Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Sauti za Busara zilizokosa busara
Sauti za Busara zilizokosa busara
By Habari Tanzania | Published  02/16/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated

WAPENZI wasomaji, leo tuzungumzie tamasha la Sauti za Busara ambalo hivi karibuni limefanyika kwa mara ya pili mfululizo kule mjini Unguja, Zanzibar.

Kubwa la kuzungumzia leo ni juu ya tamasha hili kukosa hamasa, hasa ukizingatia ni tamasha kubwa Afrika Mashariki na Kati, linalowashirikisha wasanii wengi kutoka nchi mbalimbali duniani.

Jambo la kusikitisha ni namna tamasha hilo linavyoshindwa kupenya ndani ya mioyo ya Watanzania tofauti na tamasha kama la Fiesta ambalo likifanyika huvuta watu wengi.

Kwa tamasha la Sauti za Busara, Watanzania wengi huwa hawafahamu kinachoendelea ndani yake, na mbaya zaidi, waandaaji wamekuwa wakimnadi msanii mmoja tu mkongwe, Fatma Baraka ‘Bi Kidude’ kama ndiyo mbiu ya tamasha hilo. Kila mwaka tamasha hili linapofanyika, utasikia mara ooh maisha ya Bi. Kidude, mara Bi. Kidude anasema hivi, kwani hakuna wakongwe wengine, mbona tuna wasanii wengi wa kuwapa heshima?

Nina imani wapo watakaopingana na mimi, lakini katika hili naenda sawa. Kwanini wasiwatangaze wasanii kama Issa Matona, Moris Nyanyusa, Hukwe Zawosa, Siti binti Saad, Mbaraka Mwinshehe, Hemed Maneti, Nico Zengekala ‘Steve Wonder’ wa Tanzania na wengine wengi? Kufanya hivyo, itasaidia kuwapa historia nzuri ya muziki watoto wetu ambao tusipokuwa makini, hawatafahamu historia ya muziki wa nchi yao.

Hivyo basi, kwa kuwa sisi ndiyo wenyeji wa tamasha hili la Sauti za Busara, ni vyema tukauenzi muziki wa nyumbani sambamba na wanamuziki wetu pia.

Sauti za Busara ni neno zito lenye hekima. Pia tamasha hili lipo chini ya bodi yenye watu ambao sanaa iko ndani ya damu yao, nao ni Mwenyekiti wa Bodi, Ismail Mohamed, Makamu Mwenyekiti ambaye pia ni Mkurugenzi wa bendi ya Kilimanjaro ‘Njenje’, Waziri Ally, Mweka Hazina Hildergard Kiel pamoja na wajumbe waanzilishi Rugemarila Mutahaba, Ahmed Juma, Yusuf Ahmed Aley na Emerson Skeens.

Hivyo basi, tunategemea katika miaka ijayo hasa kuanzia mwakani, wahusika na tamasha hilo, mtatuonyesha na kutufahamisha mafanikio na maisha ya wasanii wengine wakongwe na si kumrudia mkongwe mmoja tu kila mwaka.

Katika kumbukumbu zangu, nakumbuka tamasha la mwaka jana kulikuwa na mambo hayo hayo ya Bi Kidude ya kufahamu historia yake ya miaka 93 iliyopita na mwaka huu ikatangazwa filamu ya maisha yake. Kwa kweli hili linawavunja moyo wasanii walio wengi na hata hao wasanii wanaoalikwa kutoka nje ya nchi, wanashindwa kuelewa kama Tanzania kuna vikongwe wengine wa fani zaidi ya bi mkubwa huyo.

Si kama kwamba simfagilii bibi huyu, hapana, nampenda kwelikweli, hasa nikimsikia akiimba wimbo wake wa ‘Muhogo wa Jang’ombe’ ambao unanifikisha haswaa kutokana na mashairi yake na sauti yake, lakini wapeni na wengine nafasi kwa kuwatengenezea filamu na mambo mengineyo.

Ona mlivyotaka kumuua bibi wa watu kwa kutaka kumpandisha jukwaani ilhali akiwa amefanyiwa upasuaji wiki mbili kabla ya tamasha. Hivi angefia pale jukwaani mngesema mnamuenzi au? Hiyo si sanaa na huko si kumuenzi bibi huyo.

Hofu yangu ni pale baadhi ya watu wanapopotosha maudhui ya tamasha hilo na kuligeuza kama ni sehemu ya Picnic huku wakisahau kuwa ile ni sehemu ya darasa kwa wasanii wetu.

Tusiliache tamasha hili likahodhiwa na baadhi ya watu wanaoona kuwa wakati umefika wa kwenda kufanya mambo yao binafsi huku wakiwanyima nafasi wahusika na walengwa.

Vinginevyo mtaendelea kuonekana kuwa mnaenda kuwafanyia kero tu Wazanzibari na kuwachafulia mji wao kisha hakuna faida yoyote wanayoipata zaidi ya kuwafaidisha wamiliki wa mahoteli pekee kutokana na wageni kufurika kwa kipindi cha tamasha hilo.

Nionavyo mimi, wakati umefika kwa waandaaji wa tamasha kujipanga upya na kuacha kuandaa tamasha linalowapa fursa watu kwenda kula pilau la samaki pale Forodhani.

Tamasha la Sauti za Busara lilifanyika Zanzibar katika viunga vya Ngome Kongwe kuanzia Februari 9 hadi 14, mwaka huu.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.