Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Serikali kuendesha tena vivuko vyake
http://www.habaritanzania.com/articles/3027/1/Serikali-kuendesha-tena-vivuko-vyake
By Habari Tanzania
Published on 02/18/2007
 
HATIMAYE serikali imeamua kuchukua kazi ya uendeshaji vivuko vyake vya Mv Alina na Kigamboni, baada ya kampuni ya Imalaseko kubwaga manyanga.

Na Ramadhan Semtawa

HATIMAYE serikali imeamua kuchukua kazi ya uendeshaji vivuko vyake vya Mv Alina na Kigamboni, baada ya kampuni ya Imalaseko kubwaga manyanga.

Imalaseko ilishinda zabuni ya kuendesha vivuko hivyo, ambapo moja ya kazi zake ilikuwa ni kusimamia ukusanyaji mapato.

Hata hivyo, Imalaseko iliacha kufanya kazi hiyo mapema mwezi uliopita, ikiwa ni mwezi mmoja tangu kukabidhiwa kazi.

Mkurugenzi wa ufundi na umeme wa Wizara ya Miundombinu, John Ndunguru, amelithibitishia Mwananchi Jumapili mwishoni mwa wiki.

Ndunguru alisema uamuzi wa kusitisha mkataba ulichukuliwa na Imalaseko yenyewe.

"Ni kweli wamesitisha mkataba, sasa serikali inasimamia yenyewe vivuko vyote viwili," alithibitisha Ndunguru.

Ndunguru alifafanua zaidi kwamba, serikali iliendelea kufanya ukusanyaji kwa majaribio kwa kutumia mashine maalumu za mfumo wa kompyuta ambazo zimeonyesha mafanikio.

"Tumekuwa tukifanya majaribio ya kutoa tiketi kwa kutumia mfumo wa kompyuta, kumekuwa na mafanikio sasa hivi taratibu za kuusimika zinaendelea vizuri," alisema Ndunguru.


Alisema hata ukusanyaji mapato ya serikali katika vivuko hivyo unakwenda vizuri kutokana na kuwepo udhibiti ambao umewezesha kukusanywa hadi sh 4.5 milioni kwa siku.

Serikali iliamua kutafuta kampuni binafsi ya kuendesha vivuko hivyo, ambapo Imalaseko na Dengard System zilishiriki zabuni. Katika zabuni hizo, Imalaseko iliahidi kuipatia serikali sh 100 milioni kwa mwezi wakati Dengard iliahidi kutoa sh 80 milioni.