Doris Mageta
MKAZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa, Amani Mwakisyala, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Sumbawanga kwa kosa la kukutwa na kichwa cha binadamu kwenye eneo lake la kazi.
Akisoma shitaka hilo Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Cleophas Mpinge, alieleza mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Arcad Chuwa, kuwa mshitakiwa Mwakisyala ambaye ni fundi saa alikutwa na kichwa cha mtoto anayedhaniwa kuwa na umri kati ya miaka miwili na mitatu February 9, mwaka huu, majira ya saa 7:00 mchana katika eneo
lake la kazi kwenye Soko Kuu la mjini Sumbawanga, huku akiwa anaendelea na shughuli zake.
Hata hivyo, Mwakisyala amekana shtaka hilo na kurudishwa Rumande kwa kushindwa kupata wadhamini wawili wa Sh300,000 kila mmoja
wao.
Taarifa za awali za polisi zilidai kuwa mshitakiwa alikutwa na kichwa hicho kikiwa kenye mfuko wa rambo, ambapo alitarajia kukiuza kwa mteja wake kwa thamani ya Sh600,000, lakini kabla hajatimiza azma hiyo polisi hilo kwa kushirikiana na raia wema waliandaa mtego na kufanikisha kumkamata mtuhumiwa akiwa ameweka kifurushi hicho chenye kichwa cha mtu, chini ya meza yake ya ufundi.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Dhamin Zongo, kichwa hicho kimehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali Mkoa.