Rais Jakaya Kikwete ameongoza mamia ya watu waliojitokeza kuuaga mwili wa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu, marehemu Melkizedeck Sanare aliyefariki mwishoni mwa wiki iliyopita.
Shughuli ya kuuaga mwili wa marehemu Sanare ilitanguliwa na Ibada ya mazishi iliyofanyika jana asubuhi kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Azania Front Jijini Dar es Salaam.
Mbali na Rais Kikwete, viongozi wengine wa kitaifa waliohudhuria shughuli hiyo ni Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa na mawaziri kadhaa.
Baada ya Ibada hiyo, Bw. Simon Sayore alisoma wasifu wa marehemu Sanare na kufuatiwa na maelezo mafupi kutoka Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) alipowahi kufanya kazi akiwa Kamisha Mkuu.
Pia maelezo mengine yalitolewa na ofisi ya Waziri Mkuu na kutoka katika familia yake.
Mwili wa marehemu Sanare ulisafirishwa hadi uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa ajili ya safari ya kwenda kijijini Bangata mkoani Arusha atakapozikwa leo.
Marehemu Sanare aliyekuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo na kupooza kwa muda mrefu alifariki katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.