hadi juu.
Maji hayo kutoka katika bwawa la Mtera yana uwezekano mkubwa wa kusababisha maafa katika makazi ya watu wa mikoa Morogoro, Dodoma na Iringa wanaoishi kandokando ya Mto Ruaha.
Habari kutoka eneo hilo zinasema kuwa hakukuwa na juhudi za kuwaondosha wakulima wanaoishi kando ya mto huo, ingawa kumekuwa na agizo la Waziri Mkuu kwa wakuu wa mikoa kuwaondoa watu katika maeneo hayo.
Agizo hilo lilitolewa na Waziri Mkuu Februari 10 alipotembelea bwawa hilo kujionea na kufanya tathimini juu ya maji na hatma ya bwawa hilo .
Mwaka huu maji yamejaa hadi kufikia mita 698.50 baada ya kuwepo kwa mvua nyingi mwaka huu na kuvuka kiwango cha kawaida cha ujazo wa bwawa hilo ambacho ni mita 686.92.