Na Simon Berege, Zanzibar MPASUKO ndani ya Jumuiya ya Kanisa la Anglikan umezidi kupanuka baada ya Askofu Mkuu wa kanisa hilo nchini Nigeria, Peter Akinola, kushindwa kuungana na maaskofu wakuu wengine duniani kwenda Zanzibar kuhudhuria ibada iliyofanyika katika kanisa kuu la Kristu Mfalme la Mkunazini jana.
Askofu Akinola akiwa amejiondoa katika msafara huo, mpinzani wake, Askofu Mkuu mwanamke wa kanisa hilo nchini Marekani, Katherine Schori jana alikuwa kivutio miongoni mwa Maaskofu waliohudhuria misa hiyo
ya aina yake iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Canterbury, Dk Rowan Williams.
“Ni kweli hajaja” alieleza Mkurugenzi wa mawasiliano wa kanisa hilo, Robert Rosenthal, alipoulizwa juu ya kutokuwepo kwa Askofu huyo wa Nigeria lakini hata hivyo alisema bado alikuwa hajafahamu sababu ya Askofu huyo kutofika kwenye ibada hiyo.
Majuzi Askofu Akinola akiwa na maaskofu wengine Sita, walikataa kula Ekaristi mbele ya Askofu huyo wa Marekani ambaye anaunga mkono kuwepo kwa wachungaji na maaskofu mashoga katika kanisa hilo.
Akinola na maaskofu wakuu kadhaa wameweka msimamo wa kulitenga kanisa la Marekani kwa hatua yake ya kuunga mkono kuwekwa wakfu kwa Gene Robinson kuwa Askofu nchini Marekani pamoja na kanisa
hilo kumsimika Katherine ambaye ni mwanamke kuwa Askofu Mkuu.
Kwa upande wao wawakikishi wawili wa kutete haki za Mashoga na Wasagaji duniani, jana walionekana wakishiriki katika ibada hiyo baada ya kufanikiwa
kusafiri kwa boti iliyoandaliwa mahsusi kuwasafirisha maaskofu hao , wanahabari na maafisa wengine wa kanisa hilo.
Wanaharakati hao ni Mchungaji, Colin Coward kutoka Uingereza ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya kuhamasisha mabadiliko chanya ya mtazamo kuhusu Ushoga na Usagaji (CA) na Mkugenzi wa taasisi hiyo nchini
Nigeria, Davis Mac-Iyalla.
Hata hivyo Maaskofu wakuu walikuwa wametengwa ili wasionane na abiria wengine kwa kukaa sehemu ya juu huku wengine wakiwa sehemu ya chini na hakuna Mwanahabari yeyote aliyeruhusiwa kuwasogelea maaskofu
hao wala kufanya nao mazungumzo.
Akihubiri katika ibada hiyo, Askofu Mkuu Williams aliyataka mataifa tajiri duniani kuangalia adha ambazo mataifa maskini yanakabiliana nazo kisha kutafuta namna ya kuzisaidia.
Katika ibada hiyo iliyoanza saa 4:40 Dk Williams alisema kwa miaka mingi, watu wengi wakiwamo wakristo, hawakuona ubaya wa biashara ya utumwa iliyokuwa ikidhalilisha utu wa binadamu lakini kwa neema ya Mungu ikafikia siku wakafunguliwa macho kupata msukumo wa kujua dhambi hiyo.
Alisema kuna haja kubwa ya kumuomba Mungu kufungua macho ya wanadamu ili kuona yale wasiyopenda na kuweka wazi maovu ya kale kama ilivyokuwa biashara ya utumwa kasha kuchukua hatua badala ya kuyafunika kwa kujifanya hayapo.
“Upendo ndiyo utakaotufungua macho si takwimu wala mawazo “ alieleza Askofu huyo aliyekuwa amevalia joho la njano na Kofia ya Kiaskofu. Ibada hiyo iliongozwa na Askofu Mkuu wa kanisa hilo nchini, Dk. Donald Mtetemela.
Dk Williams alitoa zawadi ya sanamu yenye alama ya msalaba uliyotundikwa kwenye kanisa kuu la Canterbury nchini Uingereza kwa Msaidizi wa Askofu (Vicar General) wa Zanzibar, Mathew Mhagama naye alitoa zawadi mbalimbali kwa Askofu Mkuu huyo na maaskofu wakuu wengine waliyohudhuria ibada hiyo.
Leo maaskofu wakuu hao wanamaliza mkutano wao katika hoteli ya Whitesands jijini Dar es Salaam ambapo maamuzi makubwa kuhusu kanisa hilo yanatarajiwa kutolewa hasa baada ya kupitia mapendekezo kadhaa ya
ripoti mbalimbali ikiwemo ya Windsor hususan juu ya kanisa kuruhusu ama kutokuruhusu kubarikiwa kwa ndoa za watu wa jinsi moja na ile ya kuruhusu mashoga kuwa wachungaji au maaskofu.
Katika hatua nyingine Askofu mkuu wa Kanisa la Kianglikana duniani nchini Marekani ambaye anataka mabadiliko ndani ya kanisa hilo ya kururuhusu mashoga na ndoa za jinsi moja, Katherine Schori amesema hatalegeza msimamo wake hata kama suala hilo litasambaratisha kanisa hilo.
Msaidizi wa Askofu wa huyo alikaririwa ahirika la habari la kimataifa la AP mwishoni mwa wiki jijini Dar es salaam akisema kuwa suala hilo ambalo limo katika ripoti ya mwaka 2004 ya kanisa hilo nchini Marekani watalijadili.
Mgawanyiko wa kanisa la Anglikana umekuwa kwa miaka mingi lakini uliongezeka mwaka 2003 wakati kanisa hilo nchini Marekani lililompandisha katika daraja la uaskofu, V. Gene Robinson wa New Hampshire ambaye ni shoga