Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Wabunge wa CCM wamshtukia Rais Kikwete
Wabunge wa CCM wamshtukia Rais Kikwete
By Habari Tanzania | Published  02/18/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

Na Mwandishi Wetu

SIKU chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kukutana na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM); na kuwataka wawe huru kuikosoa serikali, kauli hiyo imepokewa kwa hisia tofauti na wabunge hao ambao wamedai mwenyekiti wao anawachezea shere.

Rais Kikwete katika kikao hicho kilichofanyika Jumapili iliyopita katika Ukumbi wa Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam aliwataka wabunge wa CCM wawe huru katika kuikosoa serikali kwa kupitia vikao vya kamati ya wabunge wa chama iliyo chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

"Kamati yenu ya wabunge wa chama ndio mahala penu pa kuuliza maswali yote mliyonayo na kuikosoa serikali katika mambo mbalimbali, hapo ndio mahali penu na ni wajibu wenu kuitumia fursa hiyo kikamilifu," chanzo chetu cha habari kilimnukuu Rais Kikwete akisema. Katika kutoa changamoto hiyo na kueleza namna kamati hiyo ilivyo na nguvu, Rais Kikwete anadaiwa kutoa mfano wa namna mawaziri wawili wa serikali ya awamu ya tatu walivyopoteza nyadhifa zao kutokana na hoja zilizoanza kutolewa katika kamati kama hiyo.

Mawaziri hao, Profesa Simon Mbilinyi aliyekuwa Waziri wa Fedha (akiwa pia Mbunge wa Peramiho) katika ngwe ya kwanza ya awamu ya tatu alijikuta akilazimika kujiuzulu kutokana na kashfa ya kutoa msamaha wa kodi kwa minofu ya samaki kinyume cha utaratibu, jambo ambalo lilivaliwa njuga na wabunge wa CCM mpaka kufikia hatua hiyo.

Waziri mwingine ambaye naye Kikwete alimtaja kama mmoja wa mawaziri waliowahi kuonja joto ya makali ya kamati hiyo ni Idd Simba (aliyekuwa Mbunge wa Ilala) ambaye alikuwa Waziri wa Viwanda na Biashara wakati huo na kukumbwa na shutuma za ukiukaji wa taratibu za kazi katika kutoa vibali vya kuagiza sukari. "Wabunge wakiwa na swali lolote wahoji katika kamati hii, kilichomwondoa Prof Mbilinyi na minofu ya samaki ni kamati hii, Idd Simba na sukari, pia ni zao la kamati hii.

Kwa hiyo wabunge wakiwa na maswali waulize hapo na wapewe majibu, wakiwa na maswali kuhusu Richmond pia waulize hapo na wajibiwe," Kikwete alidaiwa kusema. Kinachowafanya baadhi ya wabunge hao kudai kuwa Mwenyekiti wao wa chama anawahadaa na kauli zake hizo, ni kauli yake ya kusema wabunge wakiwa na maswali kuhusu suala la kampuni ya Richmond waulize na wapewe majibu.

Kilichowachanganya baadhi ya wabunge hao ni ukweli kuwa tayari wabunge wa CCM walikwishatoa hoja zao zinazohitaji majibu juu ya kampuni hiyo na mkataba wake katika kikao cha kamati yao kilichofanyika wakati wa kikao cha sita cha Bunge kilichoahirishwa Februari 9, mjini Dodoma. Pamoja na wabunge hao kuhoji maswali mazito yakiwamo shutuma kuwa baadhi ya viongozi waandamizi wa chama na serikali ni miongoni mwa watu wa karibu wa kampuni hiyo na kuufanya mkutano huo kuwa changamoto kubwa kwa serikali, hawakupewa majibu yoyote.

"Sina shaka kuwa Rais anajua vema yaliyojiri katika kile kikao chetu Dodoma, sasa kama kweli Rais anamaanisha hayo aliyotuambia, mbona asimwambie Waziri Mkuu wake atoe majibu ya maswali aliyoulizwa Dodoma kuhusu kampuni hiyo ambayo mpaka leo hatujayapata? Kuendelea kutuambia tuulize maswali ambayo tayari yameulizwa ni kutuhadaa, tunachotaka sasa ni majibu yaliyonyooka si kuuliza maswali tena," alisema mbunge mmoja.

Kwa kuwa kamati hiyo ya wabunge wa CCM iko chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu, tafsiri ya ujumbe wa Rais pia inaweza kumaanisha kuwa alikuwa akimwagiza Waziri Mkuu wake awape majibu wabunge kuhusu suala hilo la Richmond lililojaa utata mkubwa. Kikao cha kamati ya wabunge wa CCM kilikaa Alhamisi ya Februari Mosi, mjini Dodoma na taarifa za ndani zilizoandikwa katika vyombo mbalimbali vya habari na kuthibitishwa na baadhi ya wabunge waliohudhuria kikao hicho, zilisema baadhi ya wabunge wa chama hicho walionyesha ujasiri wa hali ya juu pale walipoihoji waziwazi serikali juu ya kampuni hiyo na mazingira ya mkataba wake na kuitaka serikali iwaeleze ukweli juu ya suala hilo.

Wabunge hao inadaiwa kuwa walicharuka vilivyo ndani ya kikao hicho na kudai kuwa suala la Richmond sio tu limeiaibisha serikali, lakini pia linawaweka mahala pabaya wabunge na kuwachafua katika macho ya wananchi ambao wanataka majibu ya kina juu ya suala hilo. Katika kikao hicho, wabunge hao walizipinga vikali taarifa zilizowasilishwa kwao na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati Richmond ikipewa mkataba huo, Dk Ibrahim Msabaha na waziri wa sasa, Nazir Karamagi, juu ya suala hilo.

Wabunge hao pia walihoji mantiki ya Dk Msabaha kutoa maelezo kwao wakati tayari alikuwa amekwisha kuondolewa katika wizara hiyo. Kufuatia hoja nzito zilizotolewa katika kikao hicho kilichokuwa cha ndani, wabunge hao walitaka Kamati ya Bunge ya Biashara na Uwekezaji iliyo chini ya William Shelukindo kuwasilisha ripoti yao juu ya suala hilo kwao ili waijadili kwa kina na kama wakifikia muafaka ndipo wakubaliane namna ya kulikabili suala hilo.

Hata hivyo, mpaka Bunge linaahirishwa Februari 9, ripoti hiyo haikuwasilishwa si katika kamati hiyo ya wabunge wa CCM wala ndani ya Bunge na mpaka sasa haijaeleweka ni kwa nini ripoti hiyo haikujadiliwa na hatima yake ni nini.

Katika kikao cha Jumapili, Rais Kikwete pia anadaiwa kuwaambia wabunge hao wa chama chake kuwa katika kuhoji serikali wasiporidhika na majibu watakayopewa, wanaweza kumtumia katibu wa kamati hiyo ili awasilishe masuala yao kwake na atayashughulikia kikamilifu. Katibu wa kamati ya wabunge wa CCM ambaye ni mbunge wa Fuoni, Ali Ameir Mohammed, ndiye aliyechaguliwa katika kikao cha Bunge cha Novemba mwaka jana katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali. Pamoja na Rais Kikwete kutoa changamoto hiyo, katika kikao hicho hakuna mbunge yeyote aliyeuliza swali kuhusu Richmond na wote waliopata nafasi ya kuuliza, waliuliza masuala mengine tofauti ikiwamo ya ahadi za chama kwa wananchi na ubovu wa miundombinu, hususan barabara. Kikao hicho ajenda kuu ilikuwa ni wajibu wa wabunge wa chama tawala bungeni, mada iliyotolewa na Spika mstaafu Pius Msekwa.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.