Na Salma Said, Zanzibar
MWANDISHI wa habari wa siku nyingi wa Zanzibar, Mohammed Ali Nabwa (71) amefariki dunia.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kutoka kwa ndugu wa karibu wa marehemu, Nabwa alifariki alfajiri ya kuamkia jana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa.
Mwili wa marehemu Nabwa uliwasili kwa boti ya Sea Bus kwenye Bandari ya Zanzibar saa 7:00 mchana ukitokea Dar es Salaam.
Kwenye bandari hiyo, umati wa watu ulifika kwa ajili ya kupokea mwili huo na kujumuika na ndugu na jamaa za marehemu katika maombolezo.
Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Ali Juma Shamhuna, alikuwa mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar waliofika bandarini hapo.
Shamhuna ambaye pia ni Naibu Waziri Kiongozi, ameoa nyumba moja na marehemu Nabwa.
Kiongozi mwingine wa serikali aliyehudhuria mapokezi hayo bandarini ni Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, aliyejumuika na wananchi wa kawaida kuupokea mwili wa marehemu.
Wakati wa uhai wake, Nabwa aliwahi kufanya kazi kwa miaka kadhaa katika Serikali zote mbili, akianzia na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambako mwaka 1988
aliteuliwa kuwa mwandishi wa hotuba za Waziri Kiongozi, Dk Omar Ali Juma.
Baada ya Dk Omar kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Benjamin Mkapa katika uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa mwaka 1995, Nabwa aliendelea kuwa msaidizi wa Dk Omar Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mwaka 2003, Nabwa alipata kazi ya kuwa Mhariri Mtendaji wa gazeti jipya la binafsi la Dira, lililokuwa likimilikiwa na kampuni ya Zanzibar International Media
Co (Zimco) ya mjini hapa.
Aliwahi kunyang'anywa uraia wa Tanzania kwa madai kuwa ni raia wa Comoro. Mvutano huo na serikali uliendelea mpaka mwishoni mwa mwaka jana alipoandikiwa barua rasmi na Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa ni raia halali.
Maziko ya marehemu yalifanyika Kiembesamaki, nje kidogo ya mjini hapa, baada ya mwili wake kusaliwa kwenye Msikiti wa Mabati, Kisimajongoo