Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Twaikumbusha serikali kuanza kutekeleza ahadi
Twaikumbusha serikali kuanza kutekeleza ahadi
By Habari Tanzania | Published  02/17/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

TULIANDIKA, tukaandika tena na sasa tunaandika kwa mara nyingine tena. Tutaendelea kuandika na kulifuatilia suala hili hadi hapo tutakapoona limemalizika na kuhitimishwa.

Ni miezi zaidi ya mitano imepita tangu Rais Jakaya Kikwete, na baadaye Naibu Waziri wa Miundombinu, Dk. Milton Mahanga, walipotangaza kuhakiki na kuanza kufikia urejeshwaji wa baadhi ya nyumba za serikali zilizouzwa katika mazingira yaliyoibua shaka.

Uamuzi wa serikali kuzirejesha nyumba hizo, ulitangazwa hadharani kwa mara ya kwanza na Rais Kikwete wakati alipokuwa akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, Ikulu jijini Dar es Salaam, mwanzoni mwa mwezi Oktoba.

Zaidi ya mwezi mmoja tangu atoe kauli hiyo, Mahanga aliusisitizia uamuzi huo bungeni mjini Dodoma.

Kama alivyosema Rais Kikwete, Mahanga katika kauli yake hiyo ya bungeni, alieleza baadhi ya nyumba zitakazorudishwa ni zile ambazo ziko katika maeneo nyeti kama vile hospitalini na katika maeneo ya majeshi.

Hata hivyo, Mahanga hakuishia hapo, bali alikwenda mbali zaidi na kusema, sehemu ya nyumba zitakazorejeshwa, ni zile ambazo uuzwaji wake haukufuata taratibu halali za kiserikali.

Tukiwa ni sehemu ya Watanzania ambao tumekuwa tukilifuatilia jambo hili kwa muda mrefu, msimamo wetu wa kupingana kabisa na maamuzi ya serikali kuuza nyumba za serikali, unaendelea kubakia ule ule.

Kama tulivyokwishaandika mara kadhaa siku zilizopita, sisi wa Tanzania Daima, kwa dhati kabisa tunaamini, maamuzi ya Baraza la Mawaziri la Serikali ya Awamu ya Tatu, ya kuuza nyumba za serikali kwa watumishi wake, bila kujali iwapo walikuwa na sifa au hawakuwa nazo, ni mabaya na ambayo kimsingi yalipaswa kubatilishwa kabisa.

Tunasema ni ya hovyo kwa sababu, maamuzi hayo yalifanywa katika misingi ya kibinafsi na yalilenga kulisaidia kundi dogo la viongozi na kusahau kwamba, dhamana ya mtu kuwa mtumishi au kiongozi wa serikali, ni ya muda tu na wala haimpi nafasi ya kumiliki mali ambazo kimsingi zingekuja kutumiwa na viongozi wajao wa umma.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo basi, ndiyo maana tunakiona hata hiki kitendo cha serikali kuendelea kukaa kimya pasipo kueleza mahali ilikofika katika kufanikisha zoezi hili muhimu kwa maslahi ya taifa.

Hata hivyo, wakati tukitaka kusikia matokeo ya operesheni hiyo ya kimya kimya ya serikali, tunapenda kutumia fursa hii kusisitiza msimamo wetu wa kutaka nyumba zote zilizouzwa, zirejeshwe na si baadhi.

Tunasema hivyo tukitambua kwamba, uamuzi mzima wa kuziuza nyumba hizo, ulifikiwa kwa makosa na kwa hiyo unapaswa kutenguliwa, na serikali kuangalia namna ya kulipana na hao wanunuzi wake.

Ni jambo lisiloingia akilini, kwa serikali kudai kulikuwa na kasoro katika suala zima la uuzwaji wa nyumba hizo, na halafu ikasisitiza tu kuwa zitakazorejeshwa ni baadhi tu.

Tunachokiona sisi ni kwamba, iwapo uamuzi wa kuzirejesha nyumba utafanywa nusunusu, basi kuna hatari kubwa kwa makosa kama yale yaliyotokea wakati wa operesheni ya mwanzo, yatatokea tena.

Tunasema hivyo, tukitambua baadhi ya viongozi walioamua kuuza nyumba zile wakati ule, wangali wapo ndani ya baraza hili la mawaziri na kuwa, haitakuwa rahisi kwao kutengua maamuzi ambayo kimsingi ndio walioyasimamia.

Ili tuweze kuondokana na wingu la shaka ambalo tayari limeshaanza kutanda, tunaiomba serikali yetu kutueleza kwa wazi kabisa ilipofikia sasa katika kulisimamia suala hilo, ambalo lilitolewa kauli na rais mwenyewe miezi zaidi ya minne iliyopita.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.