Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI) pamoja na wamiliki wa vituo vya kuuzia mafuta Jijini Dar es Salaam, wameelezea kufurahishwa na bajeti ya mwaka wa fedha 2006/07 kama ilivyowasilishwa Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Fedha, Bi. Zakia Meghji.
CTI na wamiliki hao wa vituo vya mafuta, wamesema bajeti hiyo inakidhi matarajio ya wananchi walio wengi na kwamba hatua ya kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika petroli, ni dhahiri kuwa itasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza si tu bei ya nishati hiyo, bali pia hata bidhaa nyingine mbalimbali.
Makamu Mwenyekiti wa CTI, Bw. Jayesh Shah, kwa upande wake aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam jana.
’’Bajeti hii inakidhi matarajio ya wananchi hususan watu wa kipato cha chini na wafanyabiashara’’ alisema Bw Shah.
Alikuwa na Mkurugenzi wa CTI, Bi. Chtistine Kilindu pamoja na maofisa kadhaa wa shirikisho hilo.
Bw. Shah alisema bajeti hiyo imezingatia mapendekezo yaliyotolewa na CTI kwa Kamati maalum iliyokuwa ikifanya marekebisho ya kodi.
Akifafanua, alisema mapendekezo yao yalihusu jinsi ya kukuza uchumi, kuboresha ushindani, kuboresha kanuni na taratibu za kodi na usimamizi wa kodi.
Alisema bajeti ya mwaka huu imelenga katika masuala ya ukuzaji uchumi.
’’Ni maoni yetu kuwa endapo hatua zilizopende-kezwa kwenye bajeti hii zitatekelezwa vilivyo hakuna ubishi wa kukua kwa uchumi kwa asilimia 7.3 ifikapo mwaka 2007.’’
Aidha, alitoa mfano wa ongezeko la bajeti kwa asilimia 16 kutoka Sh.trilioni 4.176 kwa mwaka 2005/2006 hadi trilioni 4.85 kwa mwaka huu wa fedha wa 2006/2007.
Alisema ongezeko hilo litaongeza matumizi zaidi ya wananchi na Serikali kununua bidhaa zaidi hususan wafanyakazi wa umma waliongezewa mishahara kwa kiwango cha Sh. bilioni 318.
Kuhusu ongezeko la ruzuku katika kilimo, alisema hatua hiyo itasaidia kuboresha kilimo ambacho ni uti wa mgongo na hivyo kupunguza utege-mezi wa chakula, kuongeza mapato yatokanayo na usafirishaji wa bidhaa kwenda nje pamoja na malighafi za viwandani.
Aliongeza kuwa kitendo cha serikali kutenga fungu la fedha kwa miradi ya Ukanda Maalum wa Uchumi, Ukanda huru wa Biashara na usambazaji wa maji ya ziwa Victoria katika mikoa ya Shinyanga na Kahama kitasaidia kukuza uchumi katika sekta ya uzalishaji.
Kuhusu uboreshaji wa ushindani, alisema bajeti ya mwaka 2006/2007 itaboresha ushindani wa kibiashara hususan katika sekta ya uzalishaji viwandani.
Aidha, Bw. Shah alitaja hatua zilizohukuliwa na serikali kuwa ni pamoja na kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika mafuta ya petroli.
Alisema hatua hiyo itasaidia kupungua kwa bei ya mafuta nchini.
Aliongeza kuwa hatua ya kupunguza ushuru kwa karatasi zinazoingia nchini kutoka nje kutoka asilimia 25 hadi 10 itapunguza gharama ya uzalishaji wa magazeti na hivyo kuongeza ushindani.
Kadhalika, alisema ongezeko la ushuru kwa vibiriti vinavyoingizwa nchini kutoka asilimia 35 hadi 50 itasaidia kulinda viwanda vya humu nchini kutoka ushindani usio sawa.
Mambo mengine ni pamoja na msamaha wa ushuru wa VAT kwa gesi ya petroli, na mitungi ya gesi hatua aliyoielezea kuwa itawavutia wananchi kutumia gesi kwa ajli ya kupikia na hivyo kupunguza matumizi ya mkaa na kuni.
Hali kadhalika, punguzo la ushuru kwa mafuta ya taa kutoka Sh. 122 hadi Sh. 52 itawavutia wananchi kutumia mafuta ya taa badala ya kuni na mkaa.
Kuhusu kasoro zilizoko kwenye bajeti hiyo, Bw. Shah alisema ongezeko la ushuru wa kuingiza mafuta ghafi ya mawese kutoka sifuri hadi asilimia 10 itakuwa na madhara kwa wazalishaji wa mafuta ya kupikia.
Alisema matokeo ya ongezeko hilo ni kwa watu kukosa ajira, uwekezaji na kuzuia upanuzi wa uzalishaji wa mbegu za mafuta.
Aidha,alisema ongezeko la ushuru wa bidhaa za plastiki zilizopigwa marufuku kutoka asilimia 15 hadi 120 itawafanya watu kutozalisha mifuko ya plastiki na hivyo kuchangia kufungwa kwa viwanda vya plastiki na hivyo watu kukosa ajir .
Waandishi Raymond Kaminyoge na Lucy Lyatuu wanaripoti kuwa baadhi ya wamiliki na wafanyakazi wa vituo vya kuuza mafuta Jijini Dar es Salaam, wameipongeza hatua ya serikali ya kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye petroli.
Wamesema hatua hiyo itasaidia kupunguza bei ya mafuta pamoja na za bidhaa nyingine mbalimbali.
Mmiliki wa kituo cha mafuta cha GAPCO cha Jijini Dar es Salaam, Bw. Alli Suleiman, alisema hatua hiyo iliyochukuliwa na serikali ya kuiondoa kabisa VAT, imeonyesha huruma kwa wananchi.
’’Unajua mafuta yanapopanda, kila kitu hupanda, wananchi ndiyo wanaobebeshwa mzigo huo, hivyo kwa kweli serikali imeonyesha kwamba inawajali wananchi wake kwani maisha yamepanda sana kwa sababu ya bei kubwa ya mafuta,’’ alisema.
Alisema njia pekee kwa serikali kudhibiti kupanda kwa maisha kunakotokana na bei kubwa ya mafuta katika Soko la Dunia, ni kuondoa kabisa kodi katika bidhaa hiyo jambo ambalo serikali imefanya mwaka huu.
Alisema kwa vyovyote vile, mafuta yatakayoingia nchini baada ya bajeti hii, bei yake itabidi ishuke kwa sababu asilimia 20 iliyokuwa ikitozwa, sasa itakuwa haipo tena.
Mmoja wa wafanyakazi katika kituo hicho ambaye aliomba jina lake lisitajwe, alisema serikali isimamie kwa karibu sana wafanyabiashara wa mafuta kwani wengi wana tamaa ya kutaka faida kubwa zaidi.
Alisema pamoja na kuondoa VAT katika mafuta, bila kusimamiwa ipasavyo, wanaweza kuendelea kupandisha bei kama ambayo wamekuwa wakifanya hapo mwanzo.
’’Utashangaa wenye mafuta wamekuwa wakipandisha bei za mafuta hata pale bei katika Soko la Dunia inaposhuka, jambo ambalo ni kinyume na taratibu za kibiashara,’’ alisema.
Alisema matarajio ya wananchi sasa ni kwamba bei ya mafuta itashuka kwa kiasi fulani na hivyo kuzuia mfumuko wa bei katika bidhaa mbalimbali.
Kuhusu kupanda mishahara kwa watumishi wa serikali, wafanyakazi mbalimbali wameomba sekta binafsi pia kuchukua hatua kama hiyo kwa kuwa hali ya maisha imepanda kwa wananchi wote.
’’Mara nyingi mishahara ya makampuni binafsi inatofautiana sana na ile ya serikali, wamiliki wa makampuni hayo wanawanyonya wafanyakazi wao kwa kulipa mishahara midogo. tunaomba ifanane fanane ya ile ya serikali,’’ alisema.
Aidha, waliomba mishahara hiyo mipya ianze kutolewa mapema kwani katika miaka iliyopita ilikuwa ikichelewa kwa karibu mwaka mzima baada ya Bajeti.
’’Tunaomba mwaka huu mchakato mzima wa utayarishaji mishahara uende haraka ili wafanyakazi waweze kukabiliana na mfumko wa bei uliotokea kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu,’’ alisema.
Hata hivyo, kwa upande wake, mfanyabiashara wa maduka, Bw. Ephraem Joaquim (45), alisema bei ya vinywaji imekuwa ikiongezeka kila mwaka, hali ambayo inawafanya watu wasifurahie maisha baada ya kazi.
’’Napendekeza bei ya sigara iongezeke kama bajeti ilivyoonyesha, lakini kwa upande wa bia na soda, siafiki kwani kila mwaka zimekuwa zikipanda hali ambayo imekuwa ikisababisha watu wasifurahie maisha yao, alisema.
Hata hivyo, kwa ujumla alipongeza serikali kwa bajeti hiyo kwa maelezo kuwa, imeonyesha kujali maisha ya watu wa kawaida kwa kuongeza mishahara na kuondoa kodi katika petroli.
’’Mishahara ikipanda, si wafanyakazi tu watakaofaidika, bali jamii nzima kwa sababu fedha itakuwa kwenye mzunguko, hivyo kila mtu ataipata,’’ alisema.