Na Mwasu Sware.
SHIRIKA la Biashara na Maendeleo la Marekani limetoa kiasi cha Sh401 milioni kwa Kampuni ya Sukari ya Kilombero ili kuiwezesha kutumia taka kuzalisha umeme.
Akizungumza na waandishi jana, Balozi wa Marekani nchini, Michael Retzer, alisema umeme utakayozalishwa utatumika katika uendeshaji wa kiwanda hicho na kuchangia kwenye gridi ya Taifa.
Retzer alisema hivi karibuni Kampuni hiyo inatarajiwa kuanza kuzalisha ethani (ethanol) inayotokana na taka kwa ajili ya kuuza katika soko la nje.
"Hivi sasa kampuni ya Sukari itaanza kuzalisha ethani kwa ajili kuuza katika soko la nje, hivyo tatizo la wapi taka hizo zipelekwe litakuwa limeepukika na uzalishaji wa kiwandani utaimarika na kiwango cha uzalishaji wa nishati kitaongezeka," alisema Retzer.
Alisema teknolojia mpya ya uzalishaji wa ethani kutoka kwenye taka na uzalishaji wa nishati ya umeme zitajenga mustakabali wa usimamizi mzuri wa kutunza mazingira na kuimarisha uchumi.
Naye Meneja wa Kiwanda cha Sukari Kilombero, Dave Coates, alieleza kuwa kutokana na msaada huo, kiwanda kitaweza kuzalisha kwa uhakika na kuinua uchumi wa nchi.
Coates alisema, kiwanda hicho kama kikizalisha vizuri, kitachangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa uchumi wa nchi, kuongezeka kwa ajira na wakulima wa miwa kupata soko la urahisi kwa bidhaa zao.
Alisema kwa sasa kiwanda hicho kina takribani wafanyakazi 5,000 na wakulima wapatao 7000 ambao wanawategemewa na kiwanda hicho katika uzalishaji wa Sukari.