MAASKOFU wa Kanisa la Anglikana duniani leo wanahudhuria ibada ya misa takatifu itakayofanyika mjini Zanzibar baada ya siku kadhaa za za mkutano wao mkuu unaomalizika kesho, anaripoti Simon Berege.
Mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Mkuu wa Canterbury, Dk. Rowan Williams amepangiwa kuhubiri katika ibada hiyo itakayoongozwa na Askofu Mkuu wa kanisa hilo nchini, Dk. Donald Mtetemela.
Rais wa Zanzibar Aman Abeid Karume ataungana na maaskofu hao baada ya ibada hiyo kwa ajili ya chakula cha mchana.
Kesho, maaskofu hao ambao wamekuwa wakikutana kwenye hoteli ya Whitesands, nje kidogo ya Dar es Salaam wanatarajiwa kutoa maamuzi mazito yanayosubiriwa na ulimwengu mzima hasa kuhusu msimamo wa kanisa kuhusu hoja ya ama kuruhusu au kukataa ndoa za jinsia moja, utaratibu unaotishia kuligawa kanisa hilo
Juzi, maaskofu wakuu saba waligoma kupokea komunio wakiwa kikaoni hapo kama alama ya kupinga kuwepo kwa Askofu Mkuu wa Marekani, Katherine Schori ambaye ni mwanamke wa kwanza kupewa cheo hicho nchini Marekani ambaye pia anaunga mkono ushoga.
"Suala la kupokea sakramenti (komunio)ni la mtu binafsi na jinsi alivyojiandaa kwa hiyo siwezi kueleza kwa undani juu ya uamuzi wao huo," alieleza msemaji wa maaskofu hao, ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Australia, Phillip Aspinall wakati akitoa taarifa kwa wanahabari baada ya kuisha kwa mkutano huo.
Kati ya Maaskofu waliyosusia sakramenti juzi anatajwa Askofu Mkuu wa Nigeria, Peter Akinola, kiongozi wa maaskofu wanaopinga ushoga kwa nguvu zote.Pia, anapinga wanawake kuwekwa wakfu kuwamaaskofu au wachungaji.
"Hii ni hatua nzuri kwetu kwani inaonekana kundi la wahafidhina linapungua nguvu," alieleza Mchungaji Colin Coward kutoka nchini Uingereza ambaye yuko nchini kwa ajili ya kushawishi viongozi hao kukubali ushoga. Habari zinasema katika kikao kilichopita mwaka 2003, maaskofu 14 waliogomea kupokea na kula sakramenti.