KUNDI la mashoga limefanikiwa kujipenyeza na kuingia visiwani Zanzibar na kushiriki ibada ya misa iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Canterbury, Dk. Rowan Williams, pamoja na kupokea Ekaristi Takatifu.
Mashoga hao walifanikiwa kujipenyeza katika msafara wa maaskofu wa Kanisa la Anglikana waliokwenda kufanya ibada katika Kanisa la Kristo Mfalme pamoja na kukutana na Rais Amani Abeid Karume, baada ya kujifanya waandishi wa habari wa kimataifa walioandamana na ujumbe wa maaskofu hao.
Mashoga hao ambao waliwasili katika Bandari ya Dar es Salaam jana asubuhi wakitokea Hoteli ya White Sands, walifanikiwa kujichanganya na waandishi wa habari wa ndani na nje walioandamana na maaskofu hao kwenda Zanzibar.
Baadhi ya viongozi wa msafara huo walithibitisha kuwapo kwa mashoga katika msafara huo lakini walieleza kuwa hawana uwezo wa kuwazuia, kwa sababu wana vitambulisho vya uandishi wa habari vya nchi walizotokea.
Hata hivyo, katika hali isiyo kuwa ya kawaida, baadhi ya maaskofu wanaotambuliwa kutokana na msimamo wao wa kupinga masuala ya kutambuliwa kwa mashoga ndani ya kanisa hilo, hawakuonekana katika msafara huo.
Mmoja wa maaskofu hao ni kutoka Nigeria, Peter Akinola, ambaye ni mpinzani mkubwa wa ushoga.
Taarifa zisizo rasmi zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa askofu huyo hakutaka kuandama na mashoga hao.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Mwita Akiri, ambaye alithibitisha kutokuwapo kwa askofu huyo katika msafara, alisema kuwa ameshindwa kusafiri kwa sababu anasumbuliwa na maumivu ya mgongo.
Kabla ya kuwasili kwa ujumbe wa maaskofu hao jana, mji wa Zanzibar uliwekwa chini ya ulinzi mkali wa polisi baada ya kuvuja kwa taarifa ya kuwapo kwa tishio la kikundi cha wanaharakati wanaopinga ushoga na waumini wa dini ya Kiislamu kutaka kuvuruga ziara hiyo.
Ilielezwa kuwa vikundi hivyo vilikuwa vimeanda maandamano makubwa ya kupinga ushoga katika Kanisa la Anglikana.
Magari kadhaa ya askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) yakiwa na bendera nyekundu yalionekana yakizunguka katika mitaa mbali mbali ya Zanzibar kuhakikisha ujumbe huo unaingia katika Bandari ya Zanzibar salama na kuendesha ibada kama ilivyopangwa.
Ujumbe huo wa viongozi wa ngazi za juu wa Kanisa la Anglikana duniani uliwasili katika Bandari ya Zanzibar saa nne asubuhi kwa boti ya Sea Express, na uliongozwa na pikipiki za polisi, ukipitia Mtaa wa Malindi, Darajani hadi Mkunazini, ambako ibada takatifu ilipangwa kufanyika katika Kanisa Kuu la Kristo Mfalme.
Tukio jingine lililovuta hisia za watu wengi wakiwamo wanaharakati wanaopigania ushoga ndani ya kanisa hilo pamoja na waandishi wa habari, ni kitendo cha maaskofu watatu kutoshiriki Ekaristi Takatifu.
Kinyume cha maaskofu hao, mashoga waliohudhuria ibada hiyo ambao wamekuwa mstari wa mbele kumshinikiza Askofu Mkuu, Dk. Williams, aruhusu uwepo wao ndani ya kanisa hilo, walijongea mbele ya altare na kupokea Ekaristi Takatifu.
Katika mahubiri yake kwenye ibada hiyo maalumu ya kuadhimisha siku ya kukomeshwa kwa biashara ya utumwa duniani, Dk. Williams aliwaasa viongozi wa Kanisa la Anglikana duniani kupiga vita maovu yanayofanyika katika jamii badala ya kuyafumbia macho.
Dk. Williams alisema biashara ya utumwa ilifanikiwa duniani kwa sababu watu walikuwa vipofu na viongozi hawakukemea biashara hiyo.
“Watu walikuwa vipofu, hawakuona ubaya wa biashara ya utumwa, naamini watu walikuwa wakiteswa, ingawa watu hawakukemea,” alisema.
Alisema hivi sasa ni wakati muafaka kwa viongozi wa dini na waumini wao kutafakari vitendo vinavyopaswa kupigwa vita hasa vinavyogusa kina mama, wazee na watoto.
Baada ya ibada hiyo, Askofu Mkuu Williams na ujumbe wake alikutana na Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume katika Hoteli ya Serena Inn, ambako walikuwa na mazungumzo mafupi kabla ya kuondoka jana jioni kurejea Dar es Salaam.
Habari zilizoifikia Tanzania Daima zinaeleza kuwa Rais Karume alieleza kufurahishwa kwake na ziara ya askofu huyo pamoja na ujumbe wake visiwani Zanzibar, na alimweleza askofu huyo kuwa milango iko wazi kwa kanisa hilo kuisaidia serikali yake katika sekta mbalimbali.
Awali Katibu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar, Nuhu Sallanya, alizungumza na waandishi wa habari, ofisini kwake Mkunazini, na kueleza kuwa Dk. Williams na ujumbe wake wataingia Zanzibar kwa boti ya kukodi.
Alizitaja baadhi ya shughuli zitakazofanyika katika ziara hiyo kuwa ni ibada maalumu ya kuadhimisha kumbukumbu ya Askaofu Mkuu wa Canterbury na Primates.
Taarifa ya Sallanya iliibua pingamizi kutoka Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI), ambayo iliwataka mashoga hao wasikanyage katika ardhi ya visiwa hivyo.
Katika onyo lake dhidi ya ziara hiyo, JUMIKI iliitahadharisha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuipiga marufuku ziara ya maaskofu hao, kwa sababu haitakuwa na manufaa yoyote kwa wananchi wa Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mkunazini hivi karibuni, Naibu Amiri wa JUMIKI, Sheikh Azzan Khalid Hamdan, alitoa taarifa ya kupinga ziara hiyo kwa waandishi wa habari.
Alisema ziara hiyo inaweza kuhatarisha amani Zanzibar kwa sababu baadhi ya vikundi na maaskofu wa kanisa hilo wanatetea vikundi vinavyodai haki za ushoga na usagaji, kinyume cha mafundisho ya dini ya Kiislamu.
Ziara ya Askofu Dk. Williams na ujumbe wake ambao wanaendelea na mikutano yao nchini imekuwa ikiandamwa na makundi ya wasagaji na mashoga kutoka katika sehemu mbalimbali za dunia ikiwamo Marekani, Uingereza na Nigeria, ambao wamefurika mjini Dar es Salaam.
Wasagaji na mashoga hao wanashinikiza uongozi wa Kanisa la Anglikana kutambua haki zao ili waweze kupata haki zao kamili ndani ya kanisa hilo kama wana jamii wengine.
Katika baadhi ya nchi za Afrika, ikiwamo Afrika Kusini, miswada ya kutambuliwa kwa mashoga na wasagaji imekwisha kuwasilishwa Bungeni, kufuatia shinikizo la makundi hayo ya jamii.
Katika nchi za Uingereza na Uholanzi, tayari makundi hayo yanatambuliwa na kuna sheria zinazoruhusu mashoga na wasagaji kuendesha shughuli zao katika jamii, ikiwamo pia ruhusa ya ndoa za mashoga.
Vitendo vya ushoga na usagaji vinaonekana kupanda chati kila kukicha huku watoto wenye umri wa miaka 22 na kuendelea ndio wanaoongoza.