MKUU wa Mkoa (RC) wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro jana alimshushia tuhuma nzito, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Margaret Sitta, kuwa wizara yake imekuwa ikitoa taarifa za uongo dhidi ya pesa za ujenzi wa shule.
Alisema watendaji katika wizara hiyo, wana tabia ya kuwadanganya walimu wakuu wanaofuatilia pesa za ujenzi wa shule kuwa tayari zipo na wanaonyesha mgawo ulivyo katika karatasi, lakini wanapotakiwa kuzikabidhi, zinakosekana.
Kandoro aliyasema hayo jana mbele ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa, ambaye alikuwa katika ziara ya siku moja kuangalia ujenzi wa shule za sekondari jijini Dar es Salaam.
“Tumechelewa kukamilisha ujenzi wa shule kwa sababu upatikanaji wa pesa kutoka wizarani kupitia Mpango wa Elimu ya Sekondari (MMES), ni tatizo.
“Watendaji wa wizarani wana tabia ya kuwadanganya walimu, wanawaonyesha makaratasi kuwa pesa ziko tayari, lakini wakiziomba zinakuwa hazipo,” alisema Kandoro.
Hata hivyo, kabla hajamaliza, Waziri Sitta alimkata kauli na kueleza kuwa kauli yake si ya kweli, kwa sababu Mkoa wa Dar es Salaam Hazina ipo karibu, hivyo shule zinawahi kupata pesa.
Baada ya maelezo hayo ya Sitta, waziri mkuu, alimwita Mratibu Msaidizi wa MMES, Alpius Machagge na kumtaka atoe ufafanuzi kuhusu mgongano wa kauli za vigogo hao.
Machagge alimweleza Lowassa kuwa, pesa hizo zinawasilishwa mashuleni mara moja baada ya kutoka Hazina.
Kandoro aliipinga kauli ya Machagge na kumweleza Lowassa kwa kumkumbusha kuwa hata alipokuwa Temeke, alimsikia mkuu wa wilaya akilalamika kwamba ujenzi wa shule nane umechelewa kwa sababu ya kuchelewa pesa za MMES.
Katika hali ambayo haikutarajiwa na wengi, Waziri Sitta aliingilia kati na kueleza kuwa Mkoa wa Dar es Salaam umejichelewesha kwa kupeleka majina ya sekondari ambazo hazijasajiliwa, ndio maana walishindwa namna ya kuwapelekea pesa hizo.
Malumbano hayo yalikatishwa na Machagge ambaye aliomba kuonana na Kandoro ofisini kwake ili kulizungumzia suala hilo.