Na Maura Mwingira, London
RAIS Jakaya Kikwete amewapasha Watanzania wanaoishi ughaibuni ambao kwa makusudi waliamua kuziharibu pasi walizokuwa nazo kwa lengo la kuukataa uraia wao na nchi yao, kuwa serikali haitakuwa tayari kuwapatia pasi mpya za kusafiria.
Rais Kikwete alisema hayo juzi na jijini London, Uingereza alipokuwa akijibu maswali ya Watanzania wanaoishi na kuendesha shughuli zao nchini hapa.
Rais alilazimika kusema hayo, baada ya baadhi ya Watanzania wenye asili ya Zanzibar kumtaka rais atoe tamko litakalo ruhusu Watanzania hao kupewa pasipoti mpya zitakazowawezesha kupata kibali halali cha kuishi nchini Uingereza.
Wengi wa Wazanzibar hao ambao wamekwama kupata pasi za Tanzania ni wale waliokimbilia Uingereza kati ya mwaka 1995 na 1996, wakaomba hifadhi ya ukimbizi wa kisiasa kwa kisingizio cha hali mbaya ya kisiasa visiwani Zanzibar, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995.
“ Kama kuna anayejiita mkimbizi bila shaka aliingia hapa akiwa na pasipoti ya Tanzania na kama alipanda ndege hakuna ndege utakayopanda bila kuonyesha pasipoti, sasa nataka nipate ufafanuzi tatizo liko wapi, kama pasi imekwisha muda wake basi si aende tu akaongezewe muda, ” alihoji Rais
Aliongeza: “ Kama kuna mtu aliyeikana Tanzania akisema nchi gani ile hata kuishi haifai, mimi nataka kuishi hapa (London) na kama kuna mtu aliichana pasipoti yake, akaiponda Tanzania, ‘akajilipua’ sasa ametubu kwamba amekosa anataka apewe pasi yake ya Tanzania naye atueleze hapa ili na mimi nijue nianzie wapi”.
Rais alisema serikali haiwezi kutoa pasi kwa watu ambao waliamua kuzichana pasi zao (kujilipua) kwa kisingizio chochote kile, na hawana karatasi zozote za kuwatambulisha wao ni nani. Na kuongeza kuwa pasi hazitatolewa kwa kutumia kivuli cha pasipoti halisi (photocopy) kwa kuwa hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kufanya hivyo.
Alisema kama wanataka pasipoti za Kitanzania basi waende wakachukue pasipoti zao zilizochukuliwa na serikali ya Uingereza ili ziwarahisishie kupata pasi mpya.
Alibainisha kuwa yeye hawezi kutoa tamko lolote la kuwafanya Wazanzibar hao kupata pasi mpya, kwa kile alichosema kufanya hivyo ni kujitafutia sifa ambazo hazina maana yoyote kwake.
Alisema atamshangaa afisa yoyote wa uhamiaji au ubalozi wowote wa Tanzania, atakayempatia mtu pasipoti kwa kutumia kivuli cha pasi yake badala ya pasi yenyewe.
Kwa mujibu wa Wazanzibar hao, wanadai kwamba serikali ya Uingereza ilichukua pasipoti zao na kuwapa nakala na sasa inawataka kuonyesha pasi halali za Kitanzania ili iweze kuwatambua na kuwapatia hati kamili za kuishi nchini humo.
Aidha serikali hiyo ya Uingereza ilikataa kuwapa hadhi ya ukimbizi Wazanzibar hao kwa kile ilichodai kwamba hakukuwa na ukiukwaji wowote wa haki za binadamu nchini Tanzania, wala machafuko ya kisiasa kiasi cha kuzalisha wakimbizi. Badala yake, ilidai kwamba Wazanzibar hao walikuwa wanakimbia hali mbaya ya uchumi, kwa hiyo walikuwa ni wakimbizi wa kiuchumi.
Kutoka na wimbi la Wazanzibar hao kukimbilia Uingereza kwa kisingizo cha hali mbaya ya kisiasa, serikali ya Uingereza ililazimika kuanzisha utaratibu wa viza kwa kila Mtanzania anayeingia Uingereza pamoja na kwamba Tanzania kama mwanachama wa Jumuia ya Madola haikustahili kutozwa viza kuingia nchini humo.
Rais Kikwete ambaye alikutana na Watanzania hao akiwa njiani kuelekea katika nchi za Scandnavia, alibainisha kwamba kila Mtanzania ambaye pasi yake ya kusafiria imemaliza muda wake, anayo haki ya kuongezewa muda, na yule ambaye anahitaji kubadilishiwa pasi yake na kupewa mpya anayo haki ya kupewa hati mpya ilimradi anatimiza masharti yanayohitajika.
Aidha Rais alisema kwa Mtanzania ambaye kwa makusudi kabisa hakwenda kuongeza muda baada ya muda wa pasi yake kumalizika, asikimbilie kuilaumu serikali kwa kuwa ni kosa lake mwenyewe.
Akijibu swali kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na baadhi ya watendaji serikalini, Rais alisema kuwa hakuna mtu mwenye ruksa ya kuondoa maisha ya mtu mwingine, awe katika serikali au nje ya serikali na kwamba atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria bila ya kujali yeye ni nani na kwamba tayari serikali imekwisha kuanza kuchukua hatua hizo.
Kuhusu suala la ununuzi wa rada ambalo limekuwa gumzo katika vyombo vya habari katika siku za hivi karibuni, Rais alisema serikali imeiagiza Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB) kufanya uchunguzi utakaobaini kama kuna watu ambao walipokea rushwa katika mchakato mzima wa ununuzi wa rada hiyo.
Kuhusu ni lini mazungumzo ya kumaliza mpasuko visiwani Zanzibar yatakamilika na endapo maamuzi yatakayotokana na mazungumzo hayo yataheshimiwa na kutekelezwa.
Rais alisema hawezi kusema ni lini mazungumzo hayo ambayo hivi sasa yanaendelea kati ya Makatibu Wakuu wa CCM na CUF yatakwisha kwa kile alichosema kuna tofauti za msingi kati ya CCM na CUF zinazohitajika kufanyiwa kazi.
Leo Rais Kikwete anaanza ziara yake nchini Sweden, ambako pamoja na mambo mengine atakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wakuu wa nchi hiyo.