Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Homa Bonde la Ufa pigo kiuchumi Tanzania
Homa Bonde la Ufa pigo kiuchumi Tanzania
By Habari Tanzania | Published  02/18/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

Na Mwandishi Wetu

KUIBUKA kwa Homa ya Bonde la Ufa (RVF) nchini, kiasi cha wiki mbili zilizopita kumekuwa zaidi kukitazamwa kama janga la kiafya, kuliko la kiuchumi.

Lakini, ukiangalia kwa umakini zaidi, ugonjwa huo usio na tiba unaelezwa kwamba umeanza kuiathiri kiuchumi Tanzania katika sekta ya mifugo ambayo mchango wake licha ya udogo wake katika pato la taifa ni muhimu na unahitajika.

Serikali ya Awamu ya Nne pamoja na mikakati yake mingine ya kukuza uchumi ilipanga kuona kwamba, sekta ya mifugo inakua, kupanuka na kuzidi kuchangia uchumi wa taifa.

Kabla na hata baada ya kuingia madarakani, serikali hiyo imekuwa ikitarajia kuendelea kuifanya sekta hiyo kuwa mchangiaji mwingine muhimu katika pato la taifa.

Hadi sasa, serikali imekiri kutenga zaidi ya Sh2 bilioni kwa ajili ya chanjo ya ugonjwa huo na mapema wiki hii, Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, alikaririwa akisema kwamba kiasi hicho kimekwisha kutolewa.

Wasiwasi unaoibuka ni kwamba fedha hizo huenda zikaathiri sekta nyingine za utendaji serikalini na utoaji wa huduma.

Akiahirisha Bunge mapema mwezi huu mjini Dodoma, Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alieleza kuwa zingetumika Sh800 milioni kukabiliana na homa ya Bonde la Ufa.

Meghji alieleza kuwa fedha hizo zimekabidhiwa kwa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo ambazo Mkurugenzi wake, Dk Johnson Mollel, anasema kuwa dawa hizo za chanjo zitaingizwa nchini kutoka Afrika Kusini na zitakuwa zimewasili katika kipindi cha wiki mbili.

Waziri Meghji alisema kuwa, fedha hizo zitatumika kwa kampeni ya kuhamasisha jamii kuhusu jinsi ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo ambao umeripotiwa kujitokeza katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga na Morogoro, ambako watu kadhaa wameripotiwa kufa au kuugua.

Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005, inaainisha azma ya chama hicho na serikali zake katika kuhakikisha kuwa sekta ya mifugo inazidi kuchangia kwa kiasi kikubwa zaidi kuliko ilivyo sasa katika kuondoa umaskini na kutoa mchango zaidi katika pato la serikali.

Ili kufikia azma hiyo, ilani hiyo inaeleza kuwa CCM ilijiwekea malengo ya mwaka 2005-2010 ya jinsi ya kuendeleza na kuboresha mchango wa sekta hiyo.

Miongoni mwa malengo na mikakati ni pamoja na kujenga mazingira ya kuvutia wawekezaji katika sekta hiyo kwa kuongeza thamani kwa mazao yote yatokanayo na mifugo kama vile nyama, maziwa, ngozi na kadhalika na kuhakikisha mazao hayo yanachangia katika pato la taifa.

Azma nyingine ni kuwashawishi Watanzania wale nyama, mayai na kunywa maziwa zaidi kwa ajili ya kujenga miili na afya zao na pia kukuza soko la ndani na nje la mazao hayo yatokanayo na mifugo.

Hata hivyo, ilani hiyo inaonya kuwa pamoja na kwamba Tanzania ina mifugo mingi, lakini mchango wake kwenye uchumi wa taifa ni mdogo. Hivyo suala la kuongeza ubora katika sekta hiyo halina budi kuangaliwa na kuzingatiwa zaidi.

Takwimu rasmi za Wizara ya Mifugo kupitia Bajeti ya mwaka 2006/07, zinaonyesha kwa mfano, pamoja na Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (Mkukuta), kueleza wazi mchango wa sekta ya mifugo kwa maendeleo ya nchi katika kuondoa umaskini, hadi sasa mchango huo ni mdogo mno, jambo ambalo lilichangiwa na RVF, hakika mambo yanazidi kuharibika.

Sambamba na hilo, wafugaji mmoja mmoja, walaji, wasafirishaji, wachungaji na hata wauza nyama, nao wamekuwa wakilalamikia kuporomoka kwa vipato vyao binafsi.

Tanzania inakadiriwa kuwa na ng'ombe 18.5 milioni, mbuzi 13.1 milioni, kondoo 3.5 milioni, kuku wa asili 33 milioni, wa kisasa 11 milioni na nguruwe 1.2 milioni, lakini ina kiwango cha chini cha ulaji wa nyama, maziwa na mayai.

Hata kabla ya kuzuka kwa RVF, kiwango cha ulaji wa nyama kilikuwa kwa wastani wa kilo 11.5 kwa Mtanzania kwa mwaka huku ulaji wa mayai ukiwa wa mayai 64 kwa kipindi hicho.

Wasiwasi mkubwa ambao unawakumba wataalam wa sekta za afya, lishe na mifugo ni kuendelea kushuka kwa kiwango hiki ambacho, hata hivyo ni cha chini.

Kwa mfano, mtaalam mmoja wa lishe anaeleza kuwa kuzuka kwa RVF ambako kumesababisha kuporomoka kwa mauzo ya nyama katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, kwa kiasi kikubwa kuna madhara kwa uchumi pia.

Takwimu hizo zinaonyesha kwa mfano kwamba uzalishaji wa nyama ambao kwa mwaka 2004/05 ulikuwa wa tani 378,509, ambazo zilifikia tani 388,294 kwa mwaka 2005/06, zitashuka zaidi mwaka huu kutokana na kuzuka kwa homa hiyo.

Kulingana na takwimu hizo, ng'ombe ambao wameathiriwa zaidi na homa hiyo, kwa kipindi cha mwaka jana walichangia tani 210,370 za nyama.

Wizara ya Maendeleo ya Mifugo ilieleza mwaka jana kwamba, Tanzania ilifanya biashara ya mifugo kwa kuuza ng'ombe 364,453 na kuingiza kiasi cha Sh43.7 bilioni kutokana na soko la ndani, ambalo linakabiliwa kwa kiasi kikubwa na changamoto inayotokana na kuzuka kwa homa hiyo.

Wasiwasi mwingine ni kwa soko kubwa la ng'ombe wa Tanzania ambalo liko katika nchi za Comoro, Burundi ambalo linatishiwa na kuzuka kwa homa hiyo. Mwaka jana kiasi cha ng'ombe 1,706 waliuzwa huko na kuingiza kiasi cha Sh647.9 milioni.
Mazao mengine yatokanayo na mifugo, hasa ng'ombe ambayo kwa kiasi kikubwa yanatishiwa na kuwapo kwa homa hiyo ni ngozi, ambazo ziliuzwa nje vipande 1.9 milioni kwa ng'ombe, 1.4 milioni kwa mbuzi na 960,000 kwa kondoo na kuiingizia Tanzania kiasi cha Sh6.8 milioni kwa mwaka jana.

Hata hivyo, makadirio ya serikali ya kuuza vipande 4.4 milioni vya ngozi ya ng'ombe katika soko la kimataifa, pia lipo hatarini na hivyo kutishia mapato ya Sh3.9 bilioni ambazo awali zilitarajiwa kupatikana.

Rais Jakaya Kikwete, kwa mfano wakati akizindua Bunge mjini Dodoma, Desemba 30, 2005 alisisitiza umuhimu wa kuondokana na uchungaji ambao ni ufugaji wa kuhamahama na badala yake kuibadili sekta hiyo kuwa ya kisasa na endelevu.

Wakati alipotembelea Wizara ya Maendeleo ya Mifugo, Januari 18, mwaka jana, Kikwete pia aliishauri Wizara hiyo kuhakikisha inabuni mbinu za kuhakikisha inaongeza mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa.

Aidha, alishauri kupatikana kwa masoko zaidi ya mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi, ili kuhakikisha sekta hiyo inachangia katika kukua kwa uchumi wa Tanzania.

Dhamira hiyo ya Rais Kikwete kutaka ufugaji ambao ni wa kisasa, kitaalam, unaoendana na azma ya kuondokana na uchungaji, inaingia majaribuni kutokana na kuzuka kwa RVF, huku baadhi ya wafugaji wakihamishiwa mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma ambako huenda homa hiyo ikisambaa nchi nzima, pia ikawafikia.

Jambo linalotia wasiwasi ni kuwa, wakazi wa maeneo hayo, si wafugaji wa asili, hawana uwezo mkubwa, jambo ambalo linaelezwa kuwa endapo RVF itasambaa hadi huko, huenda ikachukua muda kwa chanjo kuwafikia.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.