Barua.
Ndugu Waziri Bakari Mwapachu,
Mimi ni Raia mwema ninaeipenda nchi yangu! Lakini ninakerwa sana na jambo hili la ujambazi.
Naanza nikitanguliza shukrani zangu za dhati kwa Jeshi la Polisi kote nchini kufuatilia jitihada walizonazo za kukabiliana na ujambazi (uhalifu) uliotikisa Mikoa¸kumekuwa na matukio mengi ya kuteka magari huku wakitumia siraha kali za moto, kunyang’anya mali, kujeruhi, kuzalilisha kubaka, kupoteza maisha ya watu na kuacha wengi wao wakiwa walemavu wa maisha.
Tatizo hili limekuwa likisikika baadhi ya mikoa hapa nchini lakini mikoa ya Kagera na Kigoma matukio ya utekaji wa magari yamekuwa kama mvua za masika zinazoambatana na radi kali, kwani husikika hapa na pale pamoja na jitihada kubwa sana zinazoendelea kufanyika na Jeshi la kulinda usalama wa raia na mali zake, bado tatizo hili limezidi kukomaa siku hadi siku, hali hii imesababisha maendeleo ya wananchi kurudi nyuma kwani shughuli zote za maendeleo zinategemea kusafiri toka sehemu moja hadi nyingine, maajabu ni kwamba Wananchi wa Kigoma vijijini hata kutembea kilometa kumi (10) wana kosa amani huku wakifikiria kutekwa, kuporwa, kuuawa! Kiasi kwamba mwananchi huyu maendeleo yake anategemea pengine asafirishe bidhaa zake toka sehemu moja hadi nyingine, mkoa hadi mkoa kwa hali hii hata shughuli hizo zimekuwa mashakani kwa wananchi wa mikoa hii kuhofia usalama wa maisha yao!
Ingawaje watanzania tunafahamu ya kwamba nchi jirani zinazopakana na mikoa hii ya Kigoma, na Kagera ni muda mfupi tu, zimeondokana na vita iliyochukua muda mrefu na vifo vya watu wengi kufuatia serikali za nchi hizo kupinduliwa na waasi na kuingia msituni. Linalosikitisha ni kwamba baadhi ya matukio katika mikoa hii waharifu wengi husadikika kuwa raia wa nchi jirani ya Burundi na Rwanda ambavyo waharifu huonekana kuwa na siraha nzito za kivita kama Bunduki aina za Sub Machinegun, AK47 na mabomu ya kutupa kwa mikono. Hii husababisha Askari wa nchi yetu kufanya kazi ya ziada katika mazingira magumu.
Ndugu Waziri, kwa mtu ambaye hajawahi kuishi au kufika katika mikoa hii ya Kagera na Kigoma haya ninayoyazungumza ni kama viini macho tu, lakini ninaomba waziri wa uaslama wa raia, wizara ya mambo ya ndani, wizara ya ulinzi na jeshi la kujenga taifa pamoja na wanasiasa walitazame eneo hili kwa macho mawili, vinginevyo tutaishia kulalamikia maendeleo wakati tunajisahau kiusalama. Tukumbuke kuwa mahala pasipo na usalama maendeleo ni ndoto, mfano mkoa wa Kigoma unaongoza kwa upungufu wa watumishi wa umma, mfano walimu na wahudumu wa afya hakuna na kila anayepangiwa mkoa wa Kigoma anakimbia, na ukijaribu kuhoji sababu unaambiwa tatizo ni usalama mdogo na mazingira duni ya kufanyia kazi.
Ndugu Waziri, Kwa hali hii tunaomba vyombo vya ulinzi na usalama kupitia katika wizara zilizoziainisha hapo juu Muunde mkakati imara na wenye nguvu utakaowezesha hali ya amani kuwepo Kagera na Kigoma, na kama itabainika kuwa nchi jirani zinahusika na sakata hili la hovyo basi mawaziri wa ulinzi nao wachukue hatua za haraka na za makusudi kuwabana wenzao wa Burundi ili kuhakikisha tunaishi kwa amani na tunaingia kwa pamoja katika MKUKUTA na MKURABITA na hatimae tuwe na maisha bora ambayo Mheshimiwa KIKWETE aliahidi. Katika hili nampongeza Mkuu wa wilaya ya Kibondo ambaye mara zote anaposikia matukio ya uharifu analivalia njuga kweli kweli na amekuwa akikutana na wakuu wa mikoa ya Burundi ili kujadili hali ya usalama katiuka mipaka ya nchi zetu.
Kwa niaba ya wananchi wote ninaomba tatizo hili liwe la kitaifa kwani raia wengi wamekwisha poteza maisha yao kupata ulemavu wa kudumu, na kuacha familia zao zikihangaika na kusababisha maendeleo ya Taifa kurudi nyuma! Tunaomba askari wawezeshwe kwani wanafanyakazi katika mazingira magumu. Pia wawezeshwe kuwa na vitendea kazi vinavyoweza kukabiliana na maadui, mfano mikoa ya Kigoma na Kagera ina misitu minene aya hifadhi ambayo pia hutumiwa na majambazi kama maficho, kutokana na uzito wa hali mbaya ya amani katika eneo hili askari polisi wanalazimika kuingia katika misitu hiyo kuwasaka majambazi ambapo hata hivyoi mafanikio huwa madogo sana kutokana na ukosefu wa viona mbali kama vile DARUBINI.
Mfano, tarehe 17/1/2007 magari yalitekwa katika barabara kuu itokayo Nyakahura kuelekea Ngara/Benako Mkoani Kagera likiwemo gari DFP 3482 linalomilikiwa na shirika la kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) lililokuwa limebeba wafanyakazi wa mashirika mengine yanayosaidia wakimbizi walioko mikoa hiyo ya Kigoma/Kagera. Wafanyakazi hao waliporwa mali zao kupigwa, kuburuzwa dereva kujeruhiwa Kichwa upande wake wa kushoto:
Mheshimiwa Waziri Mwapachu; Hata kabla ya hayo kumekuwa na matukio mengine mengi ambayo ni ya kutia hofu sana, katika eneo la kambi ya wakimbizi wa Burundi iitwayo Nduta na eneo la kijiji cha Rusohoko pamekuwa kama Kosovo, kijiji cha Minyinya na Mugunzu jirani kabosa na kambi ya muda ya wakimbizi ya Muguzu hali imekuwa ya sintofahamu kila baada ya siku kadhaa watu wanatekwa na kuporwa mali zao, kama haitoshi katika kijiji cha Kilemba (Kumkugwa) limewahi kurushiwa risasi gari la polisi na kupelekea uharibifu wa kioo na mataili baada ya kupasuliwa kwa risasi za majambazi waliokuwa wamemteka |Sisita wa kanisa la Angililkana mjini Kibondo aitwaye Magdarena Lanz ambaye alikubwa na hofu na tishio la maisha.
Katika kijiji cha Kazilamihunda majambazi kutoka nchi jirani ya Burundi baada ya kupora mbuzi kwa ajili ya kitoweo cha kuwashibisha kabla ya kufanya uharamia mwingine wananchi wenye ujasiri waliwauwa wawili, napongeza IGP Mwema alitoa tuzo kwao.
Matukio haya hupishana kwa muda mfupi baada ya wiki, husikika sehemu nyingine na baada ya siku au mwezi tena! Wananchi huishi bila amani muda wote na tarehe 11/2/2007 basi la kampuni ya ALLYS lilitekwa kilomita tano (5) kutoka wilayani Kibondo Mkoani Kigoma watanzania wema waliojaa amani walichungulia kaburi kutokana na milio mikali ya risasi katika majibizano ya majambazi na askari waliokuwa wamesindikiza gari hilo, maskini baadhi ya askari wetu alijeruhiwa kwa risasi kwnye mguu wake kwa sasa amelazwa katika Hospital ya Taifa Muhimbili, mimi kama raia mwema ninaona fahali kutoa pongezi nyingi kwa Jeshi la Polisi na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya chini ya mkuu wa wilaya luteni kanali John Mzurikwao ambaye mara zote asikiapo tukio huchachamaa ili kuwatia mbaroni wahusika. Jitihada za kudhibiti hali ya ujambazi uliyokithili katika wilaya ya Kibondo na wilaya za jirani za Kasulu na Ngara-Kagera.
Hebu wote kwa pamoja tujiulize leo hii walau serikali inapata ufadhili wa vitendea kazi baadhi kutoka shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, mfano magari kwa jeshi la polisi na viongozi wengine katika wilaya zinazohifadhi wakimbizi yanatolewa na UNHCR, lakini hali ya kudhibiti uharifu ambao baadhi yake unafanywa na waliowahi kuwa wakimbizi katika maeneo haya na kuayazoea mazingira kabla ya kurejea nchini mwao, Je itakuwaje baada ya wakimbizi wote kuondoka na UNHCR kusitisha ufadhili wake kwa vyombo vya usalama katika maeneo yetu? Jamani sitanii kabisa tunahitaji msaada wa pekee kutoka kwa majeshi yetu yote na ikiwezekana basi yaungane kufanya msako au kuendesha vita kali dhidi ya majambazi na waharifu wengine waliojificha katika misitu yetu.
Asante sana, ni mimi mzalendo mwenye uchu mkubwa wa amani nisiyetaka hali hii iendelee kwani tutazidi kubaki nyuma kiuchumi.
Paul M. ATAFILE.
Raia Mwema.-Kibondo
Kigoma