Michael Uledi na Benton Nollo MAASKOFU na wachungaji wa Makanisa yote ya Mkoani Dodoma wametangaza kutoshirikiana na kiongozi yeyote wa dini anayekubaliana na suala la ndoa za jinsia moja.
Azimio la Viongozi hao wakuu wa makanisa mkoani Dodoma, limekuja baada ya kuwepo taarifa kuwa Askofu mmoja wa mkoani Dodoma, amekubali ndoa za jinsia moja na mitala.
Viongozi hao wamesema kuwa kitendo cha kufanya ushoga ni kinyume na maagizo ya Mungu na hivyo kiongozi yeyote asiyesimamia ukweli huo anastahili kutengwa.
Kauli ya Askofu huyo imetafsiriwa na wengi wa Wakristo wa mjini hapa kuwa ni yenye kutaka kuhalalisha masuala ya ndoa za jinsia moja na kwamba kutokana na mwelekeo huo, baadhi yao wameazima kutoshirikiana na kiongozi yeyote wa dini atakayeruhusu ndoa za jinsia moja.
Askofu huyo alikaririwa na BBC akitaka kutotengwa kwa watu mbalimbali wenye dhambi wakiwemo mashoga na wasagaji na hivyo kuzua mtafaruku mkubwa kwa waumini wa makanisa mbalimbali wa Mkoa wa Dodoma.
Baadhi ya waumini hao na viongozi wa makanisa mkoani Dodoma, wametangaza kutoshirikiana na kiongozi huyo kutokana na matamshi yake ambayo yanaonekana bayana kwenda kinyume na maadili ya ya ukiristo.
Wakizungumza katika kikao kilichojumuisha maaskofu, wachungaji na viongozi wengine wa dini, viongozi hao walisema kuwa kauli hiyo imetolewa na kiongozi wa ngazi kubwa na hivyo kuleta wasiwasi kwa mwelekeo wa kiimani wa kanisa na kwamba haiendani na misingi ya imani ya Kikristo na mila na desturi za Kiafrika.
Akofu huyo alinukuliwa na BBC akisema hakuna sababu ya kuwatenga waumini wengine kwa sababu ya dhambi zao na kwamba kulikuwa na umuhimu wa kuwashirikisha katika mambo mbalimbali ili neema ya Yesu iwakoe.
Hata hivyo, Askofu huyo huenda akajikuta akitengwa na waumini wake wakiwemo viongozi wa makanisa mbalimbali ambayo yako chini yake kutokana na kauli yake hiyo ambayo imechukuliwa kuwa ni ya usaliti.
Viongozi hao wa dini wa umoja wa makanisa ya mkoani Dodoma wamesema kuwa hawako tayari kushirikiana na kiongozi yeyote anayeshiriki kubariki uovu wa ndoa za jinsia moja.
Maaskofu na viongozi hao wamesema kuwa hawako tayari kushirikiana na kiongozi huyo kwa madai kuwa kauli yake inaonyesha kuwa inabariki ndoa za jinsia moja ambazo ni machukizo kwa Mungu na kwamba ni uvunjaji wa misingi ya Ukristo.
Kauli hiyo ya maaskofu na wachungaji wa makanisa yote ya kikristo mkoani Dodoma imekuja siku mbili tu baada ya kikao kikubwa cha Kanisa la Kianglikana kufanyika jijini Dar es Salaam, huku ajenda kubwa ikiaminika kuwa ni mgawanyiko uliojitokeza ndani ya kanisa hilo kuhusiana na ndoa za jinsia moja na ushoga.
Wachungaji na maaskofu hao kutoka makanisa yote ya mkoani Dodoma wametamka bayana kumtenga kiongozi huyo kwa kutoa kauli ya kuunga mkono ndoa za jinsia.
Viongozi hao wamesema kuwa inakera kuona kuwa kanisa la Kianglikana Duniani linaendesha harakati za kuruhusu viongozi mashoga katika makanisa, jambo linalokwenda kinyume na maandiko na maagizo ya Mungu.
Akichangia katika kikao hicho kilichoketi kujadili hoja hiyo, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Dodoma, Askofu Dk Peter Mwamasika, alisema kuunga mkono ushoga ama ndoa za jinsia moja ni kukiuka kanuni na misingi ya Kikristo.
Askofu Mwamasika alisema kama kuna jamii au taasisi inayounga mkono utamaduni huo, basi ni dhana potofu na inafaa kupigwa vita na wao kama umoja wa maaskofu na wachungaji wa makanisa yote ya Kikristo, Dodoma hawapo tayari kupigia chapuo suala hilo.
Askofu Mwamasika alisema wote (maaskofu) wanaounga mkono suala la ushoga na ndoa za jinsia moja, pamoja na ndoa za mitala kwa kusema kuwa ni utamaduni wa kiafrika, wamepotea.