Na Daniel Mjema, Moshi
WATEJA wa nyama na wauzaji wa kitoweo hicho mkoani Kilimanjaro, wameanza kuingiza mzaha katika suala la kujikinga na ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa, kwa madai kuwa wataalamu hawasemi ukweli kuhusu ugonjwa huo.
Uchunguzi wa gazeti hili katika maeneo mbalimbali mjini hapa, umebaini kuwa siku
za mwanzo watu wengi walichukua tahadhari na kuacha kutumia kitoweo hicho, lakini kadri siku zinavyoenda hali inaendelea kubadilika.
Baadhi ya baa na hoteli ambazo zilifuta kabisa '_nyama choma'_ sasa wamerudisha upya kwa madai kwamba kinachotakiwa ni nyama iive vizuri kwa kutumia joto la nyuzi joto 60 na kuendelea.
_"Hapa kuna kitu serikali inatuficha, kama wanasema hao waliokufa walikula nyama, ina maana mtu mmoja tu alikula ng'ombe mzima mwenye kilo zaidi ya 200 peke yake? " alihoji mchinja nyama mmoja wa hapa.
Mchinja nyama huyo anayemiliki mabucha kadhaa ya kuuza nyama, alihoji waliko watu wengine waliokula nyama hiyo na kuiomba serikali itoa ufafanuzi katika suala hilo vinginevyo (wachinjaji) hawataielewa.
Meneja wa baa mashuhuri ya Oysterbay Executive iliyopo karibu na soko la Mbuyuni, mjini hapa, Bayi Nderemo, aliiomba Serikali kutoa elimu zaidi juu ya ugonjwa huo kuliko ilivyo sasa ambapo wananchi wanachanganyikiwa.
"Kuna maneno mengi yanazungumzwa juu ya ugonjwa huo, hivyo ni jukumu la serikali kusema waziwazi kwamba ni wakati gani nyama ikiliwa haitakuwa na madhara na inatakiwa ichemshwe au ichomwe kwa kiwango gani," alisema Nderemo.