Na Lilian Lugakingira, Bukoba
Viongozi wakuu wa nchi za Afrika Mashariki, wameambiwa kuwa hakuna haja ya kuwauliza wananchi juu ya kuharakisha uundwaji wa Shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki, wakati viongozi hao tayari wamekwishatoa uamuzi kabla ya kupata maoni ya wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa jana katika kikao cha kukusanya maoni ya wananchi juu ya uharakishaji uundaji wa shirikisho hilo, kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera.
Diwani wa kata ya Rwamishenye, Dismas Lutagwelela, alisema kuwa kama viongozi wa nchi za Tanzania, Uganda na Kenya walikwishakaa na kuamua shirikisho hilo lianzishwe hakuna haja ya kutafuta maoni wa wananchi juu ya uharakishaji wa shirikisho hilo. Diwani huyo akashauri viongozi hao hao waliokaa bila kutafuta maoni wa wananchi kuona kama wanakubali liundwe, ndio wakae na kuamua kama liharakishwe au la!
Lutagwelela alisema kuwa, maoni ya wananchi yangekuwa na umuhimu zaidi kama wangeshirikishwa tangu mwanzo na kuwa, maoni yanayokusanywa hivi sasa hayana umuhimu maana hawakushirikishwa tangu awali.
Murungi Badru Diwani wa Viti Maalum katika manispaa hiyo alisema, serikali kwanza ingekusanya maoni ya wananchi kabla viongozi husika hawajakaa kutoa maamuzi na kusaini mkataba wa kuundwa kwa shirikisho hilo na kuwa, kutokana na hali hiyo ndio maana suala hilo linaleta mjadala na utata mkubwa kwa wananchi wanaotakiwa kutoa maoni yao.
Katika kikao hicho mawazo ya wananchi walio wengi walikubali kuundwa kwa shirikisho hilo lakini wakaomba lisiharakishwe kutokana na kuwepo kwa vikwanzo mbali mbali kama kutokuwepo kwa uwiano wa kiuchumi, elimu duni ya Watanzania na baadhi ya viongozi katika nchi husika kubadili katiba kwa lengo la kutaka kutaka madaraka ya juu ya shirikisho hilo.
Mengine yaliyozungumzwa ni pamoja na, kutokuwepo kwa utulivu wa kisiasa katika nchi hizo, hali waliyosema Tanzania isipojiandaa inaweza kukaribisha migogoro na mapigano kama yalivyo katika nchi za Rwanda na Burundi. Tena ilielezwa kuwa hata Kenya na Uganda bado hazijatulia kisiasa hivyo, wanaweza kuingia nchini na kuwachukua vijana na kuwafundisha masuala ya kivita wakati wao wamezoea kuishi katika nchi ya amani na kuhatarisha amani ya nchi.
Aidha wananchi hao walisema kuwa kabla ya kuundwa kwa shirikisho hilo masuala yaliyoko katika mkataba uliounda Jumuiya ya Afrika Mashariki kama umoja wa forodha, sarafu moja, soko la pamoja na baadaye shirikisho; utekelezaji wake ungetangulia kwanza na kupima mafanikio yake kabla ya kuunda shirikisho.
Naye Rais wa chama cha wafanyabiashara , wenye viwanda na wakulima nchini (TCCIA) ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo, Elivis Musiba, akitoa ufafanuzi juu ya malalamiko hayo ya wananchi alisema wakati wa mchakato wa kukubali kuunda shirikisho hilo wananchi walishirikishwa na kutoa maoni yao na kuwa sio kweli kuwa hawakushirikisha wananchi kama mawazo ya wananchi wengi yanavyodai ingawa haikuwa rahisi kuwashirikisha wananchi wote.
Musiba alisema kuwa, mbali na viongozi wa nchi hizo kukubali kusaini mkataba wa kukubali kuundwa kwa shirikisho hilo hata ripoti ya Amos Wako Mwanasheria Mkuu wa Kenya aliyekuwa akiongoza Tume ya kufanya uchunguzi kama kuna umuhimu wa kuharakisha kuunda shirikisho hilo inaonyesha wananchi walioshiriki.