Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Serikali bado yang'ang'ania kupinga mgombea binafsi
http://www.habaritanzania.com/articles/2997/1/Serikali-bado-yang'ang'ania-kupinga-mgombea-binafsi
By Habari Tanzania
Published on 02/16/2007
 

MPANGO wa serikali kukata rufaa kupinga hukumu ya kesi ya kikatiba ya kuruhusu wagombea binafsi katika uchaguzi umeiva na sasa itawasilisha hati yake ya rufaa ndani ya siku 60 kuanzia mwezi huu.


Na Ramadhan Semtawa

MPANGO wa serikali kukata rufaa kupinga hukumu ya kesi ya kikatiba ya kuruhusu wagombea binafsi katika uchaguzi umeiva na sasa itawasilisha hati yake ya rufaa ndani ya siku 60 kuanzia mwezi huu.

Hatua hiyo inatokana na notisi ya serikali ya azma ya kutaka rufaa kujibiwa na Mahakama ya Rufaa wiki iliyopita.

Kutokana na hali hiyo, kinachoonekana sasa ni serikali kujipanga kikamilifu kuhakikisha ikiingia mahakamani haibwagwi tena kama mwaka 1994 na mwaka jana.

Msimamo huo wa serikali utolewa siku mbili tu tangu tangu wanaharakati wa muungano wa baadhi ya asasi zisizo za kiserikali (FemAct) kutoa msimamo wa kutaka uchaguzi mdogo wa jimbo la Tunduru ufanyike baada ya kuandaa utaratibu wa kuruhusu kuwapo kwa wagombea binafsi kama ilivyoamriwa na Mahakama Kuu Mei 5, mwaka jana.

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jonson Mwanyika, alisema inachofanya serikali sasa ni kujiandaa kwa kusoma kwa kina hati ya uamuzi wa Mahakama Kuu kuamuru wawapo wagombea binafsi kabla ya kuamua kuwasilisha hati ya rufaa.

Mwanyika alisema rufaa kama hiyo inahitaji maandalizi na si kitu cha kukurupuka kwani ni lazima hati ya rufaa iendane na maamuzi yaliyomo ndani ya hukumu.

"Tunapaswa kukata rufaa ndani ya siku 60, sasa hivi tunafanya utafiti kwa kupitia kwa kina hati ya uamuzi wa Mahakama Kuu ili tutakachokiwasilisha kisiwe nje ya uamuzi," alisema Mwanyika.

Hata hivyo, alipoulizwa zaidi ni lini hasa serikali inategemea kuwasilisha hati hiyo ya rufaa alijibu; "Kwa kuwa tunatakiwa kukata rufaa ndani ya siku 60, hata kama tukiwasilisha kabla ya siku mbili ni sawa."

Alisema katika hati hiyo serikali itaeleza kwanini inaamua kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu na kwanini haikubaliani na kuwepo wagombea binafsi nchini.

Kuhusu msimamo wa FemAct, alisema
uamuzi wa Mahakama Kuu umeelekeza kuwepo na wagombea binafsi katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa 2010 na si uchaguzi mdogo.

Mei 5, mwaka jana jopo la Majaji watu wa Mahakama Kuu, Amir Manento, Salum Massati na Thomas Mihayo, lilitoa uamuzi wa kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, ya kuitaka itamke kuruhusu wagombea binafsi katika uchaguzi.