Na Muhibu Said
MUFTI wa Tanzania, Sheikh Mkuu, Issa bin Shaban Simba, amelifumua Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kwa kuwavua nyadhifa wakurugenzi wake wote, akiwamo Mkurugenzi wa Dini, Sheikh Suleiman Gorogosi.
Mbali na kuwavua nyadhifa hizo, Mufti Simba amefuta pia kurugenzi zote za makao makuu ya Bakwata na kuunda Mfumo Mpya wa Utendaji na kuwaagiza viongozi hao kukabidhi ofisi na majukumu yao kwa Kaimu Katibu Mkuu wa baraza hilo, Sheikh Hassan Luambano.
Kurugenzi zilizokuwa Bakwata ambazo sasa zimefutwa ni pamoja na Utawala, Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Habari, Uhusiano na Mambo ya Nje, Afya, Maendeleo ya Jamii, Wanawake, Vijana, Watoto na Wazee, Dini na Usalama.
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata (NEC), Sheikh Khamis Mataka, alisema jana kuwa, kuanzia Februari 14, mwaka huu, Bakwata haitakuwa tena na cheo cha Mkurugenzi na kwamba wakurugenzi wote waliovuliwa nyadhifa hizo, wataendelea kuwa wafanyakazi wa baraza wakisubiri maelekezo juu ya majukumu yao mapya.
Sheikh Mataka, ambaye pia ni Kamishna wa Tume ya Mufti ya Kuchunguza Mali za Waislamu, alisema uamuzi huo ulitangazwa na Mufti kwenye kikao na wakurugenzi hao kilichofanyika ofisini kwake, jijini Dar es Salaam juzi, ambako aliwaeleza pia kuhusu azma yake ya kutaka kuunda mfumo mpya wa utawala.
Alisema uamuzi huo wa Mufti, ni katika mchakato wa kujipanga upya kwenye baraza kwa ajili ya kuutumikia Uislamu na Waislamu na kujenga njia ya maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Mbali na Sheikh Gorogosi, wakurugenzi wengine waliovuliwa nyadhifa hizo, ni Mohamed Mvogogo aliyekuwa Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na pia Kaimu Mkurugenzi wa Utawala.
Wengine, ni Ustadh Suleiman Lolila aliyekuwa Mkurugenzi wa Afya na Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Uhusiano na Mambo ya Nje, Maendeleo ya Jamii, Wanawake, Vijana, Watoto na Wazee, Sheikh Twaha Majaliwa aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa Dini na Ramadhan Samamba aliyekuwa Mkurugenzi wa Usalama.
Hata hivyo, hatua hiyo imezusha maswali mengi kuhusu nani atakayeshughulikia kesi za talaka, ndoa na mirathi ambazo zimekuwa zikiendeshwa kwenye ofisi ya Kurugenzi ya Dini chini ya Sheikh Gorogosi na Naibu wake, Sheikh Twaha.
Hatua hiyo imechukuliwa wiki mbili tangu Mufti alipofanya mabadiliko ndani ya Bakwata kwa kuwateua viongozi mbalimbali, akiwamo Sheikh Mataka kuwa Mwenyekiti wa NEC badala ya Alhaj Habib Ndassiwa aliyekuwa akishika wadhifa huo.
Wengine, ni Sheikh Luambano aliyeteuliwa kukaimu nafasi ya Katibu Mkuu iliyoachwa wazi kutokana na kufukuzwa kazi kwa aliyekuwa Katibu Mkuu, Ustadh Abbas Kihemba, Mohamed Khamis (Kaimu Naibu Katibu Mkuu-Dini) na Ramadhan Sawaka (Naibu Katibu Mkuu-Utawala), wakiwa wote wapya ndani ya Bakwata kwa kushika nafasi muhimu za uongozi wa juu.