RAIS Jakaya Kikwete amesisitiza wito wake kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutosita kuikosoa serikali pale inapokosea.
“Nilisema katika semina ya wabunge na wawakilishi wa Chama Cha Mapinduzi wiki mbili zilizopita kwamba, wanao wajibu kama wabunge wa CCM wa kuikosoa na kuishauri serikali yao pale inapokosea.
“Nasisitiza tena kwamba wanao wajibu huo wa kukosoa, lakini vilevile kuishauri na kutoa ushirikiano wao kwa serikali iliyoko madarakani,” alisema.
Kikwete alitoa kauli hiyo juzi, alipokuwa akisalimiana na Watanzania wanaoishi Stockholm , Sweden, baada ya kuwasili kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kwa mwaliko wa Waziri Mkuu wa nchi hii, Frederick Reinfeldt.
Alibainisha kwamba, wabunge hao wa CCM wanao wajibu mkubwa katika kuishauri serikali katika utendaji wake, huku wakikosoa pale panapostahili.
Akijibu swali kutoka kwa mmoja wa Watanzania hao kuhusu hoja ya kuitishwa kwa kura ya maoni kuhusu muungano, Rais alisema kuwa, kwa sasa haoni sababu ya kuitisha kura hiyo, kwa sababu tayari tume mbili za majaji Kisanga na Nyalali walishaifanya kazi hiyo na wananchi wakatoa maoni yao.
Alisema haoni haja ya kurudisha suala la muungano kwa wananchi, kwa sababu wananchi walitamka kwamba wanataka serikali mbili.
Alieleza kwamba, yale mambo yote ambayo yanaonekana kama dosari katika muungano, hivi sasa yanajadiliwa katika vikao vinavyowahusisha Waziri Mkuu, Edward Lowassa, na Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha.
Akiwa hapa Stockholm, Rais atakuwa na mazungumzo na Mfalme wa Sweden, Carl XVI Gustaf, Waziri Mkuu, Frederick Reinfeldt, Mkurugenzi Mkuu wa SIDA, Maria Norrfalk, Spika wa Bunge la Sweden, Per Westerberg na Waziri wa Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa, Gunilla Carlsson.