TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekataa kuanza kuutumia sasa, uamuzi wa Mahakama Kuu wa kutaka wagombea binafsi waruhusishwe.
Uamuzi huo wa NEC unamaanisha kuwa, uchaguzi mdogo wa Jimbo la Tunduru, ambao mchakato wa maandalizi yake umeshaanza, utafanyika ukiwahusisha wagombea wa vyama vya siasa tu, kinyume cha shinikizo la asasi kadhaa za kiraia.
Taarifa ya Mwenyekiti wa NEC, Jaji Lewis Makame, iliyotolewa jana, ilitaja sababu kadhaa ambazo zimesababisha tume yake iamue kutoanza kuruhusiwa kwa wagombea binafsi katika chaguzi kadhaa ndogo za udiwani na ubunge kabla ya mwaka 2010.
Makame alisema moja ya sababu hizo ni ukweli kwamba, kilichofanywa na mahakama ni kutangaza ibara katika katiba, ambazo zinatoa uhuru wa kutoruhusiwa kwa wagombea binafsi, huku nyingine zikionyesha kuwapo kwa uhuru huo.
Aliitaja sababu ya pili kuwa ni ukweli kwamba, hukumu hiyo ya Mahakama Kuu ilikuwa ikiielekeza serikali kuanza kufanya mabadiliko ambayo hatimaye yataruhusu kuanza kwa wagombea binafsi wakati wa uchaguzi mkuu ujao, mwaka 2010.
“Maamuzi hayo yanaielekeza serikali kuandaa utaratibu wa kisheria kuwezesha wagombea binafsi kushiriki katika chaguzi mbalimbali ifikapo uchaguzi mkuu ujao, kwa mujibu wa ibara ya 30 (5).
“Kwa sababu hiyo basi, NEC inautafsiri uamuzi huo kuwa, unamaanisha sheria isiyoruhusu ushiriki wa wagombea binafsi itaendelea kuwa halali na hivyo kuendelea kutumika mpaka muda uliotolewa na Mahakama Kuu utakapokwisha au serikali itakapofanya marekebisho katika sheria na kuruhusu wagombea binafsi kushiriki katika chaguzi mbalimbali,” alisema Jaji Makame.
Katika taarifa yake, Jaji Makame alisema kuwa, kwa mahakama kutoa maamuzi hayo, haina maana kuwa ibara husika za katiba zimefutwa.
“Utaratibu ni serikali kutayarisha muswada na kuuwasilisha bungeni na kama Bunge likiridhia, ndipo Ibara husika zinaweza kufutwa au kubadilishwa, na mpaka sasa mchakato huo haujafanywa na serikali, na hii ina maana kwamba, ibara zinazokataza mgombea binafsi hazijabadilishwa,” alisema Jaji Makame.
Alisema kuwa, pamoja na serikali kutoanza mchakato, pia Mwanasheria Mkuu alitoa taarifa ya kusudio la kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa, hatua ambayo inazuia utekelezaji wa maamuzi yoyote hadi hapo rufaa itakaposikilizwa.
“Kutokana na sababu hizo, tume itaendelea kuendesha chaguzi zinazokujua kwa kufuata misingi ya sheria kama ilivyo hivi sasa, mpaka hapo ibara husika itakapofutwa na serikali kukamilisha maandalizi ya sheria itakayoruhusu na kuwawezesha wagombea binafsi na sheria hiyo kupitishwa na Bunge. Kwa hiyo tume haitasitisha uchaguzi mdogo wa Tunduru kama ilivyotarajiwa na baadhi ya asasi za kiraia,” alisema.