Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Anglikana wapiga marufuku ndoa za mashoga
Anglikana wapiga marufuku ndoa za mashoga
By Habari Tanzania | Published  02/21/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:

Na Simon Berege

KANISA la Anglikana duniani limepiga marufuku kubarikiwa kwa ndoa za watu wa jinsi moja pamoja na kulitaka kanisa hilo nchini Marekani kusitisha kuwaweka wakfu mashoga na wasagaji kuwa makasisi.

Kiongozi wa Kanisa la Anglikana duniani, Askofu Mkuu wa Cantebury, Dk Rowan Williams, alitoa ufafanuzi huo wakati akitoa tamko la pamoja la maaskofu wakuu duniani waliokutana kwa siku tano katika hoteli ya Whitesands jijini Dar es Salaam, kujadili mambo mbalimbali yanayolihusu kanisa.

“Mafundisho ya Kanisa la Anglikana yanasisitiza kwamba mapenzi ya jinsi moja hayaendani na maandiko matakatifu… Injili itabaki kuwa Injili”, alieleza Askofu Williams alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juzi saa 5.00 usiku katika hoteli ya Whitesands.

Askofu Mkuu Williams hata hivyo alisema kwamba pamoja na kupigwa marufuku kwa ndoa hizo, kanisa halitawatenga wala kuwafukuza mashoga na wasagaji ambao ni waumini wa kanisa hilo, bali litatafuta njia ya kichungaji ya kuwasaidia watu hao kuondokana alichokiita na ugonjwa huo.

Kuhusu kuwekwa wakfu kwa Askofu Mkuu mwanamke wa Marekani, Katherine Schori, aliyekuwa akipingwa na maaskofu kadhaa, akiwamo Peter Akinola wa Nigeria, Dk Williams alisema kanisa linamtambua kusimikwa kwake kwani waumini wa kanisa hilo walimchagua kwa kutumia njia halali zinazokubaliwa na kanisa.

Kwa upande wa Askofu jimbo la New Hampshire nchini Marekani, Gene Robinson, ambaye alijitangaza hadharani kuwa ni shoga, Dk Williams alisema kwamba suala lake litaamuliwa siku zijazo baada ya kuundwa kwa baraza la kichungaji litakalotafuta muafaka kwa waumini wa majimbo ya Marekani na mengine duniani.

“Tutajitahidi kumaliza matatizo yanayolikabili kanisa hasa la Marekani, lakini hatuwezi kusema kwamba yatamalizika kesho, inahitaji muda,” alieleza Askofu huyo ambaye katika mkutano huo alikuwa ameambatana na Maaskofu Wakuu, Dk Donald Mtetemela (Tanzania), Dk Phillip Aspinall (Australia), Drexel Gomex (West Indies), na Bernard Ntahoturi wa Rwanda.

Maamuzi hayo ya maaskofu yanaonekana kutuliza kwa muda hali tete iliyokuwa ikitishia kugawanyika kwa kanisa hilo, hasa baada ya Askofu Mkuu Akinola wa Nigeria kukubali kusaini makubaliano hayo ya pamoja ya maaskofu wengine. Hata hivyo, bado haieleweki kanisa la Marekani litachukua uamuzi gani kuhusu maelekezo hayo mapya ya maaskofu wakuu (Primates) ambao wameipa Marekani hadi septemba 30 kuwa wameyatekeleza.

Kuhusu hilo, Askofu Mkuu, Williams alisema hafahamu maamuzi hayo yatapokelewaje na Kanisa la Marekani mbali na kwamba jitihada kubwa zinafanywa kuhakikisha kwamba kanisa halimeguki.

Maaskofu hao pia wametupilia mbali hoja ya kanisa la Marekani kutaka maaskofu kutokuingiliana majimbo katika ufanyaji kazi hasa, baada ya Askofu Mkuu wa Nigeria, Akinola kumsimika raia wa Marekani, Martyn Minns kuwa Askofu mwakilishi wa Nigeria anayeratibu mchakato wa parokia za Marekani zinazotaka kujitenga na kanisa la Marekani.

Askofu Minns anafahamika kwa msimamo wake wa zaidi ya miaka 30 kupinga ushoga na mabadiliko mengine ndani ya kanisa hilo. Askofu Minns alikuwa ni miongoni mwa wanaharakati waliyokuja jijini Dar es Salaam kushawishi Maaskofu wakuu kukataa vitendo hivyo.

Mgawanyiko katika kanisa la Anglikana ulianza mwaka 2003 baada ya Robinson kutawazwa kuwa Askofu. Kanisa la Anglikana lina waumini wapatao 77 million wengi wakiwa nchini Uingereza wakifuatiwa na Nigeria wenye waumini 17.5 milioni wakati Marekani ina waumini wapatao 2.4 milioni.

Masikio ya waumini wa kanisa hilo sasa yanaelekezwa nchini Marekeni kuona kama kanisa hilo litaridhia maelekezo ya maaskofu hao. “Kanisa la Marekani litaipitia kwa kina tamko hili la maaskofu,” alisema Mkurugenzi wa Mawasiliano wa kanisa hilo nchini Marekani, Robert Williams alipozungumza na Mwananchi.

Nao wawakilishi wa Wanaharakati wa kutetea haki za mashoga na wasagaji ndani ya kanisa hilo, Davis Mac-Iyalla kutoka nchini Nigeria na Mchungaji Colin Coward wa Uingereza, walisema uamuzi huo wa maaskofu bado unawapa fursa ya kutoa sauti yao.

“Kwanza nashukuru kwamba kanisa halijaamua kututenga wala kutufukuza sisi mashoga…. Lakini tunafurahi kwamba kanisa halijasambaratika kama watu wengi walivyofikiri kwamba mkutano wa maaskofu Dar es Salaam ndiyo utakaoligawa kanisa,” alieleza Mac-Iyalla ambaye pamoja na mwenzake walikuwa kwenye mkutano huo wa Askofu wa Canterbury na waandishi wa habari.

Naye Nora Damian anaripoti kuwa Kanisa la Anglikana Tanzania limesema halitachukua fedha toka kwa watu binafsi, dayosisi ama shirika lolote la Anglikana nchini Marekani linalochochea ushoga ama kufungisha ndoa za ushoga hadi hapo litakapopotoa tamko la kupinga ushoga.

Hayo yalisemwa na Katibu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dk Mwita Akiri, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, juu ya maazimio yaliyofikiwa na maaskofu wa kanisa hilo waliokuwa wakikutana nchini.

“Kanisa la Marekani limeendelea kuwa na jeuri na sisi hatutachukua fedha zozote kutoka kwa mtu binafsi, dayosisi ama shirika lolote la Anglikana Marekani linalochochea ushoga na tulishawaandikia barua tangu Desemba mwaka jana kuwa hatutafanya hivyo,” alisema Dk Akiri na kuongeza;

“Msimamo wetu sisi kama Tanzania ushoga ni dhambi, lakini shoga ni binadamu asinyimwe haki ya kuishi waendelee kuwa wenye dhambi kama wengine, wasifanywe kama wanyama, wahubiriwe ili wabadilike.”

Alisema maaskofu waliokutana Dar es Salaam, wamelipa Kanisa la Anglikana Marekani hadi Septemba 30 liwe limetoa tamko la kutokuendelea kuweka maaskofu mashoga pamoja na kutofungisha ndoa za watu wa jinsi moja na kwamba lisipofanya hivyo hatua zitachukuliwa juu ya ushiriki wao katika kanisa hilo ulimwenguni.

Alisema kwa kufanyika mkutano huo hapa nchini, Tanzania imejitangaza kitalii na kwamba maaskofu hao watakuwa mabalozi wema wa Tanzania kutokana na hali ya amani na utulivu waliyoiona pamoja na vivutio mbalimbali vya utalii.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.