Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete amemteua rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu kipya cha serikali kinachojengwa Dodoma.
Kikwete, pia amemteua aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Mohammed Gharib Bilal kuwa mwenyekiti wa baraza la chuo hicho kitakachoanza rasmi Septemba mwaka huu.
Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Petter Msolla alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa kuanzishwa kwa chuo hicho ni sehemu ya jitihada za serikali kukabiliana na changamoto ya ongezeko la wanafunzi wenye sifa za kujiunga na vyuo vya elimu ya Juu nchini.
"Rais, pia amemteua Profesa Idris Kikula kuwa Makamu wa Mkuu wa chuo kikuu cha Dodoma na Profesa Ludovick Kinabo kuwa Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho anayeshughulikia taaluma, utafiti na ushauri," alisema Msolla.
Aidha, alisema kuwa Profesa Shaaban Mlacha ameteuliwa kuwa Naibu Makamu wa chuo anayeshughulikia fedha, mipango na utawala