WANAFUNZI waliofutiwa matokeo yao ya mtihani wa darasa la saba mwaka jana, wanatarajia kuanza kufanya marudio ya mitihani hiyo kesho.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa, Joyce Ndalichako alisema mitihani hiyo itafanyika kwa siku mbili.
“Kutokana na taarifa ya tume iliyochunguza tuhuma za udanganyifu katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi Septemba 2006, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilibatilisha matokeo ya watahiniwa 1,857 ambapo walipewa fursa ya kurudia mtihani,” alisema.
Ndalichako alisema, orodha ya watahiniwa wanaopaswa kurudia mtihani wa kumaliza elimu ya msingi inapatikana kwa maafisa elimu wote wa mikoa na wilaya husika na katika shule zote zilizokuwa na watahiniwa waliositishiwa matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi 2006.
Alisema lengo la wizara ni kuhakikisha kuwa, wanafunzi wanaorudia mtihani ambao watafaulu wanapata fursa ya kuchaguliwa kujiunga na elimu ya Sekondari kabla ya Machi 15 mwaka huu. Matokeo yao yatatolewa Machi 4.
Mikoa yenye mtihani wa marudio ni Arusha, Dodoma, Kagera, Kilimanjaro, Mara, Mtwara, Mwanza, Shinyanga, Tabora na Mbeya.
Kutokana na udanganyifu wa mtihani wa darasa la saba uliofanyika mwaka jana, Januari 26 Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Margaret Sitta alitangaza kuwavua vyeo baadhi ya maafisa elimu na walimu wakuu ambao maeneo yao yalionekena kuhusika kwa namna moja au nyingine katika udanganyifu huo.